ULIZA UJIBIWE,

Dimba - - Jumapili - ULIZA UJIBIWE

SWALI: Simba na Yanga zimekutana mara ngapi na nani mwenye rekodi ya kumfunga mwenzake mara nyingi zaidi? Ameuliza msomaji mwenye simu no 0627186094.

JIBU: Pamoja na kwamba swali lako limekuwa likiulizwa mara kwa mara lakini safari hii limekuja wakati mwafaka na linapaswa kujibiwa kwa wakati.

Katika mechi mbalimbali zikiwemo za Ligi Kuu, Kombe la FAT, Headex Cup, Tusker Cup, FA, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Mtani Jembe na hata zile za kirafiki, timu hizo zimekutana mara 121 hadi hivi sasa, ambapo Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 ikiwa mwaka mmoja kabla ya Simba, inaongoza kwa kushinda mara 44 wakati Simba ikiichapa Yanga mara 43 huku zikienda sare mara 34.

Hata hivyo, kwenye mechi za Ligi Kuu peke yake, ukiacha mchezo wa jana Jumamosi, timu hizo zimekutana mara 91, Yanga ikiwa imeshinda mara 34, Simba mara 25, huku zikiwa zimetoka sare mara 32. Kwa upande wa mabao katika mechi za ligi, Yanga imefunga mabao 99 huku Simba ikiwa imetumbukiza nyavuni mabao 88. SWALI: Naitwa Ntuli Mwanginde kutoka Mbeya, nauliza eti straika Mganda Emmanuel Okwi amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara? 0758292594.

JIBU: Tangu atue nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na kuichezea Simba akitokea SC Villa ya Uganda na kwenda nje ya nchi kisha kurejea Yanga na baadaye tena Simba, Okwi hajawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara mwaka wowote zaidi ya kushinda nafasi ya pili msimu wa 2011/2012 akiwa na mabao 12 nyuma ya John Bocco wa Azam (enzi hizo) aliyekuwa kinara kwa mabao 19.

Wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara waliowahi kutokea tangu mwaka 2004 ni Abubakar Mkangwa (Mtibwa Sugar) mabao16; 2005, Isse Abshir (Simba) mabao 19; 2006 Abdallah Juma (Mtibwa Sugar) mabao 20; 2007-08 Michael Katende (Kagera) mabao 11; 2008-09 Boniface Ambani (Yanga) mabao 18, 2009-10 Mussa Mgosi (Simba) mabao 18; 2010/11 Mrisho Ngassa (Azam) mabao 18, 2011/12 John Bocco (Azam) mabao 19, 2012/13; Kipre Tchetche (Azam) mabao 17; 2013/14 Amiss Tambwe (Simba) mabao 19; 2014/15 Simon Msuva (Yanga) mabao 17, 2015/16 Amis Tambwe (Yanga) mabao 21; 2016/17 Simon Msuva (Yanga) mabao 14.

SWALI: Katika mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 20, 2013 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam; kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Haruna Chanongo/Said Ndemla dk48, Abdulhalim Humud/William Lucian ‘Gallas’ dk48, Betram Mombeki/ Zahor Pazi dk90, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Yanga SC iliwakilishwa na; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kevin Yondan, Athumani Iddi 'Chuji,' Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza/Simon Msuva dk61 na Haruna Niyonzima. SWALI: Naitwa Mohammed Issa wa Mbagala, naomba kuuliza, hivi yuko wapi mchezaji mahiri wa zamani wa soka, Msenegali El Hadhji Diouf? 0654977699.

JIBU: El Hadji Ousseynou Diouf kwa sasa amestaafu kucheza soka, lakini kwa mara ya mwisho alikuwa akiichezea klabu ya Sabah ya Malaysia. Katika kipindi chake chote alichocheza soka, Diouf alikuwa akicheza kama straika au winga wa pembeni tangu alipoanza kucheza soka katika klabu za Sochaux, Rennes na Lens, zote za Ufaransa kabla ya baadaye kuhamia katika klabu ya Liverpool ya England, huku akiwa ameonyesha kung'ara zaidi katika fainali za michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2002, nchini Korea na Japan, ambapo aliipeleka Senegal katika hatua ya robo fainali.

Pia aliwahi kuzichezea klabu za Bolton Wanderers, Sunderland na Blackburn Rovers, kabla ya kuhamia katika klabu ya Rangers ya Scotland. SWALI: Je, klabu ya Simba imenolewa na makocha wangapi tangu mwaka 1991? Na ni yupi kati ya hao aliyeipa mafanikio makubwa? Jina langu ni Ahmad Sebarua wa Nkaloi, Tamota. 0672188257.

JIBU: Kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990, Simba imewahi kufundishwa na makocha 24 na ni wazungu wawili tu raia wa Serbia ndio walioweka rekodi ambayo imeshindwa kuvunjwa na wenzao na wote.

Baba lao ni Dragan Popadic kisha anafuatiwa na Milovan Cirkovic, walioibeba Simba kwa nyakati tofauti katika michuano ya ndani na nje ya nchi.

Popadic aliibeba Simba kwa mafanikio makubwa kati ya mwaka 1994 na 1996, ambapo aliiwezesha kunyakua mataji saba; mawili ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) 1995 na 1996, ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, 1994 na 1995, ubingwa wa Ligi ya Muungano mwaka 1994 na ubingwa wa Kombe la Nyerere miaka ya 1994 na 1995.

Popadic aliichukua timu hiyo kutoka mikononi mwa kocha Abdallah Kibadeni aliyesaidiana na Mhabeshi, Etienne Eshente, waliokuwa wametoka kuifikisha Simba katika Fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, ambapo Wekundu wa Msimbazi walipoteza fainali kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abdijan. Milovan ndiye kocha wa mwisho kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-12, kuanzia hapo haijawahi kushika hata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kwa ujumla makocha wa Simba walikuwa ni (Abdallah Kibadeni 1990-1994), Dragan Popadic (19941996), Mansour Magram/Kibadeni (1997), Mohamed Kajole (1998), David Mwamaja (1999), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (1999-2000), Abdallah ‘King’ Kibadeni (2000), Syllersaid Mziray (2000), Mkenya James Siang’a (20012004), Mzambia Patrick Phiri (2005), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Talib Hilal raia wa Oman (2007), Milovan Cirkovic (2009), Phiri (2010), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Mganda Moses Basena (2012), Cirkovic (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), Kibadeni (2013), Zdravco Logarusic (2013-2014), Phiri (2014), Goran Kopunovic (2015), Dylan Kerr (2015-2016), Jackson Mayanja na Joseph Omog. SWALI: Kati ya klabu ya Real Madrid na Barcelona ni timu ipi yenye rekodi ya kutwaa mataji mengi kwa ujumla? Renald Amos wa Moshi Bar. 0788815581.

JIBU: Ukiacha mataji madogo madogo, timu zote hivi sasa zinalingana kwa kuwa na idadi sawa ya mataji 82, ambapo Real Madrid ina mataji 33 ya La Liga, Copa Del Rey (19) Super Copa (10), Ligi ya Mabingwa Ulaya (12), Kombe la Washindi Ulaya (2), Uefa Super Cup (4) na Klabu Bingwa ya Dunia mataji mawili. Barcelona inayo mataji 24 ya Ligi Kuu ya Hispania, Copa Del Rey (29), Super Copa (12), Ligi ya Mabingwa Ulaya (5), Kombe la Washindi Ulaya (4), Super Cup (5) na Klabu Bingwa ya Dunia (FIFA) mataji matatu. SWALI: Yuko wapi mchezaji wa zamani wa TP Mazembe, Tresor Mputu Mabi? Mimi ni Dominic Dibwe wa Dar es Salaam. 0678834051.

JIBU: Mara ya mwisho alikuwa akiichezea klabu ya Kabuscorp ya Angola, lakini akavunja nayo mkataba mwezi Mei mwaka jana na sasa amerejea katika klabu yake ya TP Mazembe kama 'mhenga.' SWALI: Naomba unitajie kikosi cha Manchester United cha mwaka 1998. Naitwa Salmin Mwakisumbi wa Ilala, jijini Dar es Salaam 0784956057.

JIBU: Kikosi cha Manchester United mwaka 1998 kilikuwa: Makipa; Peter Schmeichel, Raimond van der Gouw na Nick Culkin. Mabeki; Gary Neville, Denis Irwin, David May, Ronny Johnsen, Jaap Stam, Phil Neville, John Curtis, Ronnie Wallwork, Danny Higginbotham, Michael Clegg, Wes Brown na Henning Berg.

Viungo: David Beckham, Nicky Butt, Ryan Giggs, Jordi Cruyff, Jesper Blomqvist, Roy Keane, Paul Scholes, Mark Wilson, Jonathan Greening, Philip Mulryne na washambuliaji walikuwa Andy Cole, Teddy Sheringham, Dwight Yorke, Ole Gunnar Solskjaer, Erik Nevland na Alex Notman. SWALI: Mhariri naomba unikumbushe kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kilichocheza fainali za michuano ya AFCON mwaka 1980. Naitwa Elisha Mughanga wa Singida. 0759602733.

JIBU: Baadhi ya wachezaji walioipeleka Tanzania kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika jijini Lagos, Nigeria ni Juma Pondamali, Leopard Tasso Mukebezi, Mohammed Kajole/Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally. SWALI: Mbona kila siku nikiuliza maswali yangu huwa sijibiwi? Hivi timu ya Simba iliyofika fainali za Kombe la CAF ilikuwa ni mwaka gani na ilikuwa chini ya uongozi gani na kocha yupi? Mshamu Tungupu wa Morogoro, Ifakara Town. 0783176411.

JIBU: Hatuna kawaida ya kutojibu maswali ila ukiona swali lako halijibiwi ujue zamu yako haijafika tu katika utaratibu wa kawaida. Kuhusu Simba iliyofika fainali ya Kombe la CAF, ilikuwa ni mwaka 1993 chini ya uongozi wa Amir Ally Bamchawi ambaye alikuwa ni Mwenyekiti, Makamu wake Saleh Ghulum, Katibu Mkuu alikuwa ni Privatus Mtema Nyenje, Katibu Msaidizi, Khalfani Matumla na Mweka Hazina alikuwa ni Ayoub Semvua.

Emmanuel Malima

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.