OMOG AWAZIDI KETE PRISONS

Dimba - - Mbele - NA SAADA SALIM

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ni kama amewazidi ujanja Tanzania Prisons, baada ya kutamka wazi kwamba, amewasoma vizuri na kilichobakia ni kuwashushia kipigo katika mchezo wao utakaochezwa wiki ijayo.

Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa wageni wa maafande hao wikiendi ijayo, timu hizo zitakapokutana katika mechi ya Ligi Kuu Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, ambapo kila timu inatamba kuondoka na pointi zote tatu.

Simba wapo Sumbawanga, mkoani Rukwa, wakicheza baadhi ya mechi za kirafiki, kujiweka sawa kwa mchezo huo ambapo Omog amesema anaendelea kuwasoma wapinzani wao hao kupitia baadhi ya CD.

Akizungumza na DIMBA kwa njia ya simu jana, Omog alisema anaifahamu vizuri Prisons kutokana na historia yake msimu uliopita, na ndiyo maana amelazimika kutafuta baadhi ya mechi zake, ili kuangalia mbinu kupitia CD, zitakazoifanya timu yake kuibuka na ushindi ili iweze kuibuka na pointi tatu muhimu katika mchezo huo.

"Prisons ni timu nzuri, hii ni moja ya zile timu zilizosababisha msimu uliopita tukakosa ubingwa, hivyo lazima tujiandae haswa, kwa ujumla nawafuatilia sana, kwani nataka kuhakikisha Simba inaondoka na pointi tatu siku hiyo," alisema.

Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanakuwa kileleni mwa msimamo mpaka ligi itakapomalizika, hali itakayowafanya kutwaa ubingwa na kuwatimulia vumbi wapinzani wao wa jadi, Yanga.

Katika msimamo wa ligi Simba wanaongoza, wakiwa na pointi 19, sawa na Azam FC, inayoshika nafasi ya pili, timu hizo zikipishana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17 sawa na Mtibwa Sugar, iliyopo nafasi ya nne, nazo zikipishana kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.