Viungo wakabaji waliotikisa Tanzania

Dimba - - Special - NA HENRY PAUL

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zilizobahatika kuwa na wachezaji viungo wakabaji wengi, ambao walivuma katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu) pamoja na timu ya taifa, Taifa Stars.

Lakini kati ya hao kuna baadhi ya wachache ambao walikuwa hodari katika kumudu kucheza vyema katika nafasi hiyo ya kiungo mkabaji na wengine kuvuma nje ya nchi. Wafuatao ni baadhi ya wachezaji hao:

1.Juma Mkambi ‘General’

Unapozungumzia wachezaji waliokuwa wanamudu kucheza vyema nafasi ya kiungo mkabaji namba sita, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina na Juma Mkambi au ‘General’ kama wapenzi wa soka nchini hususan wa klabu ya Yanga walivyozoea kumwita.

Mkambi ambaye hivi sasa ni marehemu alijiunga na klabu ya Yanga msimu wa 1979/1980 akitokea Nyota ya Mtwara, akiwa na mshambuliaji Rashid Hanzuruni (marehemu) ambao kwa wakati huo wote walikuwa ndio kwanza wanachipukia.

Baada ya kujiunga na Yanga kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa nao wa kucheza vyema nafasi za kati, makocha wakawa wanamtumia kucheza safu ya kiungo mkabaji namba sita huku Charles Boniface ‘Master’ ambaye naye alijiunga msimu huo akitokea Tumbaku ya Morogoro akawa anapangwa kiungo mshambuliaji namba nane.

Wakati huo Yanga kuanzia mwaka 1976 hadi 1980, ilikuwa katika kipindi cha mpito cha kutengeneza timu baada ya nyota wake wengi kutimuliwa mwaka 1976 na kuhamia klabu ya Nyota Afrika ya Morogoro.

Mwaka 1981 Yanga ilifuta uteja kwa Simba wa kufungwa kwa takriban miaka mitano mfululizo ilipowafunga watani wao hao Simba 1-0, katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru).

Katika mechi hiyo Mkambi aling’ara mno ambapo katika dakika ya 42 ya kipindi cha kwanza, alifunga bao hilo pekee kwa kichwa kutokana na kona iliyochongwa na Ahmed Amasha.

Mkambi alifunga bao hilo baada ya kuruka juu na kuwazidi mabeki wawili wa Simba, Mohamed Bakari ‘Tall’ na Aloo Mwitu na kupiga kichwa na mpira kumshinda kipa Omari Mahadhi na kutinga wavuni.

Baada ya Mkambi mwaka huo wa 1981 kubatizwa jina hilo liliendelea na kuzoeleka na wapenzi wa soka nchini hadi alipostaafu kucheza soka ya ushindani msimu wa 1988/1989 alipokuwa na timu ya daraja la pili Super Star iliyokuwa na maskani yake makuu Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Juma Mkambi ‘Generali’ alifariki dunia Novemba 21, 2010 kutokana na matatizo ya tumbo yaliyokuwa yakimsumbua kwa takriban wiki mbili na kuzikwa siku ya pili Novemba 22, 2010, saa saba mchana katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

2.Mohamed Rishard ‘Aldoph’

Rishard kama alivyokuwa Mkambi naye alikuwa mahiri mno katika nafasi hiyo ya kiungo mkabaji, kwani alikuwa anatumia akili mno kumdhibiti mshambuliaji, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika na nguvu pale inapohitajika.

Nyota huyu alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka katika miaka ya 1970 mwanzoni akiwa na timu ya Yanga watoto maarufu kama ‘Yanga Kids’.

Mwaka 1972, Rishard alipandishwa katika kikosi cha Yanga B kilichokuwa kikinolewa na Athumani Kilambo (marehemu) kabla ya kocha Tambwe Leya ambaye pia ni marehemu kumpandisha katika kikosi cha kwanza mwaka 1974.

Mwaka 1977 Rishard akiwa na wenzake chipukizi walijiunga na klabu mpya ya Pan African iliyokuwa imeanzishwa mwaka huo na kuungana na nyota wote waliokuwa Nyota Afrika ya Morogo, ambao awali walifukuzwa Yanga.

Rishard akiwa na Pan African mwaka huo wa 1977 kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa akiuonesha, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya Taifa Stars.

Akiwa na timu ya Taifa Stars mwaka 1979 katika mchezo wa kwanza wa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (KK11), uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), alifunga bao pekee.

Pia Rishard alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa timu ya Taifa Stars waliocheza fainali za Mataifa ya Afrika, zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980.

3.Mtemi Ramadhani

Ramadhani kama walivyokuwa Mkambi na Rishard, naye alikuwa mahiri katika nafasi ya kiungo mkabaji ambaye alivuma hapa nchini hususan wakati akicheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu).

Nyota huyu alisiÀka mno kutokana na aina ya uchezaji wake, kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika, uwezo mkubwa wa kudhibiti washambuliaji wasumbufu na uwezo wa kupachika mabao.

Mwaka 1980 akiwa na klabu ya Waziri Mkuu alichaguliwa kuchezea timu ya Taifa Stars na alikuwa katika kikosi kile cha timu hiyo kilichoshiriki fainali ya michuano ya Mataifa Huru Afrika, iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.

Mwaka 1981 alijiunga na klabu ya Simba na kuwa mmoja ya wachezaji wa kutumainiwa wa timu hiyo, akicheza safu ya kiungo mkabaji namba sita ambapo pia wakati huo alikuwa akiendelea kuchezea timu ya taifa, Taifa Stars.

4.Ramadhani Lenny ‘Abega’

Lenny naye ni miongoni mwa wachezaji wanaokumbukwa na wapenzi wa soka nchini, kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa nao wa kumudu kucheza vyema nafasi ya kiungo mkabaji.

Nyota huyu ambaye hivi sasa ni marehemu alisiÀka mno kutokana na aina ya uchezaji wake, kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika na uwezo mkubwa wa kuwadhibiti washambuliaji waliokuwa wasumbufu uwanjani.

Lenny ambaye aliibukia eneo la Temeke, jijini Dar es Salaam miaka ya 1980 akichezea timu za mitaani, alianza kupata umaarufu mkubwa katika soka mwaka 1983 wakati alipokuwa akichezea timu ya Simba B.

Kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa nao wa kumudu kucheza vyema nafasi ya kiungo mkabaji, mwaka 1984 alipandishwa kuchezea kikosi cha kwanza Simba A ambapo baada ya kuichezea timu hiyo takribani mechi nne alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa ikinolewa na kocha Hudson raia wa England.

Akiwa na kikosi cha Simba kutokana na jinsi alivyokuwa hodari katika kumudu nafasi ya kiungo mkabaji, wapenzi wa timu hiyo walimbatiza jina la ‘Abega’ wakimfananisha na kiungo mahiri wa zamani wa Cameroon, Abega Mbida.

Mwaka 1988, Lenny alitimkia Uarabuni kucheza soka la kulipwa ambapo alikaa huku hadi 1992, aliporudi nchini alijiunga tena na klabu yake ya Simba ambayo aliichezea hadi 1995 alipojiunga na klabu ya Vijana ya Ilala kabla ya kujiunga na klabu yake ya mwisho Kajumulio FC mwaka 1997.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.