NIYONZIMA ASHTUKA, ATEMA CHECHE

Dimba - - News - NA MWANDISHI WETU

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Haruna Niyonzima, ameichungulia mechi dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, Jumamosi ijayo, kisha akagundua kuwa ngoma itakuwa ngumu kwa pande zote, lakini akawaambia mashabiki wao wasife moyo, kwani wachezaji watapambana kuhakikisha wanashinda.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kabla ya kikosi hicho kwenda Zanzibar kuweka kambi, Niyonzima alisema mara kwa mara timu hizo zinapokutana si rahisi kujua nani ataibuka na ushindi, lakini akawatoa wasiwasi mashabiki wao kwamba maandalizi wanayoyafanya yatazaa matunda.

“Huwa hizi timu zinapokutana si rahisi sana kujua nani anakwenda kushinda, kwani kila moja inajiandaa kivyake, lakini yote kwa yote niseme mchezo utakuwa mgumu, japo sisi tumejiandaa kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu,” alisema.

Niyonzima, ambaye alitokea Yanga kabla ya kujiunga na Simba, ni mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kung’ara katika mchezo huo kutokana na aina ya uchezaji wake na pia kujua falsafa za timu hizo kongwe.

Kwa sasa Simba wamejichifa Zanzibar, wakijifua vilivyo kuhakikisha wanawatoa nishai wapinzani wao hao wa jadi, huku Yanga wenyewe wakiamua kuikacha kambi yao ya mara kwa mara ya Pemba, na kwenda mkoani Morogoro.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.