DAKIKA 450 ZA REKODI YANGA V KAGERA SUGAR KAITABA

YANGA V KAGERA SUGAR KAITABA

Dimba - - Special - NA MAREGES NYAMAKA

M ACHO ya wapenzi wengi wa soka nchini wikiendi hii yatakuwa kwenye viwanja viwili nchini, lakini asilimia kubwa wanausubiria kwa hamu mtanange wa aina yake kati ya wapinzani Simba na Mtibwa Sugar, utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Lakini kabla ya hapo, vita kubwa itakuwa mkoani Kagera, pale wenyeji Kagera Sugar watakapokuwa wakiwakaribisha Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba; mechi zote hizo zikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka kote nchini.

Simba na Mtibwa zina pointi sawa kileleni mwa msimamo, isipokuwa Wekundu wa Msimbazi wanajivunia kuwa na mabao mengi ya kufunga yakiwa ni mara mbili zaidi ya mpinzani wake Mtibwa Sugar ya Thobias Kifaru.

Mbali ya upinzani wa wawili hao ambao unachagizwa na uimara wa vikosi vyao, lakini pia kivutio zaidi ni uwepo wa wachezaji watano wa kikosi cha Simba waliowahi kuitumikia Mtibwa Sugar kukutana na kikosi hicho cha zamani.

Na katika mechi ya Kagera Sugar na Yanga, kuna kitu kimoja kinasubiriwa kwa hamu.

Uhalisia wa vikosi hivi viwili hadi sasa una taswira mbili ambazo kila moja itatumia madhaifu ya mwenzako kupata matokeo bora kulingana na walivyosomana michezo iliyopita.

Kagera Sugar ambaye ni mwenyeji wa mchezo, anaonekena kuwa hoi zaidi tofauti na msimu uliopita chini ya kocha wao bora wa msimu uliopita, Mecky Mexime, wakivuna pointi mbili pekee.

Kwa upande wa Yanga ambao wanaonekana kusuasua licha ya kutopoteza mechi hadi sasa wakikusanya pointi tisa, lakini wameonekana kutokuwa kwenye ubora wao wa kucheza soka la kasi muda wote wa dakika 90.

Safu ya ushambuliaji ya Wanajangwani hao haijaridhisha kabisa kutokana na wastani wao mbovu wa kuziona nyavu za wapinzani, kwani hadi sasa wamefunga mabao manne pekee, huku wakiruhusu mabao mawili vyavuni mwao.

Mapungufu ya vikosi hivi viwili ambavyo vilimaliza ligi msimu uliopita kwa kishindo, huenda ukaufanya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na kila upande kusaka matokeo bora.

Hata hivyo, takwimu zinaibeba Yanga katika misimu mitano iliyopita sawa na dakika 450, ambapo Wanajangwani hao wameshinda mitanange mitatu kati ya mitano waliyokutana Uwanja wa Kaitaba, wakifunga jumla ya mabao 10, huku wavu wa Wanajangwani ukiguswa mara tano.

Kati ya ushindi ulioacha rekodi ni msimu uliopita Yanga ikichomoza na ushindi wa mabao 6-2, ambapo inachagizwa na ubora wa uwanja baada ya matengenezo na kuufanya kuwa 'kapeti' kuliko ilivyokuwa misimu ya nyuma.

BALAA LA WANANKURUNKUMBI 2014/15, 2012/13

Kagera Sugar wataingia uwanjani vichwani mwao na jambo moja wakiamini wanaiweza Yanga na ni wakati wa kuondoa gundu la kutokushinda wakiwa na kumbukumbu ya kuwachakaza Yanga katika misimu ya 2014/15, 2012/13. Novemba mosi 2015, bao la dakika ya 52 la Paul Ngway, liliwawezesha Kagera Sugar kuondoka na pointi tatu mbele ya Wanajangwani waliocheza pungufu dakika 20 za mwisho, ikiwa ni baada ya nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Abdallah Kambuzi, lakini pia matokeo kama hayo yaliwakumba Yanga Oktoba 8, mwaka 2013.

MATOKEO YA JUMLA, YANGA INA BALAA KUBWA

Wakati Kagera Sugar ikijivunia rekodi zao mbili za kuwalaza chali Yanga, lakini ni kama wanajiliwaza kwani katika mitanange yote 10 waliyokutana wanankurunkumbi wamefungwa mara nane, huku ugenini Uwanja wa Uhuru na Taifa wakipigwa mechi zote tano.

KUBWA KULIKO

Wastani wa Yanga msimu huu kushinda kwa bao 1-0, inapotokea wameiubuka na ushindi huenda wakaendelea na mwendelezo huo, ambapo tangu wakutane na Kagera misimu hiyo mitano walipata ushindi kama huo 2012/13 kwa kulipiza kisasi kilichowakumba Kaitaba.

Vilevile ile shamra shamra ya mabao 6-2 waliyovuna Yanga msimu uliopita, watashuka dimbani bila ya nyota wake watatu waliokuwa hatari kwenye kikosi msimu uliopita wakifunga miongoni mwa mabao hayo, ambao ni Simon Msuva na Deus Kaseke pamoja na pasi mbili za mwisho kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Kagera wao watakuwa bado wanateswa na kivuli cha Mbaraka Yusuph kutokana na timu yake hiyo ya zamani kuwa na bao moja pekee la kufunga, dhidi ya Yanga Oktoba 22 na ndiye aliyewafuta machozi mashabiki wao katika viunga hivyo kwa kufunga mabao yote mawili.

Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini

Baadhi ya wachezaji wa Kagera Sugar

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.