TUMEMSIKIA MSUVA, TUNAMTARAJIA STARS

Dimba - - Jumatano -

W AKATI timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) ikielekea katika mpambano wake mkali dhidi ya Botswana, siku ya Jumamosi, wadau wa mchezo wa soka wanazidi kupata faraja kufuatia mafanikio anayoendelea kuyaonyesha winga wa Tanzania, Simon Msuva, anayecheza katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco.

Stars na Botswana zinacheza mchezo wa kirafiki uliomo katika kalenda ya nchi wanachama wa Shirikisho hilo, ambapo miongoni mwa wachezaji wanaocheza nje walioingia kikosini ni pamoja na Msuva.

Kadhalika nahodha Mbwana Samatta, anayekipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji naye ni miongoni mwa wachezaji watakaokuwamo katika kikosi hicho, kwa mujibu wa majina yaliyotajwa na kocha mkuu, Salum Mayanga.

Katika mchezo huo, Stars ina matarajio ya kushinda kihistoria na hata kwa uwezo, kwani kikosi hicho kimezidi kuimarika na hasa kutokana na kuwapo kwa wachezaji kadhaa wenye uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

Sisi DIMBA tunafahamu kwamba, wachezaji waliopewa nafasi hiyo wataitendea haki kwa kucheza kwa kujituma zaidi na kuleta ushindi, kwani wanatambua deni walilonalo kwa Watanzania kufuatia kutolewa katika michuano ya Chan.

Tuna imani kubwa na kikosi cha Mayanga, lakini tuna imani maalumu kwa wachezaji wetu Msuva na Samatta, ambao kwa uzoefu walioupata wanaweza kuwaongoza wenzao kupata ushindi Jumamosi.

Ni matumaini yetu kwamba, Tanzania sasa inakaza buti ili kuhakikisha lile jina la Kichwa cha Mwendawazimu linapotea na kuja zuri linaloashiria ubabe katika soka la Afrika.

DIMBA tuna imani na wachezaji walioitwa na Mayanga, uongozi mpya wa TFF pamoja na Watanzania ambao wanatambua umuhimu wa kuiunga mkono timu yao pale inapocheza katika viwanja vya nyumbani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.