Simba, Yanga hakupatikana mbabe 1995

Dimba - - Jumapili - NA HENRY PAUL

MIONGONI mwa matukio yaliyowahi kufanywa na wachezaji wa enzi hizo ambayo yanakumbukwa na wapenzi wa soka nchini, moja ni lile la wachezaji chipukizi wa Yanga, maarufu kama ‘Yosso’, kuwadhibiti vilivyo wachezaji wakongwe wa Simba na hatimaye kutoka sare ya 0-0.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu),uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), siku ya Jumamosi Machi 18, 1995. Katika mechi hiyo, timu ya Yanga iliwachezesha wachezaji wengi Yosso, baada ya wakongwe wengi wa timu hiyo msimu wa nyuma yake 1993/1994 kufukuzwa na kubakiza wanane tu.

Kwa upande wa timu ya Simba, yenyewe iliwachezesha wachezaji wakongwe ambao wengi wao walikuwa wakichezea timu ya Taifa Stars wakati huo na walikuwa na uzoefu mkubwa na mechi hizo za watani wa jadi.

Mchezo ulianza kwa kasi, huku Yanga wakilishambulia lango la Simba toka dakika ya kwanza tu ya mchezo. Katika dakika ya pili, mshambuliaji Peter Louis alipiga shuti kali lililodakwa na kipa wa Simba, Mohamed Mwameja.

Dakika mbili baadaye, Simba nao walifanya shambulio moja la nguvu langoni mwa timu ya Yanga, lakini shuti la mshambuliaji Nteze John liliokolewa na kipa wa Yanga, Said Kalokola.

Katika dakika ya 15, mshambuliaji wa Simba, Said Mwamba ‘Kizota’, alipata mpira akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lake lilitoka nje kabisa ya lango la Yanga.

Baada ya Mwamba kukosa kufunga, mshambuliaji wa Yanga, Nonda Shabani ‘Papii’, aliwapita mabeki wawili wa Simba, George Masatu na Mustapha Hoza, lakini shuti lake alilopiga lilidakwa na kipa wa Simba, Mohamed Mwameja.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika timu hizo zilikwenda mapumziko matokeo yakiwa ni sare ya bila kufungana.

Kipindi cha pili kilipoanza, Yanga waliingia kwa kasi na kuanza kupeleka mashambulizi makali ya mfululizo langoni mwa timu ya Simba, huku mabeki wao wakionekana kuwa na kazi moja tu ya kudhibiti mashambulizi hayo. Katikati ya kipindi cha pili, Simba walichachamaa na kuanza kufanya mashambulizi ya mfululizo langoni mwa timu ya Yanga, lakini washambuliaji wao, Madaraka Seleiman na Nteze John, ambao walikuwa wakipishana upande wa winga ya kushoto, walidhibitiwa vilivyo na ‘kinda’ beki Anwar Awadh.

Awadh pamoja na kuwa chipukizi na umbo dogo, lakini aliwadhibiti nyota hao na kushindwa kupachika mabao. Hivyo hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika, timu hizo zilitoka uwanjani matokeo yakiwa ni sare ya 0-0.

Kikosi cha Yanga kiliwakilishwa na Said Kalokola, Silvatus Ibrahim ‘Polisi’, Anwar Awadh, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Ruben Mgaza, Salvatory Edward, David Mjanja, Peter Louis, Ally Yusuf ‘Tigana’, Nonda Shabani ‘Papii’, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na Maalim Saleh ‘Romario’.

Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na Mohamed Mwameja, Deo Mkuki, Alfonce Modest, Mustapha Hoza, George Masatu, Hussein Marsha, George Lucas ‘Gaza’/Dua Said, Juma Amir, Madaraka Seleiman, Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu)/Mwanamtwa Kiwhelo na Nteze John.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.