Nyimbo na video chafu…TUKI na BASATA msimung'unye

Dimba - - Special - KWA LEO NAISHIA HAPA, ALAMSIK.

Karibuni tena katika safu yetu hii maalumu kila wiki inayoangazia mambo mbalimbali ya kimichezo na sanaa kwa upana wake kadiri yanavyojiri kila siku ndani ya jamii yetu ya Tanzania. Wadau wote karibuni sana.

Cheka kwa Uchungu leo inazikumbusha mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sanaa ya muziki, hasa wa kizazi kipya bila kujali maudhui na mitiririko yake juu ya udhibiti wa matumizi ya maneno (mashairi) na picha jongefu (video) zisizozingatia maadili ya Mtanzania.

Ikiwa mdau mkubwa wa vitu hivyo, safu hii inazigutua taasisi muhimu za Kiserikali kama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) kuwajibika kwa kufanya chunguzi za mara kwa mara kwenye nyimbo za wanamuziki wa ‘Bongo Fleva’ ambao ndio umegeuka kinara wa kuharibu au kuporomosha heshima na maadili kwa tafsiri ya baadhi ya wasanii kuimba na kuvaa mavazi au kucheza ‘staili’ zenye viashirio ya ‘matusi’.

Aidha, safu hii inapendekeza taasisi hizo kubuni njia mwafaka na stahiki za kusimamia vema ustawi wa sanaa yote bila kuathiri upande mwingine kwa vile wanamuziki na wapenzi na mashabiki wao wote ni sehemu ya jamii. Ni imani yetu kuwa chini ya mawaziri, Dk. Harrison Mwakyembe na Profesa Joyce Ndalichako uwezekano wa kudhibiti ‘upotoshaji’ huu utafanikiwa, kama kweli watadhamiria.

Kama watapata wakati mgumu wa kutimiza wajibu huo, wanaweza kurejea mfumo wa zamani uliotumika zama za utawala wa muziki wa dansi hapa nchini ambapo hakuna bendi iliyoruhusiwa kurekodi nyimbo zake katika studio yoyote bila mashairi yake kupitiwa na kuhakikiwa na mamlaka zilizowekwa. Hilo linawezekana kabisa ukiongezwa na uhakiki wa video zinazozalishwa sasa.

Ukijiuliza, inawezekanaje wimbo wa msanii fulani wa Bongo Fleva unafungiwa kwa kutokidhi au kukiuka vigezo na msanii anatii? Halafu itashindikanaje kuzuia nyimbo hizo hizo zisiingizwe mitandaoni kabla hazijaidhinishwa? Kinachojionesha hapa ama ni ‘uzembe’ au ‘kutowajibika’ kwa baadhi ya wahusika wa idara za Serikali, huku wakiliacha Taifa likipoteza mwelekeo wa kimaadili polepole kiasi cha kuwaaminisha wanetu kuwa huenda ndivyo maisha yanavyopaswa kuwa.

Mifano ipo mingi sana, siku hizi karibu kila kituo cha runinga kinachoonesha vipindi vya muziki, haishangazi kuona wanamuziki au wanenguaji wao wakiwa wamevaa zaidi ya nusu uchi na kama haitoshi wakicheza kwa ishara zisizo na taswira njema kwa watoto wetu kama si jamii kwa ujumla.

Mara nyingine inatuwia vigumu kuangalia video za muziki wa Bongo Fleva na zile za Kinigeria kama si Ivory Coast, hasa ukijikuta upo na wanao sebuleni, achilia mbali mitandaoni ambako kuanzia watumiaji wa simu za viganjani na kompyuta mpakato hujionea ‘uchafu’ wa kila aina kiasi cha kukufanya ujiulize kama kuna vyombo vya Serikali vyenye dhamana ya kusimamia na kulinda maadili ya Mtanzania.

Hili si la kulifumbia macho, tuamke sasa na kuchukua hatua. Tusipolidhibiti na kulikomesha leo, litatusumbua zaidi kesho na tutakuwa hatuna wa kumlaumu bali kucheka kwa uchungu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.