MARTIAL AIPA UNITED POINTI TATU AKITOKEA BENCHI

Martial aipa United pointi tatu akitokea benchi dhidi ya Spurs

Dimba - - Mbele - MANCHESTER, England

JOSE Mourinho mdogo mdogo anaendelea kuisogeza Manchester United kuelekea kileleni mwa Premier League, baada ya jana kuitandika Tottenham bao 1-0, katika mtanange uliopigwa Old Trafford, shukrani kwa bao la Anthony Martial.

Timu hizo zilichuana katika mtanange huo ikiwa ni siku chache tu baada ya mechi zao za Kombe la Ligi, United ikishinda 2-0 dhidi ya Swansea, huku Spurs ikikutana na kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa West Ham.

Kabla ya mechi hiyo, Spurs walikumbwa na taarifa mbaya ya kuwa watamkosa straika aliyetupia mara mbili katika ushindi wa bao 4-1 dhidi ya Liverpool, Harry Kane, kwa hofu ya kuwa ataumia zaidi kabla ya kuvaana na Real Madrid wiki hii.

Kwa upande wa United, taarifa nzuri kwao ilikuwa ni kupona kwa beki wao wa kati, Eric Bailly.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi, huku United ikitumia dakika 10 za awali za mtanange huo kwenye eneo lote la Spurs (takribani asilimia 77.65, kwa mujibu wa mtandao wa Squawka), lakini hawakuwa na ubunifu wa kutosha.

Pia Spurs nao walikuwa wakicheza soka safi, wakitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini mlinda mlango wa United, David de Gea, alikuwa imara langoni na hadi mchezo huo unamalizika, alikuwa ameokoa mashuti yote 13 aliyopigiwa Old Trafford.

Kipindi cha kwanza kilimalizika timu hizo zikaenda vyumbani nguvu sawa, huku mchezaji pekee aliyetengeneza nafasi kwa United akiwa ni Henrikh Mkhitaryan (1).

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi, United ikitandika mashuti matatu ndani ya dakika mbili (54, 55), shuti la Mkhitaryan likiokolewa, huku Romelu Lukaku na Antonio Valencia wakipiga nje.

Mchezo huo ulizidi kuwa mgumu, kwani Spurs hawakuonesha dalili ya kuchoka na wao wakihakikisha wanaondoka na ushindi, lakini, uamuzi wa Jose Mourinho kumtoa Ashley Young dakika ya 70 na kumwingiza Anthony Martial ulilipa, baada ya Mfaransa huyo kufunga bao la ushindi dakika 10 baadaye, akitumia vyema pasi ya Lukaku.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.