YANGA YAMWAGIWA MAMILIONI USIKU

BILIONEA ASHUSHA WACHEZAJI KWENYE BASI, SASA KUKWEA PIPA ALHAMISI

Dimba - - Mbele - NA HUSSEIN OMAR

YANGA na Kagera Sugar zitavaana Jumamosi wiki hii katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Wenyeji Kagera Sugar ambao wanashika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa kutokana na kuwa na pointi mbili tu, wamekuwa katika maandalizi mazito kwa ajili ya mechi hiyo, wakifanya mazoezi kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko eneo la Misenyi, mjini Bukoba, ndani ya Kiwanda cha Sukari cha Kagera.

Lakini huenda wakashituka na kupigwa butwaa kwani Yanga ambayo inaondoka kesho Alhamisi kuwafuata, imetuma mashushushu wake kwenda kuwavamia.

Yanga ilikuwa ianze safari ya kwenda Kanda ya Ziwa leo Jumatano asubuhi kwa basi lake la kisasa, ambapo inatarajiwa kucheza michezo miwili huko huko ugenini wakianza na wa Jumamosi Oktoba 14 dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba kabla ya kuelekea Shinyanga kucheza na Stand United, Oktoba 22 mwaka huu.

Lakini bilionea wa timu hiyo aliibuka ghafla jana usiku na kuwamwagia wachezaji mamilioni, huku akiwazuia wasiondoke kwa basi na badala yake wasubiri hadi kesho awapandishe ndege.

Wakitambua umuhimu wa michezo yote miwili, mabingwa hao watetezi wameamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja baada ya kuwatanguliza matajiri wenye utashi mkubwa ndani ya timu kuweka mambo sawa kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye michezo yote hiyo.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia DIMBA Jumatano, kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa timu hiyo Samuel Lukumay, tayari yupo mjini Bukoba kwa ajili ya kushughulikia kuhusiana na mahali timu itafikia pamoja na uwanja wa kufanyia mazoezi.

"Tumedhamiria kufanya kweli tunaondoka hapa kwa kishindo kwenda Bukoba lakini nikwambie tu tayari kuna baadhi ya vigogo wameshatua kule akiwemo Lukumay,” alisema kigogo huyo.

Mbali na Lukumay vigogo wengine ambao wapo mjini Bukoba ni pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kutoka mikoa ya Mwanza na Geita, ambao wamepewa kazi maalum ya kuhakikisha hakuna kinachoharibika.

Tayari Yanga wameshacheza michezo mitano wakishinda miwili na kutoka sare michezo mitatu wakijikusanyia pointi tisa na sasa wanataka kuhakikisha wanashinda michezo hiyo dhidi ya Kagera Sugar na Stand United.

Licha ya kwamba kikosi hicho kitamkosa mshambuliaji wake Donald Ngoma pamoja na kiungo Thaban Kamusoko kutokana na majeraha yanayowakabili lakini wenye timu yao wanadai kuwa hiyo haitawasumbua kwani wachezaji waliopo wanaweza kufanya lolote.

Yanga itaikabili Kagera Sugar Jumamosi huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 6-2 ilioupata kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na Ngoma aliyefunga mawili sawa na Chirwa huku Simon Msuva ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Morocco, alifunga moja na lingine likifungwa na Deus Kaseke ambaye kwa sasa anaichezea Singida United.

Hadi sasa Kagera Sugar ndiyo timu mojawapo kati ya tatu ambazo hazijapata ushindi wowote tangu Ligi Kuu Bara ianze msimu huu. Timu nyingine ni Ruvu Shooting na Majimaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.