Stars bila Samatta inawezekana tu

Dimba - - Jumapili - NA MAREGES NYAMAKA

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, analazimika kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita, baada ya kupata majeraha wakati akiitumikia klabu yake.

Samatta aliumia hivi karibuni, katika mechi ambayo timu yake ya KRC Genk ilikuwa ikiikabili Lokeren, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, uliomalizika kwa timu hizo kutoka suluhu.

Katika mchezo huo, Samatta alidumu uwanjani kwa muda wa dakika 40, kabla ya kutolewa nje baada ya kuumia.

Samatta, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, hatakuwamo kwenye kikosi cha Stars kitakachocheza mechi ya kirafiki ugenini leo Jumapili dhidi ya Benin, mchezo unaotambuliwa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa).

Baada ya jopo la madaktari wa klabu ya KRC Genk kugundua jeraha la Samatta ni kubwa, uongozi wa klabu hiyo ulilitaarifu Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwa nyota huyo atafanyiwa upasuaji wa goti na hivyo hataweza kuwa kwenye mipango ya kocha Salum Mayanga.

Hii ni mara ya kwanza kwa Samatta kukumbwa na majeraha ya muda mrefu zaidi, tangu aanze kucheza soka barani Ulaya.

Ilikuwa ni taarifa ya simanzi kwa kila Mtanzania, hasa wadau wa soka, kutokana na umuhimu wake katika kikosi cha timu hiyo kama mchezaji tegemeo, akiwa ndiye nyota pekee anayecheza timu ya daraja la juu barani Ulaya.

Hata hivyo, wadau wa soka wanapaswa kufahamu kuwa, huu ni wakati wa kuondokana na unyonge wa kushika tama na kubali kilichotokea, kwani hilo ni jambo ambalo haliepukiki michezoni.

Kinachopaswa kufanywa ni mambo mawili muhimu, kumuombea Samatta apone mapema ili arejee mapema uwanjani, lakini pia kuamini wachezaji waliopo wanaweza kutuvusha kupata matokeo bora mbele ya Benin.

Kama hiyo haitoshi, Stars pia inakabiliwa na mashindano makubwa ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2019, nchini Cameroon, ambapo nahodha huyo anahitajika mno kuweza kutuvusha, ambapo Stars iliyoko kundi L pamoja na timu za Uganda, Lesotho pamoja na Cape Verde, itaendelea na kampeni yake ya kusaka tiketi mwezi Machi, hiyo ikiwa ni miezi miwili baada ya yeye kurejea uwanjani. Ikumbukwe pia kuwa, hii si mara ya kwanza Samatta kukosa kwenye kikosi hicho cha Stars, hususan katika miezi ya hivi karibuni, chini ya Kocha Salum Mayanga.

Moja ya michuano ambayo nahodha huyo alikosekana ilikuwa ni katika mashindano ya Cosafa, yaliyofanyika nchini Afrika Kusini, lakini timu ilionyesha uwezo bila uwepo wake.

Rekodi zinaonyesha kuwa, kwa miaka ya karibuni, katika michuano hiyo, ambayo kitambaa kilivaliwa na Himid Mao, ndipo Stars ilipofanya vizuri sana na kuweka historia ya aina yake.

Ilikuwa ni mara ya kwanza Stars kufika nusu fainali ya michuano hiyo tangu kuanzishwa kwake, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ilikuwa ikiongozwa na Elias Maguli, Simon Msuva na Shiza Kichuya na waliweza kuifikisha hadi kushika nafasi tatu na kutwaa kitita cha dola za Kimarekani 10,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 23) na kutwaa medali ya shaba.

Pia wachezaji Shiza Kichuya, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin na Elias Maguli walirejea na tuzo za wachezaji bora, huku tuzo ya jumla ikienda kwa kipa Said Mohamed 'Nduda', aliyeibuka mlinda mlango bora wa mashindano.

Vilevile ilikuwa chachu kwa Msuva, ambaye dili lake la kutimkia nchini Morroco anakokipiga hivi sasa katika klabu ya Difaa El Jadida liliiva, baada ya mawakala kuthibitisha uwezo wake.

Hiyo ilikuwa taswira tosha kuwa wachezaji wa timu hiyo wanaweza kujituma na kupiga hatua kutoka moja kwenda nyingine bila hata ya kuwa na nahodha wao, Mbwana Samatta.

Kama hiyo haitoshi, Stars pia inakabiliwa na mashindano makubwa ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2019, nchini Cameroon, ambapo nahodha huyo anahitajika mno kuweza kutuvusha, ambapo Stars iliyoko kundi L pamoja na timu za Uganda

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.