Ilikuwa mechi ya kitajiri

Dimba - - Jumapili - NA EZEKIEL TENDWA

MECHI ya jana iliyowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga, ukisema ilikuwa ya kitajiri utakuwa sahihi kutokana na kila timu ilivyojipanga siku moja kabla ya mpambano.

Simba ambao walikuwa wameweka kambi Zanzibar, walitua Ijumaa mchana kwa ndege na kwenda Hoteli ya Serena, ambayo mara kwa mara inatumiwa na watu wenye fedha zao ambapo walipata fursa ya kula chakula cha mchana na cha usiku na matajiri wao.

Kwa upande wao Yanga, ambao walikuwa wameweka kambi mkoani Morogoro, walipotua jijini Dar es Salaam, Ijumaa, moja kwa moja walikwenda Hoteli ya Protea, ambayo ni moja ya hoteli zenye heshima kubwa hapa nchini na kisha kwenda kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.

Na walipokuwa huko, wachezaji walipata fursa ya kula chakula cha mchana na bilionea wao ambapo pamoja na mambo mengine, iliripotiwa kuwa aliwapa kila mchezaji laki tatu na kuwaahidi kwamba kama watashinda atawapa milioni 50 wagawane.

Hamasa ya Yanga ambao walikuwa wakitajwa kuwa na hali mbaya ya kiuchumi, imekuwa kubwa baada ya kigogo wao kuwamwagia fedha za kutosha huku akiwaahidi kuwamwagia Sh milioni 50 iwapo watashinda.

"Ni kweli jamaa (kigogo huyo) alikula chakula cha mchana na wachezaji ambapo kila mmoja alipewa laki tatu na akawaahidi kutoa tena milioni 50 wagawane kama watawafunga Simba," kilisema chanzo cha habari ndani ya Yanga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.