NAMCHUKIA MUME WANGU (14)

Dimba - - Jumapili - MTUNZI: ZUBAGY AKILIMIA SIMU: 0712313192 Je, nini kitaendelea? Tukutane wiki ijayo. Usikose kitabu changu cha NAMCHUKIA MKE WANGU, na KAFARA LA KISHETANI. Vinauzwa kila kimoja Tsh 4000/= tu; kwa wauzaji wa magazeti nchi nzima. 0712313191 Zubagy Akilimia.

ILIPOISHIA WIKI ILIYIOPITA... “Wee fungua...,” alisema, nikafungua mlango nusu .... vuuup! Ghafla, macho yangu yalikutana na sura za wanaume watatu na wanawake wawili. “Ndiye huyu?” Mwanaume aliuliza akiniangalia kwa makini. Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi isiyo kawaida, tayari mshale wa hatari ulipiga ubongoni mwangu na kuona nimekamatwa na Jeshi la Polisi. Nilipowaangalia wale watu hawakuonekana raia wa kawaida, sura zao zilikuwa za kijeuri jeuri. Kupitia jicho langu la kengeza la kipelelezi, mwanamke mmoja alikuwa ameficha bastola, woga ukaanza kuniingia nikihisi baridi kali. Sasa endelea na simulizi hii...

Nilipoiona bastola, moja kwa moja neno ‘amani hakuna’ likaibuka ubongoni mwangu, nilihitaji akili ya kujiongeza kama mwanajeshi niliyepitia mafunzo ya kijeshi. Nilikumbuka Kamanda wangu alinifundisha kuua bila kutumia silaha, hiki ndicho kipindi nilihitaji kufanya niliyoelekezwa jeshini. Sikutaka kamwe kuruhusu kutiwa mikononi mwa polisi. “Ndiye au siye?” “Siye, lakini kuna kitu nimehisi...,” mwanamke mmoja alijibu akinitazama kwa makini. “Umehisi kitu gani?” “Anatufaa kwa kazi yetu...” “Ndiyo...,” baada ya kauli ile, walionyeshana ishara ambazo nilianza kuzielewa kwa mbali.

“Samahani, wewe ni nani?” Sauti ya kiume iliniuliza.

“Mimi ni mfanyakazi, nimeajiriwa...” “Unafanya kazi gani?” “Mtumishi wa serikali .... ,” nilijibu, tayari nilianza kuhisi huenda wale watu ni majambazi.

“Watumishi serikalini wapo wengi, hata sisi ni watumishi wa serikali, sema tunatofautiana...”

“Okay, mimi ni mpelelezi...,” nilidanganya.

“Tuambie ukweli, sisi kuna kazi tunataka kukupa...” “Kazi gani?” “Kazi nzuri ya kukupa mabilioni ya pesa!”

“Sawa, naomba niwape namba zangu...mnipe zenu nitapigia... tutaongea...” niliwaambia hivyo.

“Sawa...,” yule mwanamume alijibu kisha akaniandikia namba zake za simu, nikampatia zangu, akanibip. Nikaziona namba zake na kuzisevu katika simu yangu. Lakini kabla ya kuondoka, nikawauliza.

“Mmevutiwa na nini kwangu, mpaka mnataka tufanye kazi wote?”

“Tumevutiwa na mwili wako, unaonekana umekomaa kimazoezi, vidole vyako zimekomaa sana, mikono yako ya mazoezi, upo vizuri dada...”

“Ahsante, kwa herini tutawasiliana!” Niliwajibu, nikafunga mlango kwa funguo kisha nikaondoka eneo hilo nikiwa siamini kama nimesalimika.

“Wale watu kuna mtu wanamtafuta, sijui ni majambazi au askari wenzangu?” Niliwaza nikiingia ndani ya gari na kuondoka na funguo ya hotelini. Sikutaka watu washtuke mapema kabla sijaenda mbali, nilihitaji kuendelea na zoezi langu la mauaji. ***** Nikiwa makao makuu ya jeshi Dar es Salaam, niliweza kuonana na shangazi aliyeniambia nilitakiwa kwenda masomoni China kwa ajili ya kuongeza ujuzi, alinipatia barua hiyo iliyoniacha kinywa wazi. Ni jambo ambalo lilininyong’onyesha sana.

“Natakiwa lini niende masomoni?” Niliuliza kwa sauti ndogo.

“Wiki mbili zijazo, sasa hivi tunataka kushughulikia vibali vyako na pesa za matumizi ukiwa China...”

“Sawa, usijali mkuu!” Nilimuita Anti hivyo, akacheka sana.Nilirejea nyumbani nikiwa mchovu sana, sikutaka mazungumzo na mtu, nilienda moja kwa moja chumbani kwangu kulala, saa tatu usiku niliamshwa kwa ajili ya kula chakula.

Nilikula kivivuvivu nikiwa nahisi usingizi mzito, hata hivyo niliona simu yangu ikiita na nilipoiangalia mpigaji ni Saimon Mota, mwanamume aliyenitenda na kunisababishia nisiweze kuitwa mama, kwa kunitoa mimba bila ridhaa yangu na kuniletea tatizo la kuharibika kizazi kilichowafanya madaktari wakitoe kizazi.

Nilisikia moyo ukiugua, hasira zilinikaba na kuniumiza moyoni.

“Habari yako!” Nilisema kwa sauti ndogo ya kike iliyotulia, hakujua kama najua namba yake.

“Salama, habari za siku nyingi mke wangu...” “Mkeo! Wewe nani?” “Saimon Mota, mumeo!” “Samahani, sina mume... Saimon naomba usiniite mkeo, sitaki kusikia habari hizo...”

“Samahani, ila nimesahau kusema aliyekuwa mke wangu, barafu wa moyo wangu...”

“Sitaki uniite mkeo, unanikera...”

“Ahaaa, sasa mke wangu naomba tuonane...nina mazungumzo nawe...” aliniambia yule mwanamume. “Kuhusu nini?” “Ndoa yetu, hatuwezi kuachana mapema kiasi hiki, naomba unipe muda niweze kuzungumza nawe...,” alizidi kunibembeleza. “Unataka tukutane wapi?” “Tukutane Sinza...” “Lini?” “Leo!” “Saa ngapi?” “Muda huu...” “Hapana, kesho asubuhi, nitafute...,” nilimjibu na kukata simu.

“Sijui ananitaka nini huyu mshenzi, anachokitafuta atakipata...,” niliongea moyoni nikirejea kitandani. Usingizi ulinipitia muda mfupi tu nilipopanda kitandani. Alfajiri, niliona meseji saba, nilipoanza kuzifungua, zilikuwa zimetumwa na watu tofautitofauti, meseji mbili zilikuwa za Saimon Mota, alinijulia hali, na nyingine akinikumbusha tukutane Sinza asubuhi hiyo.

Nilimwambia nitakwenda kukutana naye, ila suala la mapenzi nilimuonya alifute kichwani mwake, aliridhia na kuniambia hahitaji mapenzi, alihitaji tuzungumzie tofauti zetu ndani ya ndoa.

“Rose, siku hizi mwanangu huna muda wa kutulia, vipi uko sawa?”

“Nipo sawa, kazi mama... naenda kushughulikia viza ya kwenda China, natakiwa kwenda kusomea kozi fupi ya kijeshi...”

“Haya, pole...nakuonea huruma,” mama aliniambia, nikamweleza kazi za jeshi ni ngumu, ingawa napaswa kupambana. Ukweli ni kwamba sikuwa na kazi nyingi kihivyo, nilimdanganya mama tu, hakujua nalipiza kisasi kwa wabaya wangu na wote wanaotaka kuniharibia maisha yangu.

Kabla ya kutoka, nilitoa pochi zangu mbili na kuziweka kitandani, nilihitaji kuchagua pochi nitakayotoka nayo kwa siku hiyo. Niliifuta mikoba yote na kuchukua bastola ya baba ambayo nilichukia kwa siri bila kujua, nikaiweka kwenye pochi nyeusi. Baada ya kumaliza usafi wa mwili na kujipodoa, nilijipulizia manukato mazuri kisha nikavaa nguo za kisasa zenye mvuto wa kimahaba, nilidhamiria kulipiza kisasi kwa Saimon Mota, sikutaka kuendelea kubaki na jeraha moyoni mwangu.

“Umependeza, utafikiri sio mwanajeshi!” Mama aliniambia akinicheka nilivyotokelezea.

“Ahsante mama, natoka kidogo...” “Sawa, umemuaga baba yako?” “Hapana...” “Muage basi baba...,” nilienda na kusimama nje ya mlango wa chumbani kwa baba, nikamsalimia na kumweleza kuwa natoka kidogo kikazi.

“Sawa mwanangu, mi’napumzike macho yananiuma sana...” “Umefanyaje?” “Uzee tu, wala sijafanya kitu...” “Pole dady! Nitakupeleka hospitali kesho.” Nilimwambia, akaitikia nikaondoka zangu na safari ya Sinza ikaanza. ***** Nje ya jengo zuri nilipoelekezwa na Saimon Mota, nilikutana na dada mmoja aliyenipokea na kunikaribisha ndani.

“Wewe ni mgeni wa Saimon Mota?” “Ndiyo...yupo wapi?” “Yupo ndani, chumba namba 7...”

“Ahaa! Kwani wewe ni nani?” Nilimudu kumuuliza yule msichana mrembo.

“Mimi ni mhudumu wa hoteli hii...,” aliniambia akitabasamu.

“Ohoo, ahsante..naitwa Nancy...,” nilidanganya jina, sikutaka watu wanijue kiundani.

“Umenidanganya, unaitwa Rose...”

“Yap! Umenijuaje? Au Saimon Mota amekuambia...”

“Ndiyo...na kaniambia wewe mkewe!”

“Mmh! Haya! Sina tabia ya kujitambulisha jina langu halisi...”

“Ni kweli, sio vizuri kila mtu kukujua...,” tuliingia ndani ya hoteli hii na kwenda moja kwa moja chumba namba saba, msichana huyu alifungua mlango nikaingia nikiwa na hasira kali, hakuna mwanaume niliyemchukia duniani kama Saimon Mota, ukatili alionifanyia ulitosha kunijaza chuki kwa wanaume wote. Sikutaka kumwamini mwanaume, niliona wote sawa!

“Helooo, mambo sweetiee!” Saimon aliinuka na tabasamu pana, akataka kunikumbatia, nikazuia kwa mikono yangu.

“Vipi, nilikuambia hakuna kukumbatiana hapa...”

“Unasemaje?” Aliniuliza kwa hasira.

“Nimekuja kuzungumza nawe tu, hapa utakula maneno...na sio mapenzi...”

“Sikiliza Rose, siwezi kuzungumza chochote na muuaji, wewe ndiye umemuua rafiki yangu...,” kauli ile ilinishtua kidogo, nilijisikia mwili ukiingiwa na ubaridi wa woga. “Mimi?” “Ndiyo, najua kila kitu Rose! Wewe sio mwanamke mwema...,” baada ya kauli ile, nikasogeza mkono wangu kufungua zipu ili nitoe bastola yangu, nikashtuka, hapakuwa na bastola. Nilijichanganya na kuchukua mkoba ambao haukuwa na bastola na kuacha wenye bastola nyumbani. Hofu ikaongezeka zaidi na kushindwa cha kufanya.

“Sikiliza Saimon, kama ndiyo mazungumzo umeniitia hapa, niache niondoke...”

“Huwezi kuondoka salama katika chumba hiki...,” alisema akijichekelesha tena kwa kejeli.

Nikiwa mwenye mawazo mengi, nikijilaumu kuacha bastola yangu nyumbani, nilimsikia akiita, “Kambona, njooni mfanye kazi niliyowatuma...cash yenu hii...,” sauti hiyo ya Saimon ilinitisha, nilishangaa wanaume sita wakitoka mvunguni mwa kitanda na kukabidhiwa pesa za kitanzania kiasi cha milioni tano. Walikuwa vidume hasa, wote walionekana watu wa mazoezi makali, vifua vyao vilijaa nyama ngumu zenye misuli mizito kama mizizi ya Mwarobaini.

“Saimon, unataka kunifanya nini?” Nilimuuliza nikijaribu kuwaangalia kama ningeweza kupambana nao kwa ngumi.

“Hapana Saimon, ndicho ulichopanga nibakwe?”

“Kabisa, lazima ubakwe upende usipende...”

“Sitaki, siwezi kukubali ukatili huu,” niliongea niking’ata meno kwa hasira, nilimwangalia Saimon, hasira zikanijaa mwili mzima, nilitamani kumng’atang’ata na kumtema.

“Ukubali ukatae lazima watu wacheze na mwili wako,” alisema, nikasimama kikakamavu, mkono wa kushoto nikakunja ngumi kwa ajili ya kupambana, sikutaka nibakwe kizembe, kwani kilikuwa kitendo cha ukatili sana kwa mwanamke.

Alinifuata yule baunsa wao, mwenye mwili mkubwa, ingawa sikutaka kumpa nafasi ya kunishika, nikamtwanga ngumi moja akaenda chini.

“Saimon, naomba unisamehe...” nilimwambia kwa sauti ya upole, niliamini nisingeweza vita hii, wamejipanga na wana bastola mifukoni.

“Siwezi, lazima uumie...hii ni historia nzuri ya maisha yako...”

“Lakini kwanini unanifanyia yote haya, naomba uniambie nilikufanyia kosa gani katika maisha yangu ambalo lilikufanya unipeleke hospitali ukiniambia naenda kupimwa ujauzito kumbe ulikuwa na nia ya kunitoa mimba. Mbaya zaidi utoaji mimba ukafanyika vibaya na kuathiri kizazi changu, hali iliyosababisha nitolewe kizazi na sasa siwezi kuzaa tena na kuitwa mama fulani, hiki kilema umeniletea wewe Saimon... ajabu, leo umeniita ili tuzungumze kumbe umeandaa wanaume wanifanyie ukatili, unapenda uone nikibakwa mbele yako! Saimon... usinifanyie ukatili huo...tafadhali nakuomba...” niliongea kwa hisia kali, nilijaribu kumpigia magoti.

“Lazima ufanyiwe, siwezi kukuonea huruma..., ” baada ya kauli ile, nilijikuta nikitetemeka mwili ukiishiwa nguvu, hakuna kitu nilichokiogopa maishani mwangu kama kubakwa, nilifahamu ni maumivu makali sana na pengine ningepata maambukizi ya virusi au magonjwa kama kaswende nk. Machozi yalianza kunitoka mwanamke! Nilijuta kwanini nilikubali kuja kuonana na Saimon bila bastola ya baba.

“Kambona, mkamateni haraka, muda unakwenda...,” walinivamia wanaume wanne, kila mmoja alishika sehemu yake. Mwingine alishika mkono wa kushoto, wa pili akashika mkono wa kuume, wa tatu alinishika mguu mmoja na wa nne akashika mguu wa pili.

Kwa macho yangu mawili, nilimshuhudia mwanamume akijipanga kunisulubu kimapenzi bila hiyari yangu, nilizidi kuangua kilio nikitetemeka, wakati huo Saimon Mota akicheka! Nililalamika ingawa sauti yangu ilikuwa kama muziki mzuri wa kuliwaza, hakuna aliyejali kiasi gani niliumia, nilianza kutendewa vitendo vya ukatili na mwanamume zaidi ya mmoja.

“Saimon, nashukuru! Nashukuru Saimon, wewe ni mwanamume katili sana...” nilisema nikiangua kilio, wao wakicheka kweli kweli. Walipoona napiga kelele, walinifunga midomo, nikawa nahangaika nikiugulia maumivu makali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.