LOST BEN

KIJANA ANAPOTEA, TATIZO NI MBAPPE, NEYMAR, DI MARIA AU KOCHA EMERY?

Dimba - - Jumapili - Na Ally Kamwe 0655 321415 kamweally@yahoo.com 'Nifollow Insta' Instagram: Kamwejr Nani anaweza kumsaidia mshkaji wetu? Claude Puel? Hebu jaribu basi, tunamhitaji tena Ben.

WANASOKA wengi wa sasa, hasa wale waliopo kwenye mitaa yetu, wakisota na vumbi huku wakijua wazi kuna wadau wanaowatazama watakaoweza kuwasaidia, mfano, hebu tuwatazame wale wanaocheza nafasi za ushambuliaji, kutokea pembeni…

Katika majibu yao juu ya namna wanavyopenda kucheza, lazima tu watajieleza namna hii:

‘Napenda kukimbia pembeni na kufinyia ndani.’

Naam, atakuelezea hivyo huku kiganja cha mkono wake wa kushoto kikipindia upande huo huo.

Nawe picha itakujia. Utamtazama mwili wake, umejengeka kimazoezi. Halafu utapata taswira ya mshambuliaji matata, mwenye pumzi, nguvu, miguu yenye wepesi wa hali ya juu akiwa na mpira.

Ndiyo, utakapomwona uwanjani, utafurahishwa jinsi anavyojaribu kufanya kila kitu kwa kutumia maarifa na akili aliyobarikiwa.

Kwa wakati huo atakufurahisha, lakini ukifikiria nje ya boksi, wachezaji wa aina hii ambao hujaribu kufanya vitu vingi wenyewe, inaweza kuwa ndio uwezo ama kipaji alichobarikiwa, lakini, ni udhaifu mkubwa unaowatafuna wengi baadaye.

Ni aina ya wachezaji wanaohitaji kudekezwa sana, ndiyo maana ni ngumu kwa aina yao kudumu kwenye ramani ya soka kama akikutana na kocha asiyejua kucheza na saikolojia yake.

Amini, ni ngumu kufundisha timu iliyojaa wachezaji wanaopenda kucheza kivyao. Lakini hakuna kazi ngumu kwenye soka kama kumfundisha mtu wa aina ya Hatem Ben Arfa kama haujazoea kuishi nao.

Ngumu sana. Aidha, kocha ulaumiwe kwa kipaji chake kupotea na kusababisha aangukie kwenye kifo cha soka badala ya kudumu. Au mchezaji mwenyewe akakiri alikosea tangu awali.

Ben Arfa anaelekea kuangukia kwenye kifo cha soka.

Na hawezi kukubali ni yeye ndiye chanzo. Anaumia ndani kwa ndani. Inasikitisha.

Ndiyo maana hatuchoki kumsubiri arudi tena kama zamani.

Hebu tulia na umkumbuke Ben Arfa wa miaka tisa nyuma. Muda mrefu kidogo.

Yule alikuwa ni winga hatari, hatari kweli kweli.

Akiwa katika klabu ya Lyon, Ben Arfa alionekana kumudu vyema jukumu la kutengeneza nafasi kwa wenzake. Alikuwa mchezaji mwenye faida uwanjani.

Guu lake la kushoto liliwaka mithili ya almasi kila alipougusa mpira, alikuwa ni ‘Sensationnel’ (alitisha).

Kocha yeyote angejaribu kumwelekeza Ben Arfa asiwe anashambulia, bali atulie nyuma na kumlinda beki wake wa pembeni, nakuhakikishia, angeonekana mjinga sana. Unadiriki vipi kumwambia Messi afanye hiyo kazi hiyo unayotaka Ben Arfa aifanye?

Mchezaji wa kariba ya Ben Arfa, ana uwezo wa kufanya kitu ambacho hujawahi kukiona kokote kule. Kitu ambacho hujawahi kukipatia picha. Aina ya mabao aliyokuwa akifunga ni yale ambayo hata wataalamu wa kutengeneza filamu za michezo waliwaza na kujaribu kutengeneza filamu ya shujaa wa soka aliye kwenye maisha ya uhalisia.

Huyo ndiye Ben Arfa. Mchezaji anayefanya maajabu kwenye maisha ya kweli.

Ilikuwa ni ngumu kutabiri atakachokifanya sekunde tatu baadae akiwa na mpira mguu mwake lakini tayari unakuwa ushajua kuna kitu cha ajabu kitatokea.

Angeweza kukokota mpira kwa kasi ya roketi na kuwapita wachezaji wanne au watano, akichanganya miguu kwa chenga za gemu la Fifa. Simple like that.

Angeweza kufunga bao la dakika za mwisho kwa mguu wowote, na mpira ungeenda kutua nyavu za juu, pembeni kabisa. Kwisha kazi.

Angeweza kufunga bao kali la mpira wa adhabu kutoka umbali wa yadi 40. Kwenye pembe ngumu mno.

Katika kizazi cha wachezaji walioibuka 2008, akina Bojan Krkic, Alexandre Pato, Mario Balotelli, Ivan Rakitic, ilikuwa ngumu kuliacha jina la Ben Arfa na mwenzie Karim Benzema waliokuwa wakitishia vigogo na kikosi cha Lyon.

Kilichomfanya aondoke Lyon na kuhamia Marseille ni ujeuri na ukorofi.

Hivyo vitu vimeharibu maisha ya soka ya Ben Arfa.

Vimechangia kwa kiasi kikubwa kumpoteza kwenye ramani haraka kuliko mvurugiko wa anga, juu ya kisiwa cha Bermuda, unavyoweza kuipoteza ndege na isijulikane wapi ilipoenda.

Sote tunaujua uwezo wake wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kwa kuwatambuka mabeki na chenga zake za maudhi zitakazokuacha ukitoa msonyo wa kukoshwa.

Lakini, ni kwa muda gani tulihitaji aendelee kuzikuna nafsi na kuifanya mioyo yetu itabasamu na kujivunia kuwa mashuhuda wa moja ya kipaji maridhawa juu ya ardhi ya muumba?

Hakuna yeyote aliyejaribu kumsaidia hapo kabla na inaonekana kuna dalili finyu ya Ben Arfa kupata mtu wa kumsaidia aondoke kwenye giza la hivi sasa.

Anazidi kupotea kwenye kaya ‘inayomtenga’ kwa tatizo ambalo hakutaka kuwa nalo.

Ni vigumu sana kwa mchezaji wa aina yake kupambana na hali yake halafu akashinda na wengi muanze kumsifia tena kama ilivyokuwa miaka tisa iliyopita.

Ben Arfa, kisaikolojia anaharibika. Mchezaji mwenye kipaji, na anayejijua ana uwezo wa kufanya kitu kikubwa, hutaka afanye hicho kitu kwa gharama yeyote ile, mategemeo yake ni kuonekana.

Yes, Ben Arfa anayatamani mafanikio ya Lionel Messi.

Kocha wake, Unai Emery, anakasirishwa kumuona Ben Arfa akitaka kuwa Messi.

Hili linamdidimiza Ben Arfa badala ya kumpandisha juu.

Na baada ya hapo, jinamizi la kushuka kiwango linamkumba. Benchi linampenda. Jina lake linapotea kwenye vinywa vya wadau wa soka.

UNAI EMERY BEN ARFA NEYMAR DI MARIA MBAPPE

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.