JINI MKATA KAMBA-19

Dimba - - Special - Na Mawazo Lusonzo (Ferguson) Simu 0772 677 633 ITAENDELEA A

ILIPOISHIA JUMATANO ILIYOPITA.. WAKATI huu ambapo haya yanawaumiza vichwa huko kijijini, Emma alionekana akiitikia jambo alilokuwa akiambiwa na mama mzazi wa Eyana juu ya nini kilichombele yao hivi sasa. "Ninachoshukuru kwenu nyote ni hatua ya utayari wenu wa kutufariji sisi wazazi wenu kwa kuamua kufunga ndoa inayotokana na ridhaa yenu .... si ndiyo wanangu?" SASA ENDELEA ....

Alizungumza mama Eyana huku akiwatupia macho akina Emma na mpenziwe huyo wakiwa wameketi varandani hapo bila ya kuwepo baba wa msichana huyo, ambaye tayari aliondoka mapema nyumbani hapo kwenda katika kusimamia miradi ya kampuni zake.

"Ndiyo mama, nadhani hadi nimeamua kuja huku kwa ajili ya kukutana nanyi, ni ishara ya kwamba nimeshaamua kuyatekeleza yote tuliyopanga sisi wawili."

Jibu hili lilionekana kumfariji mno mama huyo, ambaye hakuficha ukweli kuwa, harusi waliyoipanga itakuwa miongoni mwa zilizolifanya Jiji la Ankara lizizime na kuacha historia nyuma yake!

"Nimefurahi kusikia pia kuwa wewe ni kijana ambaye bado hujaoa na kwamba, hakuna kipingamizi chochote cha kutekeleza mlichoamua kutoka ndani ya

nafsi zenu?".

Katika mazingira ya kigugumizi flani hivi, Emma alijikuta akipata shida ya kujibu haraka haraka, kwani mkanda wa kumbukumbu ya siku ya harusi ya kimila waliyoifunga na mkewe aliyemwacha kijijini Lusende ulipita ndani ya fikra zake, akaonekana kama ni mtu aliyeduaa kwa sekunde hivi!

Lakini, ndani ya nafsi ya kijana huyo ni kama alishapitisha uamuzi wa kutaka kusahau kila aliloliahidi kule kwao.!

Tamaa ya maisha mazuri na hata matarajio ya kurithi mali na utajiri wa familia ya baba ya mchumba aliyenaye (Eyana) ilitosha kabisa kuazimia kuzungumza uongo ili mradi kila jambo lililowafanya wasafiri hadi huko ukweni liweze kutimia.

Sekunde za kusubiri kutoa majibu zilitosha kabisa kurejesha fikra zake huko kijijini kwao, aliangalia madhari ya nyumba ya baba yake, hali ya familia yao, Emma alijikuta akitikisa kichwa!

Alifanya hivyo huku akirejesha fikra hizo na kutua juu ya uso wa mke aliyemwacha huko kijijini, akamfananisha na Eyana, hakuona ulinganifu wa karibu!

"Ninawezaje kuacha bahati hii ya mti wa mtende ya kuota katika ardhi ya jangwa iliyozungukwa na uhaba wa maji na mimea hai!!?

Emma alijiuliza nafsini huku akijishtukia tu akijisemesha kimoyomoyo .....

"Liwalo na liwe, maana hata wahenga waliyanena ya kwamba, Maadamu umesaula nguo ndani ya maliwato kwa ajili ya kuoga, huna budi kutekeleza lililo mbele yako ...... "

Jibu likamtoka haraka haraka .... ".... Ni kweli mama, mimi sijaoa na ndiyo maana nimekuja huku kwa ajili ya utambulisho mbele ya ninyi wazazi."

Kauli hii ilimfanya mama yake Eyana afurahi kwa kupiga makofi, kama ishara ya faraja iliyomo ndani ya nafsi.

Alifarijika kutokana na ukweli kuwa, Eyana alihitajika kupata mchumba wa kumuoa kabla ya wazazi wake hao hawajaaga dunia na hilo lilikuwa linazungumzwa kila siku na wao kama wazazi! Baba yake Eyana ndiye aliyekuwa kinara wa kuuliza swali la lini atafanya sherehe ya harusi ya mwanae huyo pekee ndani ya familia yao hiyo ya kitajiri.

Hivyo hatua ya jibu hilo ni kama linatoa ishara ya kwamba, harusi waliyokuwa wakiitarajia ipo jirani kufanyika!

Wakati huu, huko kijijini kwao Emma wanaonekana baadhi ya wanafamilia wakijikusanya nyumbani kwa mzee Haikosi wakisubiri kuanza kwa kikao cha kujadili kila linalohusu tambiko hilo la kimila na hatua ya kukatika mawasiliano na kijana wao huyo!

Ilikuwa jioni iliyokuwa na hofu ya kunyesha kwa mvua za vuli, kwani jua halikuwahi kuonekana siku hiyo!

Anga la kijijni hapo lilifunikwa na mawingu ya mzimbaa, yalishindwa kutoa nafasi kwa jua kuangaza miale yake, hivyo kuzusha hofu ya kunyesha kwa mvua wakati wowote! Hali hiyo ndiyo iliwalazimu wanafamilia kujikusanya mapema kwa ajili ya kikao hicho ili kimalizike mapema kila mmoja aweze kurejea makwao!

Mzee Haikosi ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hicho wakati huo ambaye alionekana kukosa raha kutokana na ukimya wa mwanae (Emma) wakati huo walisikika wakizozana na mkewe ndani ya nyumba yao, huku hoja ikiwa utayari aliouonesha mzee huyo!

Utayari wa kwamba, endapo pakitokea ukimya wa mawasiliano hadi inafika siku ya tambiko, basi hana sababu ya kuzuia nguvu ya mizimu kutoa adhabu inayostahili Emma, kwa kile kinachoonekana kudharau mahitaji ya kuhudhuria siku ya tambiko hilo!

Msimamo huu unakwenda kinyume na matakwa ya mama Emma anayemtaka mumewe huyo kurejea katika kibanda cha mizimu ya tambiko ili kwenda kumtolea dharura kijana wao huyo pindi akishindwa kutokea katika tukio hilo la tambizi la ukoo!

Kinachoonekana ndani ya dhamira ya mama Emma ni ule msemo wa wahenga walionena ya kwamba, 'Uchungu wa mwana aujuae mzazi'! Kwa mama huyo hakuwa tayari kuona mwanae huyo pekee wa kiume anapata madhara yatokanayo na adhabu ya jadi ya ukoo wa mzee Haikosi!

Lakini, msimamo wa mzee Haikosi ulionekana kutosikiliza hoja ya mkewe, badala yake alitoka nje tayari kwa ajili ya kuanza kikao hicho huku akiwa amekunja 'ndita' juu ya paji lake la uso!

Alipofika mbele ya familia, mzee huyo alionekana kuhofia hali hiyo ya ishara ya kunyesha kwa mvua, hivyo alikiendesha kikao kwa mtindo usiozoleka na wanaukoo ambao walizoea urefu wa kikao vya namna hiyo.

"Jamani ..... mimi sina hoja ndefu leo, maana huko juu (ananekana akiangalia mawinguni) hakuna ishara njema ya kukosa kunyesha mvua kubwa leo".

"Hivi kutokana na hali hii, ninachoweza kusema ni kwamba, hoja ya kikao cha leo kila mmoja anaijua, kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi huu ulioandama hivi karibuni, tutafanya lile tambiko letu!".

"Kama ilivyo ada, kila mmoja anatambua wajibu wake wa kujiandaa na kila linalohitajika katika kufanikisha shughuli yetu hii, ikiwemo suala la kuitana kila mtu aliye mbali na hapa apate kuja pasipo kukosa".

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.