Mo amwaga fedha kuiua Yanga

Dimba - - News - NA SAADA SALIM

SI unakumbuka jinsi Mohamed Dewji (MO), alivyomwaga fedha na kufanya usajili wa kutisha Simba? Sasa bilionea huyo maarufu ndani na nje ya nchi wala hajachoka na badala yake amewaambia wachezaji kama watakomaa na kuifunga Yanga Jumamosi, atawamwagia neema nyingine.

Timu hizo zitakutana Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, ambapo tayari Simba wanajifua vikali Visiwani Zanzibar, huku Yanga wakiamua kuikacha kambi yao ya Pemba na kwenda kujificha mkoani Morogoro. Taarifa ambazo zimenaswa na DIMBA Jumatano kutoka kwa kigogo mmoja ndani ya klabu hiyo zinadai kwamba, tayari Mo amewahakikishia wachezaji kwamba kama watampa raha siku hiyo, naye hatawaangusha.

"Si unajua yule jamaa (Mo), anaipenda sana hii timu na ameahidi kwamba kama wachezaji watajituma na kushinda, naye atawapa kifuta jasho, kwani huwa anafurahi sana tunapowafunga Yanga,” alisema kigogo huyo.

Alizidi kudokeza kwamba, mbali na Mo, pia wapo baadhi ya matajiri ndani ya klabu hiyo nao wameahidi kumwaga fedha za kutosha kwa wachezaji kama watawatoa nishai watani zao hao wa jadi na kuondoka na pointi zote tatu.

"Mbali na Mo, pia kuna wengine nao wameahidi mambo makubwa siku hiyo kama timu itashinda, kwani kama unavyojua, Simba inao watu ambao kutoa fedha wanaona si tatizo kabisa, tunaamini kwamba mambo yatakuwa tu mazuri,” alisema.

Wakati huo huo, mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema timu inaendelea kujifua vikali Zanzibar, huku akidai kwamba, straika wao, John Bocco, ameanza mazoezi kuwawinda Yanga.

"Bocco amejiunga na wenzake tayari na asubuhi ya leo (jana) alifanya mazoezi katika Uwanja wa Amaan, suala la kucheza litakuwa liko chini ya benchi la ufundi, linaloongozwa na kocha Joseph Omog,” alisema Abbas.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.