Hawa wanadaiwa chenji Simba, Yanga

Dimba - - Front Page - EZEKIEL TENDWA NA CLARA ALPHONCE

WAKATI baadhi ya wadau wa soka wakiamini kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, kaenda kwao Zambia kwa ajili ya msiba wa mpwa wake, kumbe amebadili gia na kuunganisha hadi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwenda kusaka kiungo mwingine fundi ambaye atakuja kukinukisha na Kabamba Tshishimbi pale Jangwani.

Yanga inahaha kusaka kiungo mwingine mwenye ufundi ambaye atakuwa na uwezo wa kucheza nafasi za kati na pembeni, hasa upande wa kushoto ambako Lwandamina anasema kama atampata mtu sahihi, basi Yanga itatisha.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa Yanga ni kwamba Tshishimbi aliwakabidhi jina la kiungo anayemwamini ataweza kuongeza nguvu katika maeneo hayo ili Yanga iweze kutisha katika mechi za ligi na zile za Kimataifa.

DIMBA limejiridhisha kwamba viongozi Yanga wanalo jina la kiungo huyo ambaye Lwandamina amemfuata na wanasubiri majibu ya mazungumzo kati yake na kocha huyo na kama yatafanikiwa aweze kusajiliwa katika usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.

Mtu mmoja wa karibu na Tshishimbi amemkariri kiungo huyo akisema ni kweli wamefanya naye mazungumzo na kukubaliana kwamba aje kujiunga na Yanga wakati wowote katika kipindi cha usajili cha dirisha dogo.

Imeelezwa kuwa kiungo huyo ni Mcongoman na rafiki mkubwa wa Tshishimbi, ingawa walikuwa hawachezi timu moja na kwamba akija watakinukisha vilivyo.

Ingawa hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuanika jina la beki huyo, lakini gazeti hili limebaini kuwa ni mmoja kati ya marafiki wa karibu wa Tshishimbi aliyekuwa akicheza soka nchini Swaziland, lakini kwa sasa amerejea Congo-DR.

Mmoja wa mabosi wa Yanga alisema: "Tuliamua kumuuliza Tshishimbi kama anaweza kumjua mchezaji yeyote anayeweza kutufanyia kazi katika safu yetu ya kiungo na atamtaja huyo."

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa, aliliambia DIMBA kwamba Lwandamina anakwenda kwao Zambia kutokana na msiba huo wa mpwa wake, lakini taarifa nyingine zinadai kuwa, ameunganisha Congo-DR, kutafuta bonge la kiungo baada ya kuvutiwa na kile anachokifanya Tshishimbi.

Taarifa ambazo zimenaswa na DIMBA Jumatano, zinadai kuwa Lwandamina amewaambia viongozi wa Yanga kwamba viungo wa hapa nchini, hawana uwezo anaoutaka yeye ndiyo maana akaamua kwenda Congo kumaliza kazi.

"Ni kweli kwamba kocha aliomba ruhusa ya kwenda Zambia, kwani wakati ligi inaendelea alipata msiba wa mpwa wake akashindwa kuiacha timu, lakini baada ya ligi kusimama ndio akapata ruhusa hiyo lakini ukweli ni kwamba atapitia Congo, kutafuta mchezaji anayecheza nafasi ya kiungo.

"Licha ya kwamba wapo baadhi ya wachezaji ambao wameshatajwa kwamba watasajiliwa, lakini kocha alisema viungo wa hapa nchini hawachezi kama anavyotaka yeye, ndiyo maana ameamua kukimbilia Congo na hii ni kutokana na uwezo alioonyesha Tashishimbi," alisema mtu mmoja wa karibu na Lwandamina.

Mbali na kiungo huyo, pia taarifa nyingine zinadai Lwandamina anafanya kila linalowezekana kunasa saini ya mmoja wa mastraika wa Zesco ya Zambia ili kuanza kuziba mapengo ya wachezaji ambao wamekuwa majeruhi mara kwa mara.

"Kama unavyoona wachezaji wetu muhimu akiwamo Donald Ngoma pamoja na Amis Tambwe, wamekuwa majeruhi wa muda mrefu, hivyo kocha anaweza akapendekeza mmoja wa mastraika mahiri wa timu ya Zesco ya Zambia, lakini pia winga ambaye ataziba pengo la Simon Msuva," alisema.

Baada ya DIMBA Jumatano kupata taarifa hizo za Lwandamina kuunganisha safari yake kwenda Congo, lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa ambaye alisema anachojua ni kwamba kocha wao yupo Zambia na kama amekwenda kwingine kutafuta wachezaji bado ni jukumu lake.

"Ninachojua ni kwamba aliomba ruhusa ya kwenda kwao Zambia, kwa habari ya ule msiba na tunatarajia atarudi Jumatatu wiki ijayo, lakini kama amekwenda huko unakosema (Congo) kuangalia wachezaji wengine, bado hilo ni jukumu lake mana yeye ndiye anatuletea majina ya wale anaowaona watamfaa na sisi tunatekeleza tu," alisema.

Akizungumzia suala zima la usajili kwa timu yake, alisema kutokana na kukabiliwa na michuano ya Kimataifa mwakani, lazima wataongeza silaha hatari ili wasiingie katika michuano hiyo kama washiriki tu bali wapambanaji.

"Tunatarajia kufanya usajili mkubwa kujiandaa na michuano ya kimataifa, kama unavyojua sisi tutaiwakilisha nchi Klabu Bingwa Afrika mwakani, hivyo lazima tujiandae vizuri ili tusiishie hatua za mwanzo na badala yake ikiwezekana tufike kabisa fainali,” alisema. Licha ya kwamba Mkwassa aligoma kusema wanataka kusajili idara gani, lakini DIMBA Jumatano linafahamu kuwa wanataka kuongeza nguvu idara ya ulinzi na huenda Vincent Bossou akarejea, kwani mwenyewe amesema anatamani kurejea kwenye kibarua chake.

Idara nyingine ni kiungo ambaye ataziba vizuri pengo la Haruna Niyonzima ili ashirikiane na Kabamba Tshishimbi pamoja na Thaban Kamusoko, kwamba mmoja atakapopata matatizo yoyote aidha ya kadi au majeraha, wasiwe na pengo kubwa.

Pia wanataka kuongeza winga mmoja baada ya kuona hakuna aliyeweza kuziba pengo la Simon Msuva, lakini pia straika mmoja kutokana na akina Donald Ngoma na mwenzake Amis Tambwe kukumbwa na majeraha ya muda mrefu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.