Wakenya, Waganda, Wacongo kupimana ubavu Bongo Movie

Dimba - - Jumatano - NA MWANDISHI WETU

WAIGIZAJI wa filamu kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, watachuana na wenzao wa Bongo Movie katika kuwania tuzo maalumu za Sinema Zetu, 'Sinema Zetu International Film Festival,' zinazoandaliwa na Kampuni ya Azam Media.

Mratibu wa tamasha hilo, Zamaradi Nzowa, amesema tuzo hizo ambazo kilele chake kitafanyika Aprili 1 mwakani, zitatolewa kwa filamu bora, makala bora, waigizaji bora wa kike na wa kiume, waandaaji bora, muziki bora pamoja na wapiga picha bora.

Kwa mujibu wa Zamaradi, lengo la tamasha hilo ni kukuza, kuthamini kazi za wasanii na maslahi yao pamoja na kukuza lugha adhimu ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, aliongeza kuwa tamasha hilo linalotarajia kufanyika kuanzia Januari mosi mwakani, litaanza katika mchakato wa kukusanya sinema na tamthilia kutoka kwa waigizaji wa mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na nje ya nchi kuanzia sasa hadi Novemba 30, mwaka huu, ambapo mwezi Desemba wataanza rasmi kuchuja filamu kwa ajili ya kupata filamu zitakazoingia katika kinyang’anyiro cha tuzo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa tamasha hilo, Jacob Joseph, alisema wanatarajia kushirikiana na wadau kutoka mikoani kwa ajili ya kwenda kuonana na wadau wa filamu pamoja na kutoa elimu na kujenga uelewa juu ya tamasha hilo pamoja na kukusanya kazi zao.

Naye Profesa Martin Mhando ambaye atakuwa msimamizi wa majaji wa tamasha hilo, ameeleza kuwa hakutakuwa na upendeleo kwa mtu yeyote na kwamba, ubunifu na utayarishaji bora ndiyo msingi wa filamu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.