Msimbazi kuchafua rekodi kwa Wakata miwa?

Dimba - - Special - NA MARTIN MAZUGWA

KATI ya timu zilizo katika ubora wa hali juu msimu huu ni klabu ya Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’, yenye maskani yake mitaa ya Kariakoo ambao ndio vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakiwa na pointi 11.

Simba wanaongoza ligi lakini wakiwa sawa na Mtibwa Sugar, ambao pia wana pointi 11 huku wakali hao wa Msimbazi wanatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Miamba hii inakutana wikiendi hii katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo huu utakuwa mchezo wa 11 kuwakutanisha wakali hawa, ambapo katika michezo hiyo Simba ameshinda mara sita sare tatu huku Wakata miwa hao wakishinda mara mbili katika kipindi cha miaka mitano.

Jumla ya mabao 13 yametinga nyavuni huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na mabao tisa na Wakata miwa hao kutoka Manungu, Turiani, wakiwa na mabao manne pekee.

Mchezo huo unapaswa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uwezo wa timu hizo huku Mtibwa akionekana kuimarika zaidi mwaka huu, ambapo hadi sasa hajapoteza mchezo sambamba na Simba ambao wameshinda mechi tatu na kutoa sare mbili.

NI VITA YA NDUGU

Mechi hii inatafsiriwa kama vita ya ndugu kutokana na mwingiliano wa wachezaji, ambapo katika kikosi cha Simba kuna nyota zaidi ya watano kutoka Mtibwa ambao wamejiunga hapo kwa misimu ya hivi karibuni.

Nyota hao ni pamoja na Salim Mbonde, Ally Shomari, Mohamed Ibrahim ‘Mo’ , Mzamiru Yasin, Said Mohamed pamoja na Shiza Ramadhan Kichuya.

Wakati kwa upande wa Mtibwa kuna nyota wanne wamepita katika kikosi cha Msimbazi ambao ni Issa Rashid ‘Baba ubaya’, Shaban Nditi, Henry Joseph ‘Shindika’ pamoja na Salum Kanoni ambao wapo katika ubora wa hali ya juu msimu huu.

MTIBWA KUENDELEZA UTEJA KWA SIMBA?

Mtibwa amekuwa akipata shida zaidi kupata matokeo katika mchezo dhidi ya Simba katika kipindi cha misimu minne mfululizo, ameshindwa kupata alama tatu ameishia kupata pointi moja pekee.

Katwila ataweza kuufuta uteja huu ambao ulimshinda kocha wa zamani wa timu hiyo, Mecky Mexime, ambaye hivi sasa anakinoa kikosi cha Wakata miwa wengine Kagera Sugar ni jambo la kusubiri na kuona.

NYOTA WA KUCHUNGWA KATIKA MCHEZO HUO

Baadhi ya nyota ambao wanatarajiwa kutupiwa macho na mashabiki katika mchezo huo kutokana na kuwa katika kiwango bora, ni mshambuliaji Emmanuel Okwi, John Bocco pamoja na kiungo fundi Haruna Niyonzima.

Wakali hawa ambao wamejiunga na Simba msimu huu licha ya ugeni wao, wamekuwa moto wa hali ya juu huku Mganda Okwi akiongoza kwa upachikaji wa mabao akiwa tayari ameingia wavuni mara sita.

Kwa upande wa Mtibwa, wakali ambao watatupiwa macho zaidi ni kiungo wao fundi na injini yao Mohamed Issa ‘Banka’ , Said Dilunga pamoja na mshambuliaji, Stahimili Mbonde, ambao wamekuwa katika kiwango bora zaidi msimu huu.

NI OMOG AU KATWILA KUONDOKA NA KICHEKO?

Makocha wawili ambao wameanza msimu wakiwa hawajapoteza mchezo katika michezo mitano ambayo tayari wameshuka dimbani, huku kila mmoja akishinda mara tatu na sare moja nani atakuwa wa kwanza kupoteza ndilo swali lililopo kwa wapenzi wa mchezo wa soka.

Katwila ambaye alikabidhiwa timu msimu uliopita mara baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi cha Mtibwa, Salum Mayanga, kukabidhiwa timu ya Taifa hivyo na yeye kupewa rasmi nafasi ya kuwa kocha mkuu ambapo ameanza kwa cheche mwaka huu.

Wachezaji wa Simba wakiwa mazoezini

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.