PETE YA NDOA ILINITOKEA PUANI- (16)

(ZAMANI NILIOA MASHETANI WAWILI

Dimba - - Special - NA ALLY MBETTU SIMU: 0713 646500

Nilikumbuka msisitizo wa mke wangu Lukaiya juu ya kuvaa pete ya ndoa baada ya kumuoa lakini nilipuuza hata alipopeleka mashtaka kwa Salum kupitia ndotoni bado niliyapuuza hasa baada ya kuona gharama ya pete anayoitaka yeye ni kubwa.Ajabu pesa nilipata lakini bado moyo wa kununua sikuwa nao. Ukimya wa mke wangu Lukaiya ya kutonisumbua ulinifanya niamini ameamua kuachana na suala la pete ya ndoa kwa vile muhimu kwake kubwa ulikuwa ndoa na si hicho alichokuwa akikikazania lakini kumbe alikuwa na maana yake kubwa. SASA ENDELEA ....

Baada ya mganga kulijua tatizo langu alianza kunipa tiba rasmi ya tatizo langu, kwanza alianza kuyaondoa majini machafu na kumtuliza mke wangu ambaye alikuwa na machungu kwa kitendo changu kukaidi ombi lake la mimi kuvaa pete kupelekea kumruhusu jini mwingine kuingia ndani.

Si wanaadamu wenye wivu wasiopenda ushirika wa mapenzi hata majini nao vilevile hawapendi uke wenza japokuwa wanajua sheria ya mwanaume kuoa wanawake wanne. Walikuwa ladhi ufanye kitu kingine lakini si uke wenza hasa kwa majini wenzao. Lakini kwa binadamu hawakuwa na wasiwasi kwa vile walikuwa wana uwezo wa kuwakabili tofauti na wenzao.

Mganga alinieleza kuwaLukaiya alikuwa amejiapia kunitia adabu kwa kile nilichomfanyia, wale majini wachafu hawakumuumiza sana moyo wake kwa vile aliamini ni wapitaji si wakaaji kama jini aliyeingia na kuapa kukaa naye nyumba moja kama wake wenza.

Ilibidi afanye kazi ya ziada kumwita Lukaiya ambaye alikuwa akilia siku zote toka jini mwenzie kuingia ndani ya himaya yake. Baada ya kuja aliombwa radhi sana na kubembelezwa sana na kuahidiwa zawadi. Lukaiya alikubali kunisamehe kwa vile alikuwa akinipenda sana huku akitoa sharti moja ya kuhakikisha naitafuta pete ya ndoa kabla hajaingia jini mwingine.

Jini mwingine aliyeingia naye alisema kuingia ndani baada ya kukuta mlango upo wazi hivyo hakuwa na kosa lolote. Aliulizwa kwa nini asitoke kwa vile amemkuta mwenzake alijibu kama ameisha ingia basi atoki tena ila kama angekuta kuna kufuli(pete) asingeingia ndani, lakini kwa vile nyumba ilikuwa wazi aliamini hakukuwa na kitu ndani hivyo aliingia kwa kujiamini.

Pia alisema kwa vile sheria ya dini ya kiisalamu inaruhusu mwanaume kuoa zaidi ya mwanamke mmoja hivyo haoni sababu ya yeye kutoka ila kama mimi ningekuwa mkristo asingebaki angeondoka. Hivyo naye alikuwa akijiandaa kunipeleka ujinini kwa mara ya pili kufunga ndoa kama niliyofunga na Lukaiya.

Jini wa pili alikuwa anaitwa Hulkati alimuahidi mganga zawadi kubwa kama ataifanikisha ndoa yake na mimi. Baada ya kuwatuliza majini wote ambayo aliwaita

kwa pamoja na kuwapatanisha na kutambuana kama ndugu wa familia moja nikiwa mimi ni mume wao.

Walikubaliana mbele ya mganga kuwa kitu kimoja na kunitunza kama mume wao. Baada ya makubaliano nilipewa dawa za kutumia nilipewa ruhusa ya kurudi nyumbani nikiwa mzima wa afya njema baada ya kukaa kwa mganga kwa wiki nzima. Kwa vile nilirudi nyumbani siku ya ijumaa, nilipumzika kwa siku mbili kabla ya kurudi kazini kuendelea na kazi.

Siku niliyorudi nyumbani mke wangu Lukaiya hakujitokeza zaidi ya kujitokeza Hulkati mubashara kwa mara ya kwanza nilimuona. Kwa kweli Hulkati ni mwanamke mzuri kiasi cha kunichanganya kushindwa kujua nani kamzidi mwenzake. Baada ya kujitokeza alinieleza kuwa usiku wa siku inayofuata atanichukua kunipeleka kwao kwa ajili ya kufunga ndoa ili naye awe mke halali kama Lukaiya.

Kutoonekana Lukaiya kulinishtua sana na kujiuliza kwa nini hakuonekana hata kwenye njozi sikumuona nilijua kitendo cha kumruhusu Hulkati kimemuuzi sana japokuwa alikubali kwa mganga kuwa hana tatizo tena na mimi na amempokea mwenzake

kama mdogo wake lakini kumbe alikuwa na siri yake moyoni.

Usiku wa Jumamosi nilichukuliwa kupelekwa ujinini katika familia ya Hulkati ambako nilifunga na kurudi nyumbani usiku uleule. Baada ya ndoa yangu ya pili niliyaanza maisha ya kuoa wanawake majini wake wenza.

Lakini ajabu na mshtuko kwangu siku zote saba za mwanzo toka nifunge ndoa na Hulkati sikumuona mke wangu kipenzi Lukaiya kitu kilichonitia unyonge moyoni na kuonesha jinsi gani nilivyo mkosea na kumuumiza mke wangu. Siku zote nilizokuwa na Hulkati ilikuwa yenye mapenzi shatashata kitu kilichoniweka njia panda kwani walikuwa wakishabihiana karibu kila kitu.

Siku ya nane kwangu ilikuwa na mshtuko baada ya kutoonekana Hulkati wala Lukaiya kitu kilichozidi kunitia wasiwasi na kujiuliza kuna kitu gani kimetokea kiasi cha mke wa kwanza kuondoka bila taarifa na wa pili naye kutoonekana ghafla. Nilijikuta mtu mwenye mawazo mengi juu ya matukio yaliyonitokea.

Siku ya tisa baada ya kutoka kazini nilijikuta mtu mwenye mawazo mengi ya kutoweka kwa wake zangu bila taarifa

hasa Lukaiya ambaye nilijiapiza pindi atakaporudi nitamuomba msamaha ili anisamehe na kuwa tayari kuyafuata yote anayotaka japokuwa niliamini kama atataka nimpe talaka Hulkati ingekuwa vigumu hasa kutokana na kusema mwenyewe hawezi kutoka na yote niliamini ni makosa yangu.

Baada ya kutoka kazini niliingia chumbani kwangu na kujifungia kwa vile sikutaka kuzumgumza na mtu hata simu zangu nilizizima kwa vile sikutaka usumbufu wa mtu kwani nilijiona mkosefu mkubwa kwa Lukaiya mwanamke aliyenipenda na kujitoa kwangu huku akiyabadilisha maisha yangu.

Kutoweka ghafla kwa Lukaiya nilijiuliza nini hatima yake, kama kweli atatimiza kile alichokifikiria kunifanyia nini kitanipata. Nilijiuliza na Hulkati naye yupo wapi ikiwa ndiye aliyeingilia ndoa yangu. Nilijikuta nikipata jibu kuwa alikuja kwangu ili kuiharibu ndoa yangu kisha aondoke.

Lakini swali likabaki kama alikuja kuharibu ndoa yangu kwanini alinipeleka kwao ujinini kwa ajili ya kufunga ndoa huku ikifanyika sherehe kubwa. Kwa kweli siku hiyo kidogo kichwa kipasuke kwa kufikiria bila kupata majibu ya maswali yangu.

ITAENDELEA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.