OKWI AWAKALIA KOONI 4 LIGI KUU

Dimba - - Mbele - NA MARTIN MAZUGWA

KASI ya ufungaji mabao inayoonyeshwa na mshambualiaji wa Simba, Emanuel Okwi, imeanza kuwatia presha nyota wanne wanaowania kiatu cha dhahabu msimu huu ambao wamekuwa wakimhofia mkali huyo.

Okwi anaongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao sita, akifuatiwa na Mohamed Rashid wa Tanzania Prisons mwenye mabao manne, ambaye amekabidhiwa viatu vya Victor Hangaya, aliyetimkia Mbeya City.

Wengine ni Shiza Kichuya mwenye mabao matatu, ambaye msimu uliopita ndiye alikuwa mfungaji bora katika kikosi cha Simba kwa kuweka nyavuni mabao 13, huku Mbaraka Yusuph wa Azam FC, ambaye alikuwa akiichezea Kagera Sugar, akimaliza msimu na mabao 12.

Nyota hao kila mmoja malengo yake ni kuhakikisha anakuwa mfungaji bora, lakini kasi aliyonayo Okwi, anawatisha, licha ya kwamba wanapambana mpaka dakika ya mwisho.

Akimzungumzia Mganda huyo, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amesema anafarijika sana kuwa na mtu mwenye uchu wa kufunga mabao, hiyo ikiashiria kwamba anaweza kuwa mfungaji bora.

"Okwi atakuwa miongoni mwa wachezaji nitakaowatumia mara kwa mara kutokana na uwezo wake ndani ya Uwanja, anafunga mabao na ninaamini anaweza akawa mfungaji bora," alisema.

Okwi alifunga mabao katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting na Mwadui FC, lakini akashindwa kufunga katika michezo miwili dhidi ya Mbao FC, na Stand United, lakini sasa ameahidi kufanya vizuri mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar, Jumapili ya wiki hii.

"Kufunga au kutofunga ni sehemu ya mchezo, ila naamini nitarudi kivingine katika mchezo ujao, ambao ni muhimu kwangu na kikosi kizima cha Simba,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.