FOMESHENI MPYA YA MABAO YAIVA YANGA

Dimba - - Mbele - NA MAREGES NYAMAKA

YANGA imeanza vibaya kampeni ya kulitetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo baada ya kucheza mechi tano imejikuta ikishika nafasi ya sita, ikizidiwa na Simba, Mtibwa Sugar, Azam FC, Singida United na Prisons ya Mbeya, lakini kama kuna timu zinaichukulia poa, basi zinaweza kuumia.

Safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ilianza kwa kusuasua kutokana na uhaba wa mabao, lakini benchi la timu hiyo limeshtuka na sasa linakuja na fomesheni mpya ya mabao ambayo itakuwa mwarobaini wa ushindi.

Wanajangwani hao mwishoni mwa wiki waliambulia suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na kuwafanya kufikisha pointi tisa, mbili nyuma ya vinara, Simba.

Kitendo hicho cha kutoka sare na Mtibwa wakishindwa kabisa kuzionja nyavu za wapinzani, kimelifanya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha George Lwandamina kuivalia njuga safu ya ushambuliaji na kubadili fomesheni.

Fomesheni mpya ya mauaji kwa wapinzani ambayo itaanzia kwa Kagera Sugar Oktoba 14 ni ya 4-2-3-1, ambayo itamjumuisha straika wa timu hiyo, Amis Tambwe, aliyerejea kikosini, ikiwa ni baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha yake ya nyama za paja.

Mabeki wa timu hiyo ambao wameruhusu mabao mawili pekee katikati watasimama Kelvin Yondani na Andrew Vicent 'Dante', kulia Juma Abdul, kushoto Gadiel Michael, huku nafasi ya viungo wawili ikiwahusu Papy Kabamba Tshishimbi na Thaban Kamusoko.

Juu yao watasimama wanaume watatu ambao ni Ibrahim Ajib, Donald Ngoma na Geofrey Mwashiuya, huku mbele akisimama mchana nyavu Amis Tambwe, ambaye ana wastani mzuri wa kupiga mpira ya vichwa sambamba na inayokuwa imezagaa eneo la hatari.

Meneja wa kikosi hicho, Hafidh Saleh, aliliambia DIMBA Jumatano kuwa, kuanzia sasa timu yao hakuna kulala, kwani wanaendelea na mazoezi makali kwenye Uwanja wa Polisi, ulioko Barabara ya Kilwa, licha ya wachezaji kadhaa kuwa kwenye kikosi cha Taifa, Taifa Stars, akiwamo Ajib.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.