Tabia ya mashabiki Simba, Yanga kupigana viwanjani ikomeshwe

Dimba - - Jumapili -

ANA Oktoba 28, tukio la mashabiki wa klabu za soka Simba na Yanga kupigana ndani ya Uwanja wa Uhuru kutokana na kutofautiana kiitikadi zimejirua tena.

Baadhi ya mashabiki wamepigwa na hata kuchaniwa nguo zao eti kwa sababu walikosea na kupita maeneo ambayo mashabiki wa klabu fulani ndiko wanakostahili kukaa.

Hili si tukio la juzi wala jana ni uhuni unaojitokeza mara kwa mara na kuleta usumbufu na pia kudhalilisha baadhi ya wapenzi wa soka kutokana na ushabiki ambao unaonyesha ulimbukeni na ushamba uliopitiliza.

Ipo mifano mingi ya kulaani matukio kama haya, moja ni lazima tukubali kwamba mashabiki wote wanaoingia kuangalia mechi za timu hizi za watani wa jadi yaani Simba na Yanga si wote wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam au waliozoea kuingia katika viwanja hivyo.

Lakini pia hakuna sehemu yoyote ambayo mpenzi wa soka anaweza kupata maelekezo ya sehemu gani anaruhusiwa kukaa na ipi hatakiwi kufika hata kama atakuwa na tiketi inayomruhusu kuingia uwanjani.

Sisi Dimba tunajua kwamba, wapo mashabiki wengi wanashabikia klabu hizi kubwa, lakini hawana uzoefu na viwanja vya Dar es Salaam, hivyo wanapofika jijini wanachotambua ni kulipa fedha na kukata tiketi na kisha kuingia uwanjani kupata burudani.

Lakini inapotokea shabiki huyo kujikuta akishambuliwa na makundi ya watu eti tu kutokana na rangi ya nguo aliyovaa kwa kweli haileti tafsiri nzuri na inaleta wasiwasi kwa wananchi wanaostahili kupata burudani bila kubughudhiwa.

Sisi Dimba tumesikitishwa sana na matukio yaliyofanywa na mashabiki ambao leo hatuna haja ya kubainisha ni wa upande gani, kwani nia yetu ni kuzitaka mamlaka zinazohusika kutafuta mwarobaini utakaoponya gonjwa hili lililoota mizizi baina ya mashabiki wa Yanga na Simba.

Ifikie wakati sasa tuachane na upenzi wa kizamani na kukubali kwamba dunia sasa imepiga hatua, hivyo isitokee upenzi wa mtu fulani ukawa kero kwa mwingine.

Kwetu sisi tunaona tabia hizi ni za kibaguzi kwani Watanzania wanaweza kuwa na ushabiki wa klabu moja, lakini hayo yakabaki kuwa mioyoni mwao na kutokuwa kero kwa mwingine.

Tunatamani kuiona Bodi ya Ligi iliyopata uongozi mpya wiki iliyopita chini ya Uenyekiti wa Clement Sanga, ukaliangalia tatizo hili na kulipatia ufumbuzi.

Kamwe hatukatai kuwepo na taratibu za kupanga mashabiki maana hizo ni hulka zinazoendelezwa na nchi nyingi duniani, lakini angalau basi kuwepo na taratibu ambazo zitamwongoza shabiki fulani kupita na kuketi sehemu fulani ili asikumbane na kadhia asiyoistahili.

Rai yetu pia inalenga kuziba ufa kabla hatujajenga ukuta, maana bado tunakumbuka matukio yaliyopita ambapo mashabiki walithubutu hata kuharibu miundombinu ndani ya kiwanja kikuu cha Taifa, sembuse leo tena yanajitokeza matukio ya watu kushambuliana ndani ya uwanja.

Tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa kusimamia ulinzi wa ndani na nje ya uwanja huo ambao kwa hakika ulihemewa na idadi kubwa ya watu, lakini idadi kubwa ya mashabiki ilipata nafasi ya kukaa na kuangalia mchezo huo na kurejea majumbani mwao salama.

Nia yetu ni kuona siku za usoni mpenzi wa soka anaweza kuingia uwanjani bila hofu ilimradi ametimiza masharti ya kulipa kiingilio.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.