MAMBO MATATU YANAYOITESA EVERTON, MSIMU HUU

Dimba - - Special - MERSEYSIDE, LIVERPOOL

KATIKA kuijenga upya klabu yao msimu huu, Everton wametumia zaidi ya pauni milioni 100, kusajili nyota wapya.

Umeona wachezaji waliowasajili? Wanatisha kweli kweli. Wamefanya usajili mkubwa kwa kukusanya nyota kutoka timu mbalimbali barani Ulaya.

Wamembeba Cuco Martina kutoka Southampton (bure), Wayne Rooney kutoka Manchester United kwa Pauni Mil 10, Josh Bowler kutoka QPR kwa Pauni Mil 1.5, Boris Mathis kutoka Metz (bure), Michael Keane kutoka Burnley kwa Pauni Mil 25, Sandro Ramirez kutoka Malaga kwa Pauni Mil 5.2, Henry Onyekuru kutoka KAS Eupen kwa Pauni Mil 6.8, Davy Klaassen kutoka Ajax kwa Pauni Mil 24 na Jordan Pickford kutoka Sunderland kwa Pauni Mil 30.

Huo ndio usajili uliofanywa na timu hiyo katika dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 31.

Aina ya usajili waliofanya na matokeo wanayoyapata ni vitu viwili tofauti, hawaonyeshi mchezo mzuri licha ya kuwa na kundi bora la wachezaji. Pia wamekuwa na matokeo mabaya katika michezo yao.

Kampeni yao ya ufunguzi wa Premier League ilianza vizuri kwa kuwafunga Stoke City bao 1, kisha kutoa sare ya 1-1 na Manchester City kwenye mchezo uliofuata.

Baada ya hapo walipoteza 2-0 kwa Chelsea, kisha waliruhusu kupigwa 3-0 na Tottenham, kabla ya kukumbana na kichapo cha 3-0 kutoka kwa Atlanta kwenye michuano ya Europa.

Muendelezo wa matokeo mabaya yaliendelea baada ya kupigwa 4-0 na Manchester United. Walizinduka mchezo uliofuata kwa kuwafunga 3-0 Sunderland kwenye EFL. Haikutosha waliwafunga Bournemouth 2-1 kabla ya kutoa sare ya 2-2 na Appollon kwenye michuano ya Europa.

Kwenye mchezo uliopita dhidi ya Burnley walikumbana na kichapo cha 1-0 katika dimba lao la Goodison Park huku mashabiki wao wakiwazomea kwa kiwango kibovu kilichoonyeshwa na timu hiyo.

Kwa aina ya matokeo hayo, siku za Ronald Koeman zitakuwa zinahesabika katika kikosi cha Everton. Frank de Boer hakupewa muda baada ya Crystal Palace kupoteza michezo minne mfululizo.

Hadi sasa Everton wamepoteza michezo minne kati ya saba ya Premier League, huku wakiwa nafasi ya 16, wakikusanya pointi saba tu.

Mshale wa sekunde umepungua kasi kwa Koeman, siku zake zinahesabika.

PENGO LA LUKAKU

Romelu Lukaku amejiunga na Manchester United akitokea Everton ambako alikuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho cha Koeman.

Msimu uliopita alifanikiwa kufunga mabao 26 katika michuano yote. Usajili uliofanywa msimu huu umekuwa wa tofauti na wengi walivyodhani, Koeman amesajili wachezaji namba 10 watatu bila kusajili mshambuliaji.

Amewasajili Wayne Rooney, Davy Klaassen na Gylfi Sigurdsson. Pia hata Sandro Ramirez kwa asili sio mshambuliaji, mara nyingi hutumika kama mshambuliaji kivuli wakati yupo Malaga na Hispania U-23.

Wamekosa mshambuliaji halisi kwenye kikosi chao. Hawana mchezaji wa kusumbuana na mabeki kama ilivyokuwa kwa Lukaku.

KUCHELEWESHA MABADILIKO

Amekuwa muhanga mkubwa wa kuchelewa mabadiliko pindi timu inapohitaji mabadiliko. Katika michezo sita msimu huu alishindwa kufanya mabadiliko wakati uliostahili.

Huku wengi wakimlaumu kitendo hicho kimekuwa kikiigharimu timu hiyo pindi inapohitaji matokeo, kama ilivyotokea kwenye mchezo waliotoa sare ya 2-2 kwenye michuano ya Europa dhidi ya Appollon.

MAKOSA KWENYE ULINZI

Ashley Williams pekee amefanya makosa sita yaliyoigharimu timu hiyo. Wengi wanakumbuka kosa alilolifanya Old Trafford kwa Man United kujipatia goli la pili kupitia Henrik Mkhitaryan.

Mawasilano ya walinzi wake wa kati yamekuwa shida sana, Keane, Williams na Jagielka wote wamekuwa na wakati mgumu sana pindi timu yao inaposhambuliwa.

Hadi sasa Everton wamepoteza michezo minne kati ya saba ya Premier League, huku wakiwa nafasi ya 16, wakikusanya pointi saba tu. Mshale wa sekunde umepungua kasi kwa Koeman,

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.