Viungo wakabaji waliotikisa Tanzania

Dimba - - Special - NA HENRY PAUL

W IKI iliyopita Pazi katika toleo la nane aliishia kusimulia kwamba mwaka 1980 yeye awali hakuchaguliwa katika kikosi cha timu ya Taifa Stars, ambacho kilikuwa kinatarajiwa kucheza michuano ya fainali ya Mataifa Afrika ambayo ilikuwa inategemewa kuchezwa katika mji wa Lagos, Nigeria.

Mkongwe huyo anakumbuka kuwa yeye aliongezwa katika kikosi hicho, ambapo timu hiyo ya Stars ilikuwa nchini Mexico ikijiandaa kwa fainali hizo na kuwa golikipa wa tatu, ambapo magolikipa wengine wawili walikuwa ni Athumani Mambosasa na Juma Pondamali ‘Mensah’.

Pazi baada ya kuchaguliwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho cha Taifa Stars, alifunga safari akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Nchini wa wakati ule FAT, Said El-Mammry, mjini Lagos, Nigeria, kuungana na wenzake ambao walikuwa nchini Mexico kwa ajili ya michuano ya kirafiki ya kujipima nguvu.

Nyota huyo anakumbuka kuwa baada ya kuungana na wenzake, timu ya Taifa Stars ilipangwa katika kundi A ikiwa na wenyeji Nigeria, Misri na Ivory Coast. Mechi ya kwanza Stars walifungwa na wenyeji Nigeria mabao 3-1, mechi ya pili walifungwa na Misri mabao 2-1 na mechi ya mwisho walitoka sare ya bao 1-1 na Ivory Coast na hivyo kuondolewa katika michuano hiyo. Sasa endelea.

“Nakumbuka Taifa Stars baada ya kutolewa katika michuano ile ya Mataifa Afrika iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria, tuliporudi nchini tulikaa kama mwezi mmoja tu na timu ya Stars kuchaguliwa tena ambapo safari hii ilikuwa inatarajia kucheza michuano ya awali ya kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia.

“Baada ya Taifa Stars kuchaguliwa tena, mimi sikuteuliwa katika kikosi hicho, kwani magolikipa waliochaguliwa walikuwa ni wawili tu ambao ni Juma Pondamali ‘Mensah’ na Athumani Mambosasa.

“Nakumbuka baada ya timu hiyo kuchaguliwa walipangwa kucheza na timu ya Taifa ya Nigeria, ambapo mchezo huo wa kwanza ulichezwa mjini Lagos, Nigeria kwenye uwanja wao wa taifa Surulere, ambapo katika mchezo huo matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1 huku kipa wa Stars akiwa ni Juma Pondamali.

“Kabla ya kucheza mechi hiyo timu ya Taifa ya Nigeria walikuwa na mawazo kuwa wataifunga Stars mabao mengi kama walivyoifunga mwezi mmoja nyuma katika fainali za Mataifa Afrika, ambapo walitufunga mabao 3-1 hivyo hawakuiwekea mkazo sana mechi hiyo ya kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia.

“Nakumbuka mechi ya marudiano ya timu ya Taifa ya Nigeria ambayo ilichezwa baada ya wiki mbili katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), timu ya Taifa ya Nigeria iliifunga Stars mabao 2-0 huku golini akiwa tena na Pondamali ‘Mensah’.

“Timu ya Taifa ya Nigeria ilifanikiwa kuifunga Stars kutokana na kwamba, safari hii katika mchezo huu wa marudiano waliwaita wachezaji wao wawili ambao walikuwa wakicheza soka la kulipwa Ulaya. Wachezaji hao ni kiungo Tunji Banjo na winga hatari John Chiedozie, ambaye alifunga mabao yote mawili.

“Stars baada ya kufungwa katika mchezo huo wa marudiano na timu ya Taifa ya Nigeria mabao 2-0, tulitolewa katika michuano hiyo kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Nigeria matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1.

“Novemba 1981 wakati bado nachezea klabu ya Majimaji ya Songea, timu ya Taifa Stars ilichaguliwa tena kucheza michuano ya Kombe la Chalenji, mashindano hayo yalifanyika nchini kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru).

Katika uteuzi huo mimi sikuchaguliwa, kwani makipa waliochaguliwa walikuwa ni Juma Pondamali ‘Mensah’, Athumani Mambosasa na Juma Mhina.

“Katika michuano hiyo, Taifa Stars ilipangwa kundi A pamoja na timu ya Kenya, Malawi na Zanzibar. Katika kundi hilo Stars iliibuka mshindi wa kwanza na kucheza na mshindi wa pili wa kundi B ambayo ilikuwa ni Zambia.

Katika mechi ya nusu fainali ya kwanza, Stars iliibuka mshindi kwa kuifunga Zambia mabao 2-1. Kenya ambayo ilikuwa mshindi wa pili wa kundi A ilicheza nusu fainali ya pili na mshindi wa kwanza wa kundi B ambayo ilikuwa ni Uganda.

Kenya iliibuka mshindi kwa kuifunga Uganda mabao 2-1 na hivyo kucheza fainali na Taifa Stars. Katika mechi ya fainali Stars ilifungwa na Kenya bao 1-0 na hivyo timu ya Harambee Stars kutwaa taji hilo kwa mwaka huo wa 1981.

Fainali hiyo ilichezwa Novemba, 1981 na kipa wa Stars alikuwa ni Athumani Mambosasa, kwani Juma Pondamali ‘Mensah’ alikuwa amefungiwa mwaka mmoja na Chama cha Soka Nchini (FAT) kwa utovu wa nidhamu. Nini kitatokea mwaka 1982. Usikose toleo lijalo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.