OKTOBA MOSI SASA KUITWA KICHUYA

Dimba - - Jumatano - NA SAADA SALIM

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya, ameandika rekodi ya kuwa mchezaji mwenye bahati na mwezi Oktoba kwa misimu miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Unajua kwanini ana nyota inayowaka na mwezi huo, hebu fuatilia rekodi hii ndipo utajua kweli Kichuya mzaliwa wa Morogoro na hakuja Dar es Salaam kutazama maghorofa, bali kucheza soka.

Oktoba mosi msimu uliopita wa Ligi Kuu, Kichuya akiwa na kikosi cha Simba alifanikiwa kuisawazishia bao timu hiyo katika mchezo dhidi ya mahasimu wa jadi kisoka Yanga, ambapo mechi ilimalizika kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kichuya alifunga bao hilo muhimu zikiwa zimesalia dakika tatu kabla ya mchezo kuisha, kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakiamini siku mbaya ilikuwa imeangukia kwao.

Aidha, Oktoba mosi mwaka huu, Kichuya alifunga bao la kusawazisha kama hilo katika mchezo dhidi ya Stand United, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga, Kichuya alifunga bao hilo lililowapa furaha mashabiki wa timu hiyo na kuamua kumpachika jina Oktoba Mosi.

Mashabiki hao waliozungumza na gazeti hili walieleza kwamba, Oktoba mosi imekuwa ni siku ambayo Kichuya amekuwa akiwapa furaha kwa kufunga mabao ya kusawazisha kitu ambacho kwao ni faraja kubwa.

Walieleza watakuwa wakiadhimisha kila Oktoba mosi kwa kuiita 'Kichuya Day' kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku ya 'Simba Day'.

Winga huyo amekuwa akisaidia timu yake hiyo katika mazingira magumu na kuhitaji ushindi au pointi muhimu, hali inayomfanya kila siku mashabiki wa Simba kumuona almasi katika klabu yao.

Kichuya ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri akiwa Mtibwa Sugar, ambapo Simba ilisajili na kiwango chake kinazidi kuimarika kila siku. Kwa uwezo mkubwa wa kandanda winga huyo amefanikiwa kulishawishi benchi la ufundi kuendelea kumwamini na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Kichuya

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.