YANGA INA ZALI MWEZI OKTOBA

Mo amwaga fedha kuiua Yanga J'mosi

Dimba - - Front Page - NA CLARA ALPHONCE

KAMA mashabiki wa Simba wataisoma hii, wanaweza wakaghairi kufika uwanjani, lakini ndio ukweli ulivyo, kwamba watani zao, Yanga, wanakuwa na bahati ya kupata matokeo mazuri timu hizo zinapokutana mwezi Oktoba.

Lakini hiyo bado isiwape presha sana mashabiki hao wa Simba, kwani kama mchezo huo utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii utafanyika Uwanja wa Uhuru, inabidi wamiminike kwa wingi, kwani rekodi za michezo mitatu ya mwisho zinaonyesha kuwa matokeo si mabaya.

Mechi hizo tatu za mwisho kuzikutanisha Simba na Yanga, Uwanja wa Uhuru, zote zilimalizika kwa suluhu ya 0-0, zikichezwa, Machi 26, 2006, na mwingine, Oktoba 29, 2006, huku wa tatu ukiwa Aprili 27, 2008.

Timu hizo mbili zimekuwa na upinzani mkubwa tangu zilipoanzishwa miaka ya 1935 na 1936 na kuleta ushindani mkubwa katika ligi hapa nchini, na kuchukua hisia za wapenzi wengi wa soka.

Kwa ujumla timu hizo zimekutana mara 102 na Yanga wameshinda mara 38, huku Simba wakishinda mara 32 na wametoka sare mara 32.

Takwimu za miaka mitano iliyopita kuanzia 2009 zinaonyesha kuwa, Simba na Yanga zimekutana mara 11, ikiwa ni mechi maalumu pamoja na zile za Ligi Kuu ya Tanzania bara. Kwa kipindi hicho, Simba inaongoza kwa kushinda mara nne na Yanga ikipata ushindi mara tatu na mara nne zikienda sare, lakini kizuri kwa Yanga ni kuwa na bahati ya kupata ushindi inapokutana na Simba mwezi Oktoba. Oktoba 16 mwaka 2010, timu hizo zilikutana Uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza, katika mchezo wa Ligi Kuu na Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, mfungaji akiwa Jeryson Tegete dakika ya 70.

Yanga ilifanya tena hivyo, Oktoba 29/2011, katika Uwanja wa Taifa, ambapo walipata ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Mzambia Davis Mwape, dakika ya 75.

Oktoba 3/2012, Simba walikataa kufungwa na kukomaa na hatimaye timu hizo zikatoka na sare ya kufungana bao 1-1, mabao yakifungwa na Amri Kiemba dakika ya tatu kwa upande wa Wekundu hao wa Msimbazi na lile la Yanga likifungwa na Said Bahanuzi.

Oktoba 20,2013, kwa mara nyingine timu hizo zilitoka sare baada ya kufungana mabao 3-3, huku Yanga wakifunga kipindi cha kwanza na Simba kuyasawazisha yote kipindi cha pili.

Wafungaji wa Yanga katika mechi hiyo walikuwa ni Mrisho Ngasa, aliyefunga bao la kwanza dakika ya 14 na Mganda Hamisi Kiiza, aliyefunga mara mbili dakika ya 35 na 47. Mabao ya Simba yalifungwa na Betram Mwombeki dakika ya 53, Joseph Owino, dakika ya 55 na Mrundi Gilbert Kaze dakika ya 83.

Oktoba 18, mwaka 2014, washambuliaji wakongwe wa Yanga walishindwa kumfunga kipa mdogo wa Simba, Peter Manyika, timu hizo zikitoka sare ya 0-0.

Mwaka 2015, mechi ilipigwa Septemba 26, yaani siku nne kabla ya kuingia mwezi Oktoba, lakini Yanga ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na washambuliaji, Mrundi Amis Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79, kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa.

Mchezo wa marudiano pia, Yanga ikashinda 2-0 Februari 20, mwaka 2016, mabao ya washambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma dakika ya 39 na Tambwe dakika ya 72.

Mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Oktoba 1, mwaka 2016, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Tambwe akianza kuifungia Yanga dakika ya 26, baada ya kuuseti mpira kwa mkono bila refa kuona, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87 Uwanja wa Taifa.

Ushindi pekee walioupata Simba ndani ya mwezi Oktoba dhidi ya Yanga katika miaka mitano iliyopita ilikuwa ni Oktoba 31, mwaka 2009, ambapo iliweza kuifunga Yanga bao 1-0, mfungaji akiwa Mussa Hassan ‘Mgosi’, dakika ya 26.

Timu hizo kwa sasa zipo mafichoni kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi, huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kufanya vizuri katika mchezo huo kutokana na michezo yao ya mwisho ambapo kila moja imepata ushindi mnono wa mabao 4-0.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.