DHAMIRA YA SINGIDA UNITED IZISUTE SIMBA, YANGA

Dimba - - Jumatano -

MIONGONI mwa klabu za soka zinazoshiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Singida United inaweza kuwa ya kwanza kupigiwa mfano kutokana na maendeleo yanayoonyesha mikakati ya dhati ya kujiimarisha ndani na nje ya uwanja.

Ukiiangalia timu hiyo katika msimamo wa ligi unaweza kuanza kupata majibu ya mikakati mizuri waliyoanza nayo, kwani hadi sasa ligi ikiwa katika mzunguko wa tisa, ipo nafasi ya 6 huku ikifungana pointi na timu ya Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya tano, ambapo zote zimeshakusanya pointi 14.

Hayo ni mafanikio ya uwanjani ambapo kati ya timu tatu zilizopanda daraja msimu huu, Lipuli FC, Njombe Mji na Singida United, timu hiyo ya Singida imeshazitangulia timu hizo mbili.

Kana kwamba haitoshi, kila mpenzi wa soka aliyebahatika kushuhudia mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo dhidi ya Yanga iliyopigwa wikiendi iliyopita, watajiridhisha juu ya uwezo wa kikosi hicho kinachonolewa na kocha mkongwe Hans van der Pluijm aliyewahi pia kuinoa Yanga.

Sisi Dimba tunayaona maendeleo haya ni makubwa hasa kwa klabu hii changa iliyoasisiwa mwaka 1972, ikijulikana kama Mto ya Singida na baadaye kubadilisha jina na kuwa Singida United, ambayo kwa kasi kubwa inaziacha klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zilizoasisiwa miaka ya 1935 na 36.

Kwetu sisi tunatoa pongezi za dhati kwa wamiliki wa klabu hiyo, kwanza kwa mikakati inayotimia lakini kwa malengo yao ya muda mfupi yanayoonekana kwenda na kasi inayoridhisha.

Tumeona jinsi ahadi ya timu hiyo kutumia uwanja wake wa nyumbani ilivyotimia, lakini hata mipango sahihi ya uwekezaji ambapo hadi sasa klabu hiyo ina wadhamini mbalimbali wakiwamo SportPesa, Oryx, YARA na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mkurugenzi wa klabu hiyo, Festo Sanga, idadi hiyo inaweza ikaongezeka.

Ndiyo maana tunazishauri klabu za Simba na Yanga kuangalia mafanikio haya yanayokuja kasi na kujifanyia tathmini wajione walipojikwaa ili ikiwezekana, wajirekebishe na kuyatafuta maendeleo ya kweli yasiyokuwa na sura ya ubabaishaji.

Kwa kipindi kirefu sasa tumesikia kauli mbalimbali zinazobainisha nia ya klabu hizo kujenga viwanja vyake, ambapo Simba imepiga kelele zaidi ya miaka mitatu sasa juu ya ujenzi wake wa Uwanja wa Bunju, ilihali wenzao Yanga kila kukicha taarifa mpya za ukarabati wa Uwanja wa Jangwani zinabadilika.

Tunatarajia kuiona Singida United ikifuata nyayo za Azam FC kwa kuboresha uwanja wake na kuweka miundombinu mingine ili hizi klabu za Simba na Yanga ziweze kujiona jinsi zilivyochelewa, pengine zinaweza kurejea katika mstari na kuanza upya safari yenye malengo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.