Diamond, Zari kisu kimenasa kwenye mfupa?

Dimba - - Special - NA JESSCA NANGAWE

GUMZO kubwa kwa sasa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari nchini ni penzi la mastaa wawili, Diamond Platinumz na Zarinah Hassan (Zari the boss lady).

Tangu Diamond Platinumz alipokiri kuwa ‘alipitiwa na shetani’ na kuingia kwenye mahusiano na mrembo Hamissa Mobeto hadi kubahatika kupata mtoto mmoja, moyo wa Zari ni kama umemwagiwa pilipili.

Kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akiitumia mitandao ya kijamii kutoa povu na maneno ya mafumbo kwa mwenzake.

Zari akiandika hivi, Diamond atajibu vile. Licha ya kuendelea kusisitiza kuwa bado hawajabwagana, sintofahamu imekuwa kubwa kwa mashabiki wa mastaa hao, waliobahatika kupata watoto wawili katika mahusiano yao.

Mengi yanasemwa. Wako wanaotamani Zari ampige chini Diamond kutokana na usaliti aliofanyiwa, lakini pia wako wanaomsihi mrembo huyo wa Uganda, kupiga moyo konde na kumsamehe mpenzi wake.

Tayari Diamond ameshaonyesha kuwa licha ya kuchepuka na Hamissa, bado anampenda sana Zari, kiasi cha kusema hadharani kuwa yuko tayari kutembea kwa magoti kutoka Tanzania mpaka Afrika Kusini, kwa ajili ya kuomba msamaha.

Lakini uko upande wa tatu unaoamini kuwa, wawili hawa hawawezi kuachana hata kama wakisalitiana mara 1,000, na hii ni kutokana na wote wawili kutegemeana katika mambo yao.

Diamond anatajwa kumtegemea Zari katika kupewa mipango mingi ya kazi na kibiashara, huku mama Tiffah, akidaiwa kulitegemea jina la baba Nillan, katika kuendesha kazi zake.

Wakati hayo yakiendelea, DIMBA limefuatilia kwa kina ukaribu wa wawili hao sambamba na mikataba waliyoingia na maendeleo waliyoyafanya kwa pamoja, ili kuangalia kama ni kweli kuna ukweli wa wawili hawa kutegemeana katika shughuli zao.

Utajiri wa Diamond

Inadaiwa utajiri wa Diamond umeongezeka maradufu baada ya kuingia kwenye mahusiano na mrembo huyu wa Uganda.

Licha ya kuwapo kwa tetesi nyingi juu ya mali zake, Diamond Platinumz hajawahi kusimama hadharani na kuweka wazi kuwa ana utajiri wa kiasi gani.

Wengi wameishia kujiuliza na kujijibu tu wenyewe. Lakini baada ya kufanya uchunguzi na kufuatilia mali zake, tumeweza kupata makadirio ya utajiri wa staa huyu anayetamba kwa sasa na wimbo wa ‘Hallelujah’, aliomshirikisha Morgan Heritage kutoka Jamaica.

Kwa mujibu wa taarifa ya The Net Worth, kwa mwaka 2017, Diamond ana utajiri wa dola milioni 4 za Kimarekani, ambazo kwa fedha za Tanzania ni zaidi ya Sh bilioni 8.6.

Si kitu kinachoshangaza tena kwa Diamond kutokana na hatua aliyofikia akiwa msanii anayelipwa fedha nyingi zaidi Tanzania kwa sasa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, Diamond anatajwa kulipwa wastani wa Sh milioni 7.5 kwa kila shoo, lakini inategemea na aina ya shoo anayotumbuiza.

Fedha zake nyingi zinatokana na shoo hizo zisizokauka ndani na nje ya Tanzania, mikataba ya ubalozi na matangazo kutoka makampuni mbalimbali kama Vodacom, Coca-Cola, DSTV, Red Gold sambamba na biashara yake ya karanga. Pia amekuwa akiingiza fedha nyingi kupitia biashara ya nyimbo zake, hasa miito ya simu, malipo ya mirabaha kutoka nchi za jirani kama Kenya, bila kusahau biashara za mtandaoni, ikiwamo Youtube. Uwekezaji wake kwenye lebo ya WCB ni kitu kingine kikubwa ambacho kimeanza kumwingizia fedha nyingi kwa sasa. Katika lebo hiyo, amewasaini wasanii wengi, akiwamo Rich Mavoko, Rayvanny, Mr Lavalava, Harmonize, Maromboso na dada yake, Queen Darleen. Lakini pia staa huyo anafahamika kwa kuwekeza zaidi fedha kwenye ardhi na nyumba, huku akidaiwa kumiliki maeneo mengi jijini Dar es Salaam sambamba na nyumba pamoja na magari. Pia Diamond amekuwa akiingiza pesa kupitia watoto wake, Tiffah na Nillan, ambao wameingia mikataba na makampuni mbalimbali wanayofanya nayo matangazo.

Vipi kuhusu ‘Zari the boss lady’

Huyu ni mjasiriamali Mganda ambaye baada ya kifo cha aliyekuwa mumewe, Ivan Semwanga, huenda utajiri wake umeongezeka, kutokana na kuachiwa mali nyingi zaidi ya zile alizokuwa akimiliki awali. Zari ni miongoni mwa matajiri wanaotikisa nchini Afrika Kusini, akikimbizana na matajiri wengine wakubwa kutoka Nigeria.

Kwa sasa makazi ya mrembo huyu yapo Afrika Kusini. Amezoewa kupenda maisha ya gharama na hii ni kutokana na kumiliki kiasi kikubwa cha pesa, zikiwamo mali alizoachiwa kabla na baada ya kifo cha mumewe, Ivan.

Mbali ya kumiliki majumba ya kifahari nchini Uganda na Afrika Kusini, ukichanganya na zile alizopewa kwa ajili ya watoto wake baada ya kifo cha baba yao, pia mwanamama huyo ambaye amejaliwa watoto watano ameachiwa utajiri mkubwa, ikiwamo shule na vyuo saba vinavyojulikana kwa jina la Brooklyn Collage, vilivyojengwa kwenye miji ya Pretoria na Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Zari pia anafahamika kwa kuendesha magari mengi ya kifahari, yakiwamo Lamborghini, Audi 2010, Hummer pamoja na Range Rover Sports, ambayo yote ameyaandika majina yake badala ya namba za usajili.

Mbali ya mali hizo, pia anamiliki hoteli ya kifahari katika Mtaa wa Kagwa nchini Uganda, vyuo vya urembo na vipodozi vilivyopo nchini Afrika Kusini sambamba na kufanya shoo mbalimbali anazozifanya kupitia jina lake. Mikataba ya pamoja

Diamond na Zari waliwahi kuingia mkataba wa pamoja na kampuni ya simu ya Vodacom, uliotajwa kuwaingia kiasi cha dola 660,000 (zaidi ya Sh milioni 100 za Kitanzania).

Wawili hawa pia wameingia mkataba mwingine na kampuni ya GSM Mall ya hapa Tanzania na kufanya tangazo ambalo kwa wiki hii limekuwa maarufu sana, baada ya mrembo, Hamissa Mobeto, kuliweka kwenye akaunti yake ya Instagram.

HAMISA MOBETO

NILLAN DAYLAN /ABDUL

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.