Sare zatawala VPL

Dimba - - Jumapili - MAREGES NYAMAKA

MATOKEO ya sare yalionekana kutawala vilivyo jana, katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa viwanja mbalimabali, akiwamo bingwa mtetezi, Yanga mbele ya Mtibwa Sugar, isipokuwa mchezo mmoja pekee kati ya saba iliyochezwa.

Kinara wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar, alifanikiwa kumbana Yanga uwanja wake wa nyumbani, Uhuru, Dar es Salaam, mchezo ukimalizika kwa suluhu kama ilivyokuwa kwa Majimaji mbele ya Kagera Sugar.

Azam, ambayo ilikuwa haijaruhusu bao katika michezo minne iliyopita, ilijikuta ikitanguliwa kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao, Singida United, kabla ya kinda Paul Peter, aliyeingia kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 88 na mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Mbao FC wakiwa kwenye dimba lao la CCM Kirumba, waliambulia pointi moja kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, matokeo kama hayo yakiwakumba pia Ruvu Shooting mbele ya Njombe Mji, huku Mwadui na Mbeya City mechi ikimalizika kwa mabao 2-2.

Ni Uwanja wa Nangwanda Sijaona wa mkoani Mtwara pekee uliokuwa na matokeo ya ushindi, ambapo wenyeji Ndanda waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.