DAKIKA 15 ZA YANGA KUCHEKA NA NYAVU

Dimba - - Mbele - NA EZEKIEL TENDWA

YANGA wanajua kwamba wamekuwa wakikamiwa sana na timu pinzani, kitu ambacho kimesababisha wasipate mabao mengi katika michezo mitano waliyokwisha kucheza na sasa wamekuja na mbinu mpya ambayo itawaumbua wapinzani wao.

Walichoamua kukifanya kwa sasa ni kuhakikisha wanafunga mabao ndani ya dakika 15 za kwanza kabla ya wapinzani wao hawajakaa sawa na zoezi hilo inawezekana likaanzia kwa Kagera Sugar.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanatarajiwa kuondoka leo kwenda Kagera kupambana na Kagera Sugar, mchezo utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii Uwanja wa Kaitaba, ambapo wenyewe walichoamua ni kuhakikisha wanapata ushindi wa mapema.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, George Lwandamina, amekuwa akiwafundisha wachezaji wake mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanamaliza mchezo mapema, hasa safu yao ya ushambuliaji, iliyopo chini ya Ibrahim Ajib na Amis Tambwe, ambaye amepona majeraha yaliyokuwa yakimkabili.

Katika michezo mitano ambayo wamecheza mpaka sasa, mabingwa hao watetezi wamefanikiwa kushinda michezo miwili na kutoka sare mitatu, wakijikusanyia pointi tisa, lakini kinachowaudhi mashabiki wao ni kutokana na kushindwa kufunga idadi kubwa ya mabao.

Katika michezo hiyo wamefanikiwa kufunga mabao manne tu na sasa Lwandamina ameanza kuisuka vilivyo safu yake ya ushambuliaji

kuhakikisha wanapata mabao ya kutosha ndani ya dakika 15 za kipindi cha kwanza, hiyo ikimaanisha kwamba, Kagera Sugar wasipojiangalia wanaweza wakajikuta wakiaibishwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani.

Licha ya kwamba katika mchezo huo Yanga wataikosa huduma ya straika wao, Donald Ngoma, kutokana na majeraha yanayomkabili, lakini hiyo haitazuia chochote kutokana na uwepo wa Ibrahim Ajib, Amis Tambwe pamoja na Obrey Chirwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.