Yanga yaichongea Mtibwa kwa Simba

Dimba - - Jumatano - NA SAADA SALIM

SIMBA ni wajanja sana. Benchi la ufundi la timu hiyo liliitumia vema siku ya Jumamosi iliyopita kutulia kwenye luninga kwa ajili ya kuwasoma Mtibwa Sugar, wakati ikicheza na Yanga Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo imewafanya vigogo hao wa benchi la ufundi kugundua mapungufu yao na kuhakikisha wanayafanyia kazi kabla ya kukutana nao Oktoba 15, mwaka huu, kwenye uwanja wa Uhuru.

Simba ipo Dodoma na itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu yenyeji wa mkoa huo, Dodoma FC, ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza, ikiwa chini ya kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio.'

Kocha wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa wamewasili salama Dodoma na watacheza mchezo huo wa kirafiki kujipima nguvu kabla ya kuvaana na Mtibwa Sugar.

Alisema Mtibwa ni timu nzuri, ina wachezaji vijana, lakini wao wamejiandaa vizuri, huku vijana wake wakiahidi kutomwangusha katika mchezo huo ambao utakuwa wa ushindani mkubwa.

"Nimewaona Mtibwa, wana vijana wazuri, pia wanajivunia kuwepo kwa wachezaji waliotoka katika kikosi cha timu hiyo ambao tunawafahamu, lakini tutacheza kwa umakini kuhakikisha hawaondoki na ponti katika uwanja huo," alisema.

Omog alisema anaifahamu vizuri Mtibwa, ameiona tangu msimu uliopita na msimu huu ikiwa inacheza, lakini anaingia kwa tahadhari kuhakikisha hawafanyi makosa waliyoyafanya mahasimu wao, Yanga na kutoka nao sare.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.