ANDREA PIRLO

Asante na kapumzike flero

Dimba - - Special - NA NIHZRATH NTANI JNR anakumbukwa sana na staili yake ya 'Panenka'.

O KTOBA 7, 2017, Andres Iniesta, alikuwa anasaini mkataba wa maisha wa kuendelea kuichezea klabu ya Barcelona.

Iniesta akiwa na umri wa miaka 33 hivi sasa, soka lake linaelekea ukingoni. Mkataba huu unaweza kuchukuliwa kama kiini macho au fumbo ndani yake kwa wapenda soka duniani.

Wakati huu ambapo Lionel Messi akiendelea kusuasua kusaini mkataba mpya ulio mezani mwake, atakuwa kabakiza miezi isiyozidi 12 kuhitimisha mkataba wake na Barcelona.

Itakuwa tukio la aibu kwa mchezaji wa kariba ya Messi kuondoka klabuni bure kabisa akiwa angali katika ubora wa kipekee na ndipo mkataba wa maisha kwa Andres Iniesta ulipoibuka.

Jiulize mbona Xavi Hernandez hakupewa mkataba kama huu? Nyuma ya mkataba wa maisha kwa Iniesta ipo nguvu ya Messi.

Kataa au kubali, huo ndio ukweli. Ziko njia nyingi za kumshawishi mtu. Barcelona wameamua kutumia njia hii kumshawishi Messi.

Hili litafanikiwa ikiwa tu harakati za kujitenga kwa Jimbo la Catalunya hazitafanikiwa.

SAA 24 ZENYE FURAHA NA HUZUNI

Ni saa zenye kumbukizi kubwa ndani yake. Wakati ambapo ikitangazwa Iniesta amekubali kusaini mkataba wa maisha kuendelea kuitumikia klabu ya Barcelona, saa 24 baadaye yaani jioni ya Jumapili, Oktoba 8, 2017, gwiji la soka la Italia, ambaye alipata kuwa kiungo wa zamani wa AC Milan na Juventus, Andre Pirlo, alikuwa anatangaza kustaafu soka mwishoni mwa mwaka huu.

Andrea Pirlo kwa sasa anaichezea klabu ya New York City, inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani maarufu kwa jina la MLS. Ni tangu mwaka 2015, huku mkataba wake ukifikia tamati Desemba 31, mwaka huu. Ni kama amebakiza miezi miwili kuanzia sasa.

MAISHA YAKE YA ZAMANI

Ni nadra kwa kijana kutoka familia ya kitajiri kucheza soka kwa kiwango cha juu mno kama Pirlo.

Luis Figo, Ricardo Kaka, Fernando Redondo pamoja naye Andrea Pirlo ni miongoni mwa wacheza soka waliotokea katika familia ya kitajiri mno na baadaye kuja kuibuka kuwa wacheza soka mahiri zaidi duniani. Inasisimua!

Pamoja naye, yuko Rui Manuel Costa ambaye walipata kuwa viungo bora na mahiri katika soka la Italia. Ni wakati wa kilele cha soka lao ndipo walipopewa jina la 'Maestro'. Wachezaji hawa wawili pekee ndio waliotunukiwa jina hili katika soka la Italia. Jina la 'Maestro' asili yake ni huko huko Italia, likiwa na maana ya fundi au mwalimu.

Likitumika zaidi katika fani ya muziki kwa aliye mahiri zaidi. Kupewa jina hili kwa mchezaji katika soka ni heshima ya kipekee.

Akitumia miaka 23 katika soka, Pirlo amecheza jumla ya mechi 755 ngazi ya klabu kwa mashindano yote, huku pia akifanikiwa kucheza mechi 116 ngazi ya timu ya Taifa.

Akifunga jumla ya mabao 86 na kutwaa mataji 17 kwa kipindi chake chote cha kucheza soka hadi makala hii inatoka.

Kiungo huyu miguu yake ya dhahabu ikampatia marafiki wengi duniani, alikuwa kiungo wa kati mahiri sana. Umahiri na kipaji chake utabakia kuwa historia kati yetu.

Katika maisha yake ya soka, alipata kuchezea klabu za Brescia, Inter Milan, Reggina, AC Milan, Juventus na kisha akimalizia soka lake klabuni New York City. Karibu maisha yake yote amecheza ndani ya nchi yake.

ATAKUMBUKWA KWA ALICHOTUONESHA

Umewahi kumuona Andrea Pirlo akicheka? Alikuwa kiungo wa kati akicheza mbele ya safu ya ulinzi. Wakati fulani alipata kucheza kama kiungo mshambuliaji hata winga.

Lakini nafasi ya kiungo wa kati ndio iliyomtambulisha zaidi kama mmoja wa viungo bora kabisa katika historia ya soka duniani.

Katika maisha yake tulimtambua Pirlo kwa kupenda sana kutumia jezi namba 21. Namba iliyokuwa na maana kubwa kwake.

Alipenda kuvaa jezi namba hii kwa sababu Mei 21, 1995 ndio siku aliyocheza kwa mara ya kwanza timu ya wakubwa katika Ligi ya Serie A.

Pia baba yake alizaliwa tarehe 21, huku baba yake akifunga ndoa na mama yake Pirlo tarehe 21. Mambo haya yalimvutia sana Pirlo na kujikuta akipenda kuvaa jezi namba 21, kila mahala anapokwenda.

Pirlo anabakia kuwa mpiga faulo bora katika historia ya Ligi ya Serie A pamoja naye Sinisa Mihjlovic mpaka hivi leo. Kila mmoja akifunga mabao 28 ya faulo.

Alikuwa mtaalamu wa kupiga mikwaju ya penalti na

ANATOKEA FLERO

Bila shaka ataelekea katika eneo alilozaliwa la Flero. Eneo lililopo kaskazini magharibi mwa Mkoa wa 'Lombardia' ndani ya mji wa Brescia.

Pirlo na Iniesta wote wawili wana historia yenye kuhuzunisha. Wote walipata kuwa viungo bora kabisa katika kizazi chao. Hata hivyo, siasa za upinzani wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi zimewafanya wajikute wakipuuzwa.

Wote wawili walistahili angalau kutwaa tuzo ya Ballon d'Or, Wakati mpaka Desemba 31 mwaka huu, Ronaldo anaweza kufikisha tuzo tano za Ballon d'Or.

Mpinzani wake Messi, wakati huu tayari anazo tano kibindoni. Wote wawili watakuwa wametimiza tuzo kumi.

Ni ndani ya miaka kumi ambayo Pirlo na Andres Iniesta walituonesha ubora na umahiri wao. Tukawasahau hawa.

Lakini tutakapokuwa tukitazama kabati la tuzo la Pirlo na mwenzake Iniesta, tunaweza kubakia tukijiuliza kwanini hatukuwapa tuzo walizostahili? Tumewadhulumu!

Ni ngumu kutafuta maneno ya kumwelezea Pirlo ni kiasi gani macho yetu yaliburudika kuona umahiri wake dimbani. Tuseme tu kizazi chetu kina bahati ya kumshuhudia mtu huyu.

Asante pekee haitoshi. Lakini hakuna jinsi. Asante Pirlo kwa wakati wako uwanjani. Asante kwa kile ulichokifanya na kutuonesha. Ni ngumu kushukuru.

Kwaheri Profesa, kwaheri Injinia. Asante Metronome. Asante Maestro. Haya ni majina yako ya utani.

Majina yenye kukutambulisha ewe Pirlo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.