TAMU, CHUNGU VPL MECHI ZA WIKIENDI

Dimba - - Special - NA MAREGES NYAMAKA

VUTA nikuvute raundi ya tano Ligi Kuu Tanzania Bara ilichukua nafasi yake mwishoni mwa wiki, huku ushindani ukionekana kuwa moto kutokana na timu mbili pekee kuibuka na ushindi kati ya mitanange nane iliyopigwa.

Walikuwa ni vinara Simba walioibuka na ushindi mbele ya Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage na kule Nangwanda Sijaona, wenyeji Ndanda wakiwanyoosha Lipuli FC na kuwa timu mbili pekee zilizovuna pointi tatu.

KICHUYA NA AGOSTI MOSI

Winga wa Simba, Shiza Kichuya, alifanikiwa kwa mara nyingine kujiwekea rekodi ya kipekee katika mchezo wao dhidi ya Stand United, Mnyama akiwalaza chali Wapigadebe hao.

Dakika ya 17 ya mchezo ikiwa ni sawa na namba ya jezi ya nahodha wa Simba, Method Mwanjale, alikuwa ni Kichuya aliyefunga bao la kuongoza akisetiwa na John Bocco na kumfanya kuwa mchezaji pekee wa Wekundu wa Msimbazi aliyewafunga Stand United mara nyingi.

Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Kichuya kuwafunga wapigadebe waliopanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita, kwani msimu uliopita aliwafunga bao pekee la ushindi hapo hapo Kambarage kabla ya kurudi tena nyavuni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika ushindi wa mabao 2-1.

Mbali ya Kichuya kuendeleza ubabe wake kwa Stand United, lakini pia amekuwa mwenye bahati na Agosti mosi, ambapo amekuwa akiingia kimiani tangu atue Simba akitokea Mtibwa, kwani alifanya hivyo msimu uliopita akiwafunga Yanga likiwa ni bao la kusawazisha.

KINDA AZAM AFUATA NYAYO ZA AKINA KIMWAGA, FARID

Jioni ya Jumamosi ilikuwa ya aina yake kwa mshambuliaji kinda wa Azam FC, Paul Peter, ambaye alifanikiwa kuibuka shujaa wa mchezo wao dhidi ya Singida United ikiwa ni baada ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha.

Peter aliyeingia dakika ya 84 akichukua nafasi ya Yahaya Mohamed, alifanikiwa kufunga bao hilo dakika ya 88 na kumfanya kuingia kwenye rekodi za mastraika wenzake akina Joseph Kimwaga, Farid Mussa na Shaban Idd.

Watatu hao ambao wote walipandishwa kutoka timu ya vijana huko nyuma, walianza kupata umaarufu kwa kuzifunga timu kubwa kama Yanga, yakiwa ni mabao muhimu dakika za lala salama.

TANZANIA PRISONS INATELEZA TU UGENINI

Ziweke pembeni timu za Simba, Azam na Mtibwa Sugar ambazo zilijikusanyia jumla ya pointi 11 kwa kila moja, zikizidiwa na Mnyama pekee kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, wageukie Tanzania Prisons ambao wamejiwekea rekodi ya peke yao kwa kuvuna pointi nyingi ugenini.

Wajelajela hao katika michezo yao mitatu waliyocheza ugenini, wameshinda miwili na sare moja, wakifanya hivyo katika mtanange wa awali kwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji, wakaendeleza wimbi la ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mwadui FC na kupunguzwa kasi na Mbao pekee katika mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

AZAM MOJA, MOJA

Licha ya Azam FC kukumbana na kisiki cha mpingo kwa mara ya kwanza ugenini msimu huu dhidi ya wenyeji wao Singida United kwa wanaume hao kutoshana nguvu, dakika 90 zikimalizika kwa sare ya bao 1-1, wanalambalamba hao waliendeleza rekodi ya kuwa na wastani wa kufunga bao pekee.

Matajiri hao wa Bongo kabla ya mtanange huo uliopigwa dimba la Jamhuri, mjini Dodoma, wakisawazisha bao dakika ya 88, walianza ligi hiyo kwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Ndanda, wakafanya hivyo pia kwa Kagera Sugar na Lipuli, isipokuwa kwa Simba pekee ambapo mechi ilimalizika kwa suluhu.

Kati ya mabao hayo manne yaliyoingia kimiani yanayoonekana kwenye msimamo, kinara ni Mbaraka Yusuph ambaye amefunga mawili, akiwaokotesha mipira wavuni makipa wa Lipuli na Kagera Sugar, huku Mghana Yahaya na kinda Paul Peter, wakiambulia bao moja kila mmoja.

KAGERA SUGAR 'INAMMIS' MBARAKA

Pamoja na kuwa na wachezaji wazoefu wa ligi kama kipa Juma Kaseja, beki Godfrey Taita walioisadia kuwa moja ya kikosi bora kilichomaliza ligi msimu uliopita kikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo, lakini hivi sasa kinaonekana kupwaya kwa safu ya ushambuliaji, ikiwamo mchezo wa Jumamosi dhidi ya Majimaji, uliomalizika kwa suluhu.

Bila shaka Wanankurunkumbi watakuwa wanakiri kimyakimya kukosa huduma ya straika wao bora wa msimu uliopita, Mbaraka Yusuph, aliyewafungia mabao 12, nyuma ya wafungaji bora Abdurhaman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva kutoka Yanga, waliongia kimiani mara 14.

Kagera ya kocha bora wa msimu uliopita Mecky Mexime, imekuwa ikicheza vizuri kuanzia safu ya ulinzi na eneo la kiungo lakini umalizijai wa mpira kimiani umekuwa shughuli pevu.

Namba hazijawahi kudanganya, kwani katika michezo yote mitano waliyocheza wamefunga bao moja pekee katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting, ambapo wanaburuza mkia na pointi zao mbili, sare zikiwa mbili, huku wakiwa wamepoteza mechi tatu.

YANGA INAMHITAJI TAMBWE KULIKO CHOCHOTE

Huenda mahaba ya mashabiki wa Yanga waliyonayo kwa kiungo wao Papy Kabamba Tshishimbi, wanamuona akifanya yake katikati ya dimba kila wanaposhuka dimbani, lakini hilo halitasaidia kama nafasi kadhaa zinatengezwa nyavu zinashindwa kutikiswa.

Yanga dhidi ya Mtibwa ilikuwa ni mechi ya tano Wanajangwani wanacheza bila huduma ya straika wao Amis Tambwe mwenye wastani mzuri wa kufunga.

Krosi na kona za Gadiel Michael na Juma Abdul nyingi zimekuwa zikikiishia mikononi mwa makipa wa timu pinzani pamoja na mabeki wao kuondoa hatari zote, huku Ngoma, Ajib na Chirwa wakishindwa kuzitumia vema.

Ikimbukwe ni mipira miwili ya vichwa pekee iliyofungwa na Ngoma dhidi ya Lipuli na Majimaji, huenda kurejea kwa Tambwe mchezo unaofuata Agosti 14 dhidi ya Kagera Sugar ikawa chachu ya ndani ya Yanga kuvuna mabao kwa kuzitendea haki krosi za Gadiel na Abdul pamoja na mipira ya kuzagaa ya eneo la hatari.

Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma kushoto, akimtoka mchezaji wa Majimaji, Tumba Suwed, wakati wa mchezo wao wa ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa Majimaji jana. Picha na Jumanne Juma

Kocha wa Yanga, Lwandamina

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.