Raphael Daudi ‘itupe Biblia’ jivishe utumwa

Dimba - - Special -

RAPHAEL Daud ni mchezaji na nusu. Jamaa ni fundi wa mpira. Kuuzungumzia ubora wake kwa kuufupisha na jamii ikakuelewa ni kusema anajua mpira. Ukisema hivyo inatosha sana kuliko kuongeza mambo mengine.

Ni zamani kidogo kuona kiungo mtaratibu wa namna hii akicheza Yanga. Eneo la Daud aliwahi kutamba Athuman Iddy ‘Chuji’, Godfrey Bonny ‘Ndanje’, Juma Seif ‘Kijiko’ na wengineo.

Licha ya ubora mkubwa kutamalaki kwenye miguu yake, mwenyewe anaonekana hapendi papara wala soka la kuminyana, kugombania mipira. Hajali vileIaNnIaEvSyToAcheza.

Anaingia uwanjani kuufanya mpira anavyotaka na mpira unabaki kumtii. Juu ya ubora wote alionao anaikosa ladha moja tu. Anakosa ladha ya uchizi wa soka.

Nimemtazama katika jezi za Mbeya City, timu ya taifa na sasa namtazama kwa karibu zaidi akiwa na jezi za Yanga. Namwona ni yule yule, anayepiga mpira mwingi, lakini akikosa uchizi wa soka kama walionao viungo wengine.

Amepoa sana uwanjani. Anacheza kinyonge. Katika eneo lake linalochezwa na watu wa kazi kama Himid Mao, James Kotei, naye alipaswa kucheza kwenye mizani hiyo.

Wakati mwingine ubora pekee hautoshi kulitawala eneo la kiungo na kuogopwa na viungo wa upinzani. Daud ni kiungo mahiri, lakini anazimwa na upole wake na viungo wa kawaida ambao hawafikii hata robo ya ubora alionao.

Siku moja Himid aliwahi kuniambia sifa ya mchezaji wa kiungo. Aliitaja sifa hiyo kuwa ni ujasiri, baadaye ndiyo akaniambia ubora.

Katika hali hii ambayo Daud anacheza kama mchungaji aliyeshika Biblia na kusoma mistari yake na waumini kumsikiliza, anafuaje dafu kwa viungo aina ya Himid?

Nafuu ya Daud msimu huu ni kucheza timu moja na Pappy Kabamba Tshishimbi. Lakini kama angebaki Mbeya City na Tshishimbi Yanga, wangekutana kati tungejiridhisha kuwa Daud kiungo wa kawaida, kumbe tunajidanganya bila kujua.

Daud anapaswa kufahamu umahiri pekee haumfanyi ahesabike kama moja ya viungo mahiri wa wakati huu. Simfundishi utovu wa nidhamu, lakini kwa anavyocheza abadilike kutokana na mahitaji ya eneo analocheza.

Mwaka 2014, Stars ilicheza ugenini dhidi ya Ivory Coast na kulilitawala vyema eneo la kiungo. Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto waliwafanya kila kitu wakina Cheikh Tiote (Hayati), lakini muda ambao Tiote na wenzie walitaka kufika langoni mwa Stars walifika na mwisho wa mchezo Stars ikalala 2-0.

Bila kujijua na kocha wetu Kim Poulsen siku ile Stars, tuliweka vijana wengi wa kukaa na mpira na kuliko kuukimbiza mpira. Daud anaingia katika kundi hili.

Aina yake ya uchezaji inamvutia kila kocha na shabiki atamani avae jezi ya timu yake, lakini kuna muda havutii hasa kwenye mechi iliyojaa vurugu na ubabe kwenye eneo la kiungo.

Daud ajifanyie tathmini kando ya pasi zake za mwisho na mabao yaliyomtoa Mbeya City na kumleta Yanga. Ndani ya muda mfupi ataona anachopaswa kukifanya atakapokutana na wanaume aina ya Himid.

Himid anacheza soka la shoka. Anajitoa sana uwanjani kana kwamba hatacheza tena mechi nyingine. Kusuguana na mwanadamu wa namna hii, hakuhitaji ubora pekee, kunahitaji nawe ucheze kama yeye au robo ya kile anachokifanya ndio rahisi kumzima.

Katika viungo wa sasa sijaona kiungo wa kumzima Himid kirahisi. Si kama Himid anajua sana mpira. Anatimiza vyema majukumu ya kiungo anavyotakiwa kuwa.

Ni muda wa Daud kujiongeza na kubadilika aina yake ya mchezo kwa mahitaji ya nafasi yake uwanjani. Mzamiru Yassin wa Simba ni aina ya mchezaji kama Himid.

Mzamiru anazunguka sehemu kubwa ya uwanja na kuwafanya wakina Okwi, Niyonzima wawe huru. Kiungo ni lazima uminyane, ugongane na uwe na uwezo wa kuishinda mipira unayokwenda kugombania na kiungo mwenzio. Kama kiungo akiwa hawezi kufanya kazi hizi basi awe na kipaji maridhawa kama cha Andres Iniesta. XAVI

WENGER

Siku moja Himid aliwahi kuniambia sifa ya mchezaji wa kiungo. Aliitaja sifa hiyo kuwa ni ujasiri, baadaye ndiyo akaniambia ubora.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.