MSONDO NGOMA WATAKA FIDIA MIL 300 KWA WCB

Dimba - - Jumapili -

HABARI ambazo zimesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ni kutokana na barua ya wanasheria iliyosambaa ikionyesha kwamba Band ya Msondo Ngoma inataka kundi la WCB linaloongozwa na Diamond Platnumz liwalipe milioni 300.

Barua hiyo iliyopelekwa pia Basata na Cosota, inasema milioni 300 hizo wanazidai kama fidia kutokana na WCB kutumia bila ruhusa melody yao katika wimbo wa Zilipendwa ambayo ni ya wimbo wa Msongo Ngoma.

KESI YA HAMISA MOBETO YAFUTWA

MWANAMITINDO Hamisa Mobeto, amekwaa kisiki mbele ya Diamond Platnumz, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa watoto kutupilia mbali kesi aliyofunguliwa ikimtaka mwanamuziki huyo kutoa matunzo ya mtoto, Prince Abdul.

Diamond aliwasilisha pingamizi dhidi ya kesi hiyo iliyofunguliwa na Mobeto akidai kuwa kesi hiyo imefunguliwa kwa kutumia kifungu ambacho si sahihi. Hoja ambayo ilipingwa na Mobeto ambaye ameomba matunzo ya mtoto waliozaa na msanii Diamond.

Kupitia hati hiyo ya madai, Mobeto anaomba Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake na Diamond aliwasilisha hati ya majibu hayo kinzani akipinga maombi hayo ya Mobeto akidai gharama anazodai kulipwa kwa mwezi ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hawezi kuzimudu.

SANCHIWORLD AVUNJA UKIMYA

MMOJA wa wanadada wenye figa kali Afrika Mashariki, Sanchi World, ameamua kuvunja ukimya juu ya kile wanachosema mashabiki wengi kuwa umbo lake linatokana na mwanadada huyo kutumia dawa za kuongeza makalio maarufu kama Mchina.

Lakini wiki hii mwanadada huyo amevunja ukimya huo na kueleza kuwa yeye ni halisi baada ya kupost picha ya mama yake ambaye anasema ameridhi umbile lake kutokwa mwa mzazi wake. …. ‘Mama yangu ni malkia wa miamba, mimi ni mtoto wa malkia….’

PENZI LA WOLPER NA BROWN LARUDI KWA KASI

BAADA ya kudaiwa staa wa Bongomovie, Jackline Wolper na mpenzi wake, Brown, penzi lao kuingiliwa na mdudu huku kila mmoja akishindwa kumpost mwenzake, sasa mambo yamefika pazuri.

Kupitia akaunti ya Instagram, Wolper alitupia picha akiwa na Brown kwenye mahaba mazito huku akiandika swali la mtego kwa mpenzi wake huyo, ‘siwezi kujaribu midomo yangu, unaweza kufanya kwa ajili yangu?’ Mashabiki mbalimbali walitumia nafasi hiyo kupongeza kurejea kwa amani katika uhusiano huo.

UJUMBE WA SAMATTA KWA MASHABIKI BAADA YA UPASUAJI

MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta, anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji leo hatakuwepo kwenye kikosi cha Stars kitakachovaana na Benin baada ya kuumia akiitumikia klabu yake ya Genk, huku akitumia mtandao wake kuelezea maendeleo ya afya yake.

Kupitia akaunti yake, Samatta aliweka picha akionekana yupo hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji na kuandika: ‘Napenda kuwajulisha kuwa operesheni yangu imekwenda vizuri...napenda kumshukuru Mungu, timu ya madaktari pamoja na mashabiki wangu. Nimepokea jumbe nyingi kutoka sehemu mbalimbali duniani, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa dua zenu.’

MANARA YUPO DUBAI ANAKULA ZAKE BATA

AKAUNTI ya msemaji wa Simba kila wakati haikauki vituko, mapema mwishoni mwa wiki hii ametupia picha mbalimbali zikimwonyesha akiwa katika maeneo tofauti mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu akidai anakula ‘bata’ na kupumzisha akili yake.

Manara alipost picha ikimwonyesha yupo ndani ya ndege aina ya Emirates na kuandika… ‘Unapopata muda kidogo...Dubai moja for weekend kidogo.’

BEN POL APATA SHAVU UFARANSA

MSANII wa miondoko ya R&B, Bernard Paul maarufu kama Ben Pol, yupo nchini Ufaransa ambapo amekwenda kwa ajili ya utambulisho maalumu wa kuwa balozi mpya wa Kampuni ya Maua Associations.

Kupitia ukurasa wake, Ben Pol, aliwatambulisha Watanzania kwa kuandika.. ‘Jana niliwasili Paris kwa ajili ya kuhudhiria hafla maalumu iliyoandaliwa na taasisi ya Maua Association itakayofanyika Nov 18 na itaambatana na utambulisho rasmi wa Ben Pol kama balozi mpya.’

NA JESSCA NANGAWE

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.