Suluhu Yanga vs Mtibwa si bure

Dimba - - Mbele - SAADA SALIM NA CLARA ALPHONCE

SULUHU ya 0-0 waliyoipata Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar, inatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wachezaji wao muhimu kuwa majeruhi na kushindwa kucheza katika kiwango chao cha kawaida.

Yanga jana ilijikuta ikiambulia suluhu hiyo mbele ya wakata miwa hao, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, na kuwafanya mashabiki wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kuondoka vichwa chini.

Mshambuliaji kama Amis Tambwe, ambaye katika misimu iliopita alikuwa akifunga mabao mengi, mpaka sasa hajacheza mchezo wowote katika michezo mitano waliyokwisha kucheza, kutokana na majeraha yanayomsumbua, licha ya kwamba ameanza mazoezi mepesi.

Mbali na Tambwe, mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye alikuwa akiogopwa sana na mabeki wa timu pinzani, kwa sasa anaonekana kutokuwa na makali yoyote, hiyo ikitajwa kusababishwa na majeraha ya tangu msimu uliopita ambapo inaonekana bado hajarudi kwenye kiwango chake.

Ngoma alishindwa kucheza baadhi ya michezo ya mzunguko wa pili msimu uliopita kutokana na majeraha hayo, huku pia Obrey Chirwa naye akiingia kwenye mkumbo huo wa kuwa majeruhi, ambapo alikosa michezo miwili ya Ligi ilipoanza.

Mbali na hao, pia yupo Geofrey Mwashiuya na kipa Beno Kakolanya, ambao pia wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha, huku kiungo Thaban Kamusoko, naye siku za hivi karibuni, akiumia, ikabidi jana aingizwe kipindi cha pili.

Katika hatua nyingine, wachezaji wa Yanga, jana walijikuta wakiwa kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki wao kukerwa na kitendo cha suluhu hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar, kitu kilichosababisha watoke uwanjani chini ya ulinzi mkali, tena gari likiwafuata uwanjani. Mbali na hivyo, viongozi wa Yanga pamoja na wale wa benchi la ufundi walikataa katakata kuzungumza na waandishi wa habari na kuondoka uwanjani kimyakimya. Yanga jana iliwakilishwa na: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vicent ëDanteí, Kelvin Yondani, Said Juma, Pius Buswita, Rafael Daudi/Geofrey Mwaishuya, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/ Thaban Kamusoko na Ibrahim Ajib.

Mtibwa: Benedict Tinocco, Salum Kanoni, Issa Rashid 'Baba Ubaya,' Dickson Daud, Kassim Ponela, Shaban Nditi, Salum Kihimbwa/Henry Joseph, Mohamed Issa, Stamilii Mbonde, Hassan Dilunga/Kelvin Kongwa na Ally Makarani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.