MBONDE:

Kombe la Dunia kwa kizazi chetu tumechelewa

Dimba - - Jumapili - NA SAADA SALIM

U SIJAJI kitabu kwa ukurasa wa mbele. Hivyo ndivyo unavyoweza kuwazungumzia mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba, mara baada ya kamati ya usajili kuamua kumpa mkataba wa miaka miwili Salum Mbonde, aliyekuwa Mtibwa Sugar.

Usajili wa nyota huyo ulizua hofu kubwa kwa baadhi ya mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba, baada ya kudiriki kusema alikuwa ni mchezaji wa kawaida sana.

Lakini kutokana na Watanzania kuzoea kumjadili mtu kwa mwonekano wa nje, hivyo ndivyo beki huyo alivyowaonyesha jambo mashabiki ambao walikuwa hawamwamini na wengine waliokuwa wakimponda, baada ya kuwapo kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Joseph Omog.

Kutokana na kiwango kizuri anachokionyesha Mbonde na kuvutiwa na kila kocha anayepewa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Tanzania `Taifa Stars` kumjumuisha katika kikosi chake, hali hiyo imepelekea kuwa tegemeo katika safu ya ulinzi ya klabu hiyo.

DIMBA Jumapili lilifanya mahojiano na Mbonde na kuzungumza mambo mbalimbali, ikiwamo maisha yake ya ndani na nje ya soka kwa sasa Simba.

DIMBA: Kuna tofauti gani ya ligi msimu huu na uliopita?

MBONDE: Msimu huu ligi ina ushindani mkubwa, kwani timu nyingi zimejiandaa vya kutosha na timu mbalimbali zimepata wadhamini, hivyo ushindani unazidi kuongezeka.

DIMBA: Kuna tofauti gani maisha ya Mtibwa Sugar na sasa Simba?

MBONDE: Maisha ya Mtibwa muda wote ni kambini, tofauti na Simba, mnafanya mazoezi mnarudi majumbani, hivyo ni nzuri, inanipa muda wa kufanya mambo mengine ya kimaisha, lakini pia inahitaji akili ya mchezaji mwenyewe kulinda afya yake ya mwili.

DIMBA: Unakitazamaje kikosi cha Simba kwa msimu huu? Unadhani usajili waliofanya utakidhi matakwa ya timu?

MBONDE: Bila shaka usajili uliofanywa na Simba ni mzuri na wengi wazoefu wa michuano ya kimataifa na ligi, kwa hali hiyo, Mungu akipenda ndiyo tutakuwa mabingwa kutokana na kujipanga kwetu vyema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

DIMBA: Ni beki gani kati ya Method Mwanjali na Jjuuko Murshid ukipangwa naye unacheza ukiwa huru zaidi?

MBONDE: Wote kwangu sawa, maana tunaelewana vizuri na hii inatokana na siyo siku zote nitacheza na mmoja tu.

DIMBA: Mechi gani unayoikumbuka hutakuja kuisahau na kwanini?

MBONDE: Mechi ya Algeria dhidi ya sisi Tanzania, ambapo tukiwa ugenini tulifungwa 7-0, siwezi kuisahau, japo sikucheza nilianzia benchi, ila ndiyo mechi ambayo sitaisahau, kwani tokea nianze kucheza mpira sijawahi kuwa katika timu iliyofungwa mabao mengi kiasi hicho.

DIMBA: Mtibwa Sugar ni miongoni mwa timu zinazobomolewa kila msimu kwa kuchukuliwa wachezaji wake, lakini msimu unaofuata wako vizuri, je, unadhani nini mafanikio ya waajiri wako wa zamani?

MBONDE: Ni kweli, lakini kinachosaidia Mtibwa Sugar ni hazina kubwa ya vijana waliokuwa nao, ambao pia wamekuwa wakisajili watu sahihi kila msimu kuziba nafasi ya walioondoka.

DIMBA: Je, unaizungumziaje mechi uliyocheza iliyopita dhidi ya Mtibwa, ambayo ilimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1?

MBONDE: Mechi ni ngumu na sitakuja kuisahau, kwani imeniharibia malengo yangu ya kucheza dhidi ya Yanga. Hii ni baada ya mimi kuumia, hivyo kushindwa kuwepo kwenye kikosi cha kucheza dhidi ya Yanga.

DIMBA: Ulipoambiwa utakosa mechi nne ulijisikiaje na vipi kuhusu matibabu yako?

MBONDE: Niliumia sana, kwani natamani ningekuwapo katika mechi kubwa hii dhidi ya Yanga, lakini ni mipango ya Mungu. Suala la matibabu niko chini ya uangalizi wa daktari ambapo nitakuwa kwenye uangalizi kwa siku tatu.

DIMBA: Ni mshambuliaji gani kwako anayekusumbua kwa wapinzani?

MBONDE: Sijawahi kusumbuliwa na mshambuliaji yeyote hapa Tanzania.

DIMBA: Kabla hujasaini Simba, kulikuwa na taarifa ya kutakiwa nje ya nchi, ilikuwa nchi gani na ilikuwaje ukasaini Simba?

MBONDE: Kweli lilikuwepo, baadaye likayeyuka, sijui ilikuwaje, ila meneja wangu anafahamu hilo.

DIMBA: Mbali na beki, nafasi gani unacheza?

MBONDE: Kiungo mkabaji ndiyo namba yangu ninayoimudu, zamani nilikuwa nacheza hiyo, ingawa baadaye makocha wakanibadilisha, hasa Kocha Mbwana Makata, wakati nipo JKT Oljoro.

DIMBA: Je, nini kifanyike Tanzania ishiriki Kombe la Dunia?

MBONDE: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuwekeza katika soka la vijana kwa kizazi kijacho, kwa kizazi chetu tumechelewa.

DIMBA: Unaishi wapi, vipi umeoa na una watoto wangapi, muda wako wa mapumziko unautumiaje?

MBONDE: Maisha yangu mara nyingi ni Morogoro, lakini kwa sasa Simba wamenipa nyumba Sinza. Sijaoa, lakini nina mtoto mmoja anaitwa Sally, jina la dada yangu anayeishi Marekani. Vilevile muda wangu mwingi natumia kukaa na familia kutokana na muda mwingi natumia katika kazi.

DIMBA: Mbali na soka, ambalo linakuingizia kipato, kitu gani kingine?

MBONDE: Nimechangamsha ubongo wangu, mbali na soka ni mjasiriamali, kuna mambo mengi nafanya kuongeza kipato mkoani Morogoro, kipindi ninapokuwa Dar es Salaam anasimamia mama yangu na familia.

Mpira una matokeo ya aina tatu, kushinda, kutoka sare na kufungwa, mimi sijaja kufanya maajabu yoyote bila kumtegemea Mwenyezi Mungu. Muhimu ni sisi kujipanga kwa kufanya maandalizi ya kisaikolojia kwa wachezaji wetu na wao kuzingatia kile ambacho tutawaelekeza kama benchi la ufundi. Hili la ukame wa mataji naamini tukishirikiana vyema mbona freshi litakwisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.