YANGA YAICHONGEA MTIBWA KWA SIMBA

Dimba - - Mbele - NA CLARA ALPHONCE

KUREJEA uwanjani kwa mshambuliaji Amis Tambwe kutakuwa kumemshusha pumzi Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ambaye sasa atakuwa na uhakika wa kuvuna mabao kupitia krosi za beki wake wa kushoto, Gadiel Michael.

Tambwe amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi, akiwa amezikosa mechi zote tano za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo timu yake hiyo imecheza, ukiwamo mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, Agosti 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa kipindi chote ambacho Tambwe amekuwa nje ya uwanja, Lwandamina na mashabiki wa Yanga walishuhudia krosi lukuki zilizokuwa zikichongwa na Gadiel kutoka winga ya kushoto, Juma Abdul (kulia) na wengineo, zikipotea kwa kukosa watu wa kuziunganisha.

Kati ya krosi lukuki zilizotengenezwa na mawinga na mabeki wa pembeni na wa kati wa Yanga, ni tatu tu zilizozaa mabao kupitia kwa Donald Ngoma dhidi ya Lipuli Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na walipovaana na Majimaji ugenini, huku lingine likiwa ni lile lililofungwa na Ibrahim Ajib, walipoichapa Ndanda FC bao 1-0 Uwanja wa Uhuru, akitumia krosi ya Kelvin Yondani.

Watu wa Yanga wanaamini iwapo 'mzee wa mipira ya vichwa,' Tambwe asingekuwa majeruhi, timu yao isingekuwa na mabao manne tu hadi sasa ndani ya mechi tano za Ligi Kuu Bara.

Na kuonyesha jinsi Tambwe alivyokerwa na hali hiyo ya ukame wa mabao, hasa jinsi wenzake walivyokuwa wakishindwa kuzitumia vema krosi, ameanza kufanyia kazi hilo kupitia mazoezi ya timu hiyo, yaliyofanyika tangu juzi na jana.

Katika mazoezi hayo, Tambwe alionyesha umahiri wake wa kucheka na nyavu kupitia mipira ya krosi zilizokuwa zikichongwa na Gadiel, Abdul na wengineo, hali iliyoanza kumpa matumaini Lwandamina kujiandaa kushangilia mabao.

Gadiel, ambaye tangu ametua Yanga amekuwa akicheza kwa kujituma mno, alikuwa akichonga krosi murua ambazo mara nyingi zilikuwa zikitua katika kichwa cha Tambwe na mkali huyo wa Burundi kutikisa nyavu kadri alivyotaka.

Kutokana na kile kinachoendelea kwa sasa kwenye mazoezi ya Yanga, ni wazi kuwa umoja wa Gadiel na Tambwe unaweza kuwa neema kwa wapenzi wa timu hiyo iwapo wawili hao wataendelea kushirikiana kama wanavyofanya mazoezini, kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara na zile za kimataifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.