HE! MOYES AFUKUZWA WEST HAM KABLA HAJAANZA KAZI

Dimba - - Jumatano -

LONDON, England KAMA unafikiri una mikosi kwenye maisha yako, ni vyema ukatulia na kumtazama kwanza David Moyes na majanga anayoyapitia.

Baada ya uongozi wa West Ham United kumtimua Slaven Bilic, taarifa zinaonyesha kuwa ‘the Chosen One’, David Moyed, ndiye atakayepewa kibarua na kuinusuru klabu hiyo na mwenendo mbovu walioanza nao ligi msimu huu.

Lakini ikiwa bado suala hilo halijawekwa rasmi na uongozi wa West Ham, tayari mashabiki wa Wagonga nyundo hao wa London, wameanzisha kampeni ya kutaka Moyes anyimwe dili hilo.

Kampeni hiyo imeendeshwa kupitia mitandao ya kijamii ya mashabiki wa klabu hiyo, wakiwashikiniza viongozi wao kuachana na mpango wa kumpa kazi Moyes kwa madai kuwa kocha huyo ana nuksi.

Ili kutaka kujua ni wangapi wanaunga mkono na wangapi wanapinga, mashabiki hao waliweka mjadala wa ‘Namtaka Moyes vs Simtaki Moyes’.

Kati ya mashabiki 5,491 waliopiga kura, asilimia 90 waliunga mkono suala la kocha huyo wa zamani wa Sunderland na Manchester United, kutopewa kazi.

Pia mashabiki hao walikumbushia utovu wa nidhamu aliouonyesha Moyes mwaka jana baada ya kutishia kumnasa makofi mwandishi wa BBC aliyemhoji juu ya uwezo wake wa kufundisha.

Lakini baadaye Moyes alikiri kuwa alifanya makosa na kukubali kulipa faini ya pauni 30,000 aliyopigwa na chama cha soka.

Bilic alitimuliwa Jumatatu baada ya kuiongoza West Ham kushinda michezo miwili tu kati ya 11 waliyocheza msimu huu, huku klabu hiyo ikiwa kwenye nafasi tatu za chini katika msimamo wa EPL.

Baadhi ya mashabiki wa West Ham walikwenda mbali na kutishia kutokwenda uwanjani katika michezo iliyobaki kama uongozi utampa Moyes timu.

Tangu aondoke Everton mwaka 2013, baada ya miaka 11 ya mafanikio na klabu hiyo, Davis Moyes amekuwa akipata wakati mgumu katika klabu anayoifundisha.

Baada ya kupewa Man United ili kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson, Moyes alitimuliwa Old Trafford kabla hajamaliza msimu wake wa kwanza.

Mkosi huo uliendelea hata alipopewa kazi ya kuinoa Real Sociedad ya Hispania, kabla ya kurejea England na kuishusha daraja klabu ya Sunderland.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.