Stars vitani Benin bila Samatta

Dimba - - Mbele - NA EZEKIEL TENDWA

TIMU ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Star’, leo inashuka katika Uwanja wa l'Amitie, kuwakabili wenyeji wao Benin, bila kuwa na nahodha wao Mbwana Samatta, kutokana na majeraha yanayomkabili, ukiwa ni mchezo wa kirafiki wa Kimataifa unaotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Mchezo huo ambao unatarajiwa kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam TV, ni muhimu kwa Stars kushinda, ili kujisogeza juu kidogo kwenye ubora wa viwango vya Fifa.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza wa kirafiki kuchezwa ugenini, tangu kocha Salum Mayanga kukabidhiwa majukumu ya kuinoa timu hiyo Januari 2, mwaka huu, akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Charles Mkwasa, ukiacha michezo ya COSAFA nchini Afrika Kusini.

Mayanga amesema licha ya kwamba watamkosa nahodha wao, Samatta, kutokana na majeraha yanayomkabili, anaamini wachezaji waliobakia watapambana kupata matokeo mazuri.

"Ninaamini utakuwa mchezo mzuri kwa pande zote, sisi tutamkosa nahodha wetu Mbwana Samatta, lakini ninawaamini wachezaji waliopo kwamba watapambana ili kupata matokeo mazuri, licha ya kwamba ni mchezo wa kirafiki lakini ni muhimu kushinda,” alisema.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Oktoba 12, 2014, ambapo Stars waliibuka na ushindi wa mabao 4-1, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, mabao ya Stars yakipachikwa wavuni na nahodha wa wakati huo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu na Juma Luizio, huku lile la Benin likifungwa na Suanon Fadel.

Katika viwango vya Fifa, timu yetu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, inashika nafasi ya 136, huku Benin wakishika nafasi ya 79, hiyo ikimaanisha kwamba Stars wanakutana na wababe wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.