TSHISHIMBI AKICHAFUA TENA

Dimba - - Mbele - NA MWANDISHI WETU

KWA mara nyingine kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, ameonyesha kwamba hakuja Tanzania kuuza sura, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika mchezo wa jana dhidi ya Simba, uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Uwezo wake wa kutoa pasi za uhakika, kuzuia, na pia kusaidia mashambulizi, umeonyesha tofauti kubwa kati yake na viungo waliocheza jana.

Mara ya kwanza kwa Tshishimbi kukinukisha ilikuwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 23, mwaka huu, dhidi ya Simba, ambapo Wanajangwani hao walikubali kufungwa kwa penalti 5-4, baada ya timu hizo kutoka suluhu ya 0-0 dakika 90 za kawaida.

Katika mchezo huo, ambao ulikuwa wa kwanza wa ushindani kwa Tshishimbi kucheza tangu kusajiliwa kwake, aliwafunika viungo wa Simba, walioongozwa na James Kotei, hali iliyofanya Uwanja mzima kulitaja jina lake.

Kudhihirisha kwamba hakubahatisha, Tshishimbi mwenyewe jana alionyesha tena umahiri wake, akilimiliki dimba la katikati akimpoteza tena Kotei, na kumfanya Mghana huyo atolewe nje na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude, ambaye angalau alionyesha kuhimili mapigo ya Mkongomani huyo.

Akizungumza na DIMBA mara baada ya mechi hiyo, Tshishimbi alisema yeye ni mchezaji wa mechi kubwa, ndiyo maana mechi kama za Simba na Yanga huwa ang'ara, tofauti na zile ndogo.

"Ujue mimi ni mchezaji wa mechi kubwa kubwa kama hizi, mara nyingi huwa napata tabu kucheza mechi ndogo ndogo na ndiyo maana mnaona nang'ara katika mechi hizi.

"Ningefurahi zaidi kama kungekuwa na mechi nyingi kama hizi za Simba na Yanga ili nionyeshe uwezo wangu," alisema Tshishimbi."

Tshishimbi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.