Dk. Bendera aagiza timu zisajiliwe

Dimba - - Jumatano - NA ELIYA MBONEA

VIONGOZI wa Chama cha Soka mkoani Manyara, wametakiwa kusajili timu zote zilizoshiriki mashindano ya michuano ya Chemchem Cup iliyolenga kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori na kupiga vita ujangili.

Wito huo ulitolewa juzi mjini hapa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera ambaye kitaalamu ni kocha wa mpira wa miguu wakati alipokuwa akikabidhi vikombe na zawadi kwa timu 23 zilizoshiriki mashindano hayo.

Dk. Bendera alisema michuano ya Chemchem Cup yanaipa hadhi mashindano hayo yenye lengo la kuhifadhi wanyamapori kwenye maeneo ya hifadhi ya jamii ya Burunge.

“Nimshukuru sana Mkurugenzi wa Chemchem Foundation, Nicolaus Negre na watendaji wengine kwa kuanzisha mashindano hayo,” alisema Dk. Bendera na kuongeza:

“Naagiza timu hizi zilizoshiriki mashindano haya, viongozi wa soka Mkoa wa Manyara fanyeni haraka kuzisajili ili kuwezesha mashindano haya kuwa ya kudumua.”

Akizungumza wakati wa kutoa zawadi, Negre alitaja malengo ya mashindano hayo kuwa ni kuhamasisha uhifadhi na kupiga vita ujangili.

“Kama mkitaka tuendelee na mashindano haya, lazima tupambane na majangili ili wageni waendelee kuja kwenye maeneo yetu ya hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge,” alisema Negre.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.