BADO KUNA MWENYE MASHAKA NA GUARDIOLA?

Dimba - - Special - NA EZEKIEL TENDWA

KWA hali ilivyo katika Ligi Kuu nchini England, mtu yeyote atakayejitokeza na kusema ubingwa utatua katika Jiji la Manchester, wala asilaumiwe maana atakuwa ameona mbali.

Ni kweli kwamba ligi bado ni mbichi sana kwani ni michezo saba tu iliyokwisha kuchezwa kwa kila timu, lakini wahenga waliosema ‘Nyota njema huonekana asubuhi’ hawakuwa wendawazimu hata kidogo.

Waliosema hivyo waliona mbali, wanajua kwamba siku zote ukiianza safari yako kwa mafanikio utaimaliza kwa mafanikio, achana na wale wengine waliosema ‘raha ya mbio ni kumalizia’.

Nani anaweza kuziondoa timu za Jiji la Manchester kwenye mbio za ubingwa? Nani huyo? Atakuwa anaujua mpira kweli? Hapana! Huyo itabidi aangaliwe mara mbilimbili.

Timu kama Manchester United na City, ndizo timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu achilia mbali Chelsea, ambao ni mabingwa watetezi wanaojaribu kupambana kuhakikisha hawapotezi heshima yao hiyo.

Manchester United inayonolewa na Jose Mourinho, ipo kwenye moto mkali sambamba na majirani zao Manchester City, inayonolewa na Mhispaniola, Pep Guardiola.

Hata hivyo, kabla ya ligi kuanza watu walikuwa na mashaka na kikosi cha Guardiola kutokana na jinsi alivyofanya usajili wa wachezaji wengi hapo ndipo wengi wakadhani kwamba hataweza kuiunganisha timu yake mapema.

Wengi walikuwa wakiipa nafasi kubwa Manchester United na kwa kweli hawajakosea lakini waliinyima heshima yake City na sasa Guardiola, anawaumbua mchana kweupe bila chenga.

Ligi imeanza na Guardiola kaanza na kasi ya ajabu kutokana na vipigo wanavyovitoa kwa kila timu inayojipendekeza mbele yao na sasa wanaogopwa hujapata kuona.

Katika msimamo wa Ligi Kuu nchini humo, wamejikusanyia jumla ya pointi 19, wakiwa hawajapoteza mchezo wowote, lakini kubwa ni kandanda la kuvutia wanalolicheza.

Awali wakati kocha huyo alipokuwa akiifundisha Barcelona, baadhi yetu tulidhani hana lolote na badala yake anatembelea nyota ya mtangulizi wake.

Alipata mafanikio makubwa akiwa Barcelona kama kocha lakini wengi wakawa na maswali kichwani kwani huo ni uwezo wake ama ni kwa sababu amekuta wachezaji waliopikwa tayari.

Baada ya kuwapa mafanikio akaamua kwenda nchini Ujerumani kuifundisha Bayer Munich, nao akawapatia kile walichokuwa wakikihitaji lakini maswali yakaendelea kama kawaida wengi wakidai hata hiyo timu aliikuta ikiwa na watu waliopikwa wakapikika.

Sasa hivi yupo Ligi ya nchini England na kwa kiwango kinachoonyeshwa na Mnchester City, ni wazi wale wote tuliokuwa tunautilia mashaka uwezo wa Guardiola, tuanze kunyoosha mikono juu na kumpa heshima yake.

Manchester City kwa kweli kwa sasa inavutia kuitazama na inatia presha ukisikia kesho inakwenda kucheza na timu yako unayoipenda kutoka moyoni kwani hujui nini kitakachowapata.

Kwa mwendo huu wa Manchester City ni wazi ubingwa upo nje nje licha ya kwamba ni mapema kulisemea kama wengi wanavyodai japo pia kuacha kulizungumzia ni sawa na kuwakosea heshima, kwani wanachokifanya kinafaa kuzungumzwa.

Na kama wakiteleza haitakuwa shida sana kwani ndugu zao yaani Manchester United, nao wapo kwenye moto wa hatari hivyo kombe hilo linaweza kutua kwenye jiji hilo la Manchester, sasa ni United au City, muda utazungumza.

Timu kama Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wanatajwa lakini kutajwa kwao hakuna nguvu sana kama timu hizo za Manchester ambazo zimekuwa zikifunga mabao mengi kadiri wawezavyo hasa wanapokutana na timu ambazo hazijiwezi.

Ili kudhihirisha kwamba msimu huu wamepania, hata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanatoa vipigo vya maana hiyo ikimaanisha kwamba wamejiandaa vizuri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.