Miaka 26 ya safari yake kisoka (10)

Dimba - - Special - NA HENRY PAUL

WIKI iliyopita Pazi katika toleo la tisa aliishia kusimulia kwamba, Novemba mwaka 1981 wakati bado anacheza klabu ya Majimaji ya Songea, timu ya Taifa Stars ilichaguliwa tena kucheza michuano ya Kombe la Chalenji, mashindano hayo yalifanyika nchini kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru).

Katika makala hiyo mkongwe huyo anasimulia kuwa katika uteuzi huo yeye hakuchaguliwa, kwani makipa waliochaguliwa walikuwa ni Juma Pondamali ‘Mensah’, Athumani Mambosasa na Juma Mhina.

Pia nyota huyo anasimulia kuwa michuano hiyo Taifa Stars ilipangwa kundi A pamoja na timu ya Kenya, Malawi na Zanzibar. Katika kundi hilo Stars iliibuka mshindi wa kwanza na kucheza na mshindi wa pili wa kundi B ambayo ilikuwa ni Zambia.

Mkongwe huyo anasimulia mechi ya nusu fainali ya kwanza, Stars iliibuka mshindi kwa kuifunga Zambia mabao 2-1 na Kenya ambayo ilikuwa mshindi wa pili wa kundi A ilicheza nusu fainali ya pili na mshindi wa kwanza wa kundi B ambayo ilikuwa ni Uganda.

Nyota huyo anasimulia kwamba Kenya iliibuka mshindi kwa kuifunga Uganda mabao 2-1 na hivyo kucheza fainali na Taifa Stars. Katika mechi ya fainali Stars ilifungwa na Kenya bao 1-0 na hivyo timu ya Harambee Stars kutwaa taji hilo kwa mwaka huo wa 1981.

Pazi alimalizia kwa kusimulia kuwa fainali hiyo ilichezwa Novemba, 1981 na kipa wa Stars alikuwa ni Athumani Mambosasa, kwani Juma Pondamali ‘Mensah’ alikuwa amefungiwa mwaka mmoja na Chama cha Soka Nchini wakati huo (FAT) kwa utovu wa nidhamu. Sasa endelea.

“Nakumbuka Novemba 1982 wakati bado niko na klabu ya Majimaji ya Songea, timu ya Taifa Stars ilichaguliwa tena ambayo ilikuwa icheze michuano ya Chalenji nchini Uganda kwenye Uwanja wa Nakivubo.

Makipa waliochaguliwa walikuwa ni watatu ambao ni mimi (Pazi), Hamisi Kinye na Juma Mhina.

“Stars baada ya kufika Kampala, Uganda katika michuano hiyo, tulipangwa kundi A pamoja na timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, timu ya Taifa ya Zimbabwe na timu ya Taifa ya Malawi. “Kundi B zilikuwa ni timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambe Stars’, Zanzibar na timu ya Taifa ya Sudan.

“Mechi ya kwanza Taifa Stars tulicheza na timu ya Taifa ya Zimbabwe na matokeo ni kwamba Stars tulifungwa mabao 3-0 huku langoni akiwa ni Hamisi Kinye.

“Baada ya Stars kufungwa idadi hiyo ya mabao, wachezaji waandamizi (wazoefu) walimpa ushauri kocha Bendera kuwa kwanini golini nisipangwe mimi (Pazi)? Kwa sababu ni mzoefu halafu nilikuwa na timu hiyo toka katika michuano ya awali ya kufuzu fainali ya Mataifa Afrika.

“Baada ya Bendera kupewa ushauri huo kutoka kwa wachezaji waandamizi, mechi ya pili Stars tulicheza na wenyeji Uganda huku golini nikipangwa mimi, lakini tulifungwa bao 1-0. Mechi ya tatu Stars tulicheza na Malawi huku golini nikiwa mimi (Pazi) ambapo mechi hiyo tulifungwa mabao 2-0.

“Kundi A Uganda iliibuka mshindi wa kwanza huku mshindi wa pili ikiwa ni Zimbabwe. Kundi B Kenya iliibuka mshindi wa kwanza huku mshindi wa pili ilikuwa ni Zanzibar.

“Katika nusu fainali ya kwanza mshindi wa kwanza kundi A Uganda ilicheza na mshindi wa pili kundi B ambayo ilikuwa ni Zanzibar, ambao Uganda ilishinda kwa mabao 3-0. Kundi B mshindi wa kwanza Kenya ilicheza na mshindi wa pili kundi A Zimbabwe na Kenya kushinda kwa mabao 2-0.

“Hivyo, katika hatua ya fainali waliingia Uganda na Kenya na matokeo katika dakika 90 kuwa ni sare ya 1-1. Ilipopigwa mikwaju ya penalti Kenya iliibuka na ushindi kwa kuifunga Uganda mabao 6-3 na hivyo Kenya ‘Harambee Stars’ kutwaa taji hilo la Chalenji kwa mwaka huo wa 1982. Fainali hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda Novemba 27, 1982.

“Nakumbuka kikosi cha Taifa Stars kilichocheza mechi mbili za mwisho kilikuwa kinaundwa na mimi (Pazi), beki wa kulia alicheza Kiwhelo Mussa (marehemu), beki wa kushoto alicheza Ahmed Amasha, namba nne alicheza Athumani Juma ‘Chama’, wakati sentahafu alisimama Lilla Shomari (marehemu) na kiungo mkabaji alicheza Mohamed Rishard ‘Adoph’.

“Winga ya kulia alicheza Omari Hussein ‘Keegan’, kiungo mshambuliaji alicheza Hussein Ngulungu, wakati sentafowadi alisimama Peter Tino, namba 10 alicheza Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ na winga ya kushoto alicheza Ally Mchumila ambaye alikuwa anabadilishana na Willy Kiango (marehemu). Nini kitatokea baada ya michuano hiyo ya Chalenji 1982. Usikose toleo lijalo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.