'HALA MADRID!'

MADRID WALISHAMSAJILI NEYMAR AKIWA BARCA

Dimba - - Jumapili -

KABLA ya Jorge Mendes, Mino Raiola na Pini Zahavi, kushika chati, alikuwepo bwana mmoja anayeitwa Wagner Ribeiro.

Wabrazil wanapenda kumuita “procurador problema” (Wakala msumbufu).

Huyu ndiye mfanyabiashara anayechukiwa zaidi Brazil. Kwanini? Nitakwambia.

Agosti 7, 2012, katika kiwanja cha ndege cha Manchester, kinachoshika nafasi ya tatu kwa kupokea wafanyabiashara wengi nchini Uingereza, Wagner Ribeiro alikuwa mmoja wa wageni waliowasili siku hiyo.

Hakuwa na biashara nyingine iliyomleta Manchester zaidi ya ile iliyompa umaarufu mkubwa duniani. Kusimamia dili za wachezaji.

Safari hii alikuja kushughulikia uhamisho wa Lucas Moura kwenda Manchester United. Kila kitu kilionekana kukamilika. Alisubiriwa yeye tu.

Kasi, nguvu, akili ya mpira ni miongoni mwa vitu vilivyomfanya Moura awe kipepeo kwenye mboni za Sir Alex Ferguson. Alimkubali mno.

Zaidi ya watu 96,000 waliofika katika dimba la Old Trafford, kutazama mchezo wa nusu fainali ya Olympic, kati ya Brazil dhidi ya Korea Kusini, waliamini Moura ni mchezaji mpya wa United.

Ajabu. Masaa 24 baadae, Agosti 8, 2012, Wagner alikuwa akiondoka Manchester huku PSG wakitangaza kumsajili Moura kwa Euro mil 45!

Nini kilitokea? Mtu wa kwanza kuulizwa juu ya hili ni Ferguson, naye hakuwa na jibu zuri zaidi ya kusema ‘mimi sio mpumbavu wa kutoa Euro mil 45, kwa kijana wa miaka 19’.

Baadae nyuma ya pazia iligunduliwa kuwa Wagner alikuwa kwenye meza ya mazungumzo na United huku akiwa bize kusoma meseji za matajiri wa PSG.

Inadaiwa Wagner, alivuta pauni mil 20 kutoka kwa PSG kwa kazi nzuri ya kuwageuka Man United. Old Trafford ikabaki na kilio.

Nilikwambia awali, Ribeiro ndiye mfanyabiashara anayechukiwa sana Brazil. Ushawishi wake wa pesa, umewafanya vijana wengi kukimbia nchini humo na kwenda kusaka malisho barani Ulaya.

Julai 2005 alikuwa akifanya dhambi isiyosameheka mpaka leo kwenye mioyo ya Wabrazil, baada ya kukamilisha uhamisho wa Robinho kutoka Santos, kwenda Real Madrid.

Ndio siku hii ambayo Wabrazil wanaamini Robinho alimaliza mapenzi yake na mpira na kuanza kuwa mtumwa wa pesa.

Sote tunajua kilichomtokea Robinho, ila hatujui kuwa dili hili ndio lililotengeneza urafiki wa karibu kati ya Wagner na Rais wa Real Madrid, Florentino Perez.

Tangu hapa, Wagner akawa mfanyakazi wa Perez kwa kuhakikisha wachezaji wenye vipaji kutoka Brazil wanatua Real Madrid.

Miaka minne baadae. Juni, 2009, Ricardo Kaka alitua Santiago Bernabeu kwa ofa ya Euro mil 67. Ndio, Wagner alikuwa wakala wa Kaka na rafiki wa Perez, unategemea kipi cha zaidi?

Ahadi pekee ambayo Wagner hajaitekeleza mpaka leo kwa Perez, ni ile ya kuhakikisha Neymar anavaa uzi wa Real Madrid.

Hili pekee ndio linalompasua kichwa Wagner mpaka leo na ndio vita hii iliyomfanya aongeze maadui wengine kutoka Barcelona.

Manchester United hawampendi kwa alichowafanyia kwa Moura, Chelsea hawampendi kwa uhuni aliowafanyia kwa Robinho, ila Barcelona wanamchukia kwa mengi Wagner. Nitakwambia.

Turudi nyuma kidogo kwenye historia ya Neymar. Akiwa na miaka 16, aliwahi kumwambia Phillippe Coutinho kuwa ndoto yake ni kucheza Real Madrid, siku moja.

Mwaka 2005, Wagner aliyekuwa wakala wake, aliitimiza robo ya ndoto yake kwa kumsafirisha mpaka Bernabeu kwa ajili ya kufanya majaribio.

Neymar alikaa katika mji wa Madrid kwa siku 19, akijifua na timu ya vijana. Alizungushwa Bernabeu na kupiga picha na magwiji wa Kibrazil waliokuwa pale, Ronaldo de Lima na Roberto Carlos.

Alipohitaji kutazama mechi, Perez alimbeba hadi kwenye chumba maalumu cha VIP na kuketi naye. Neymar akaiona pepo yake akiwa hai.

Baadae akarudishwa Brazil baada ya baba yake kushauri kuwa bado kijana wake hajafika umri wa kucheza Ulaya.

Mwaka 2011 tena, Neymar alirudi Madrid kwa ajili ya kupimwa afya. Ilionekana ndoto yake inakaribia kutimia.

Lakini ukubwa wa kikosi cha Madrid wakati ule, wakiwa na Kaka, Benzema, Ronaldo, Mesut Ozil, Angel Di Maria, ukampa hofu nyingine baba yake. Akashauri Neymar arudi tena Santos.

Miaka miwili baadae, akatua Barcelona. Inaaminika Barca walishinda vita hii baada ya kumpa pesa nyingi za udalali baba yake Neymar. Likawa pigo kubwa kwa Perez na Wagner.

Tangu hapo, licha ya Neymar kuachana na Wagner, baada ya kukutwa na hatia ya ukwepaji kodi nchini Brazil, wakala huyu hakuacha kuisumbua Barcelona.

Aliwatikisa kila uchwao. Moyoni mwake aliamini ana sababu ya kuwalipizia kisasi kwa usaliti waliomfanyia.

Ni lazima Neymar aondoke Nou Camp. Hii ikawa kazi yake ya kwanza. Na asitokee tena kijana mwingine wa Kibrazil, kwenda pale. Hii ilikuwa kazi yake ya pili.

Bila shaka unajua kilichowatokea Barca kwa kinda Vinicius Junior. Licha ya kutoa ofa kubwa kwa Flamengo, Vinicius alisaini mkataba wa bei chee wa Real Madrid.

Kwanini? Usiumize kichwa sana. Ribeiro yuko kazini. Yeye ndiye wakala mwenye ushawishi mkubwa zaidi Brazil, ni rahisi kusema jambo na mawakala wenzake wakamsikiliza.

Neymar bado yupo Barcelona? Jibu ni hapana. Ameshajiunga na PSG. Ilikuwaje? Jibu ni rahisi pia, Ribeiro alikuwa kazini.

Licha ya kuchukua pauni mil 24, pindi Neymar aliposaini mkataba mpya na Barcelona, baba mzazi wa Neymar, amefichua kuwa Ribeiro ndiye aliyeleta wazo la PSG mezani kwake.

Na alileta wazo lililokamilika. Kutoka mwanzo mpaka mwisho. Alijua Neymar atalipwaje na PSG na ataondokaje Barcelona. Kwanini watu wa Catalan wasimchukie bwana huyu?

Mpaka sasa ameshamaliza kisasi chake na Barca, kilichobaki ni kutimiza ndoto yake ya kumpeleka Neymar ndani ya dimba la Santiago Bernabeu.

Tuendelee kufatilia sinema hii ya Neymar na PSG, lakini tusisahau kuwa, Ribeiro yuko kazini akiipambania ndoto yake.

Wabrazil hawakukosea walipomuita, ‘procurador problema’.

Na Ally Kamwe 0655 321415 'Nifollow Insta' Instagram: Kamwejr kamweally@yahoo.com

FAIR PLAY

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.