Ilipigwa na Ghana nyumbani 1999

Dimba - - Jumapili - NA HENRY PAUL

TANZANIA ilionesha kuwa wanyonge mbele ya timu za Afrika Magharibi wakati ilipokubali kufungwa mabao 2-1 nyumbani na timu ya Taifa ya Ghana, (Black Stars) katika mechi ya marudiano michuano ya awali ya soka Olimpiki.

Mechi hiyo, ambayo timu ya Stars ilionekana kuzidiwa kiuwezo na timu ya Taifa ya Ghana, ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, siku ya Jumamosi Juni 27, 1999.

Stars katika mchezo huo ilionesha uwezo mdogo wa kuipenya ngome ya adui kupachika mabao na kubadili mchezo, tatizo lililoonekana kuwa kizingiti kikubwa cha vijana hao wa Tanzania, ambapo katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Accra, Ghana wiki mbili kabla, walifungwa kwa idadi kama hiyo ya mabao 2-1.

Kutokana na Stars kufungwa katika mchezo huo wa pili, kuliwafanya Waghana wafuzu kuingia katika hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2. Hatua ya makundi ya kutafuta nafasi ya kucheza michezo ya Olimpiki, ilifanyika Sydney, Australia mwaka 2000.

Ilikuwa ni simanzi kubwa kwa Watanzania ambao siku hiyo walionekana kuwa wamejiandaa kushangilia timu yao kwa nguvu zote, lakini walianza kupiga kelele za kukerwa na baadhi ya matukio yaliyokuwa yakionekana uwanjani katika dakika 20 tu za kwanza.

Pasi nyingi za Stars zilinaswa kirahisi na Waghana wakati wachezaji wengine walitumia muda mwingi kukaa na mpira na hivyo kuwapa nafasi Waghana kujipanga na baadaye kupokonya mpira kirahisi.

Mkakati wa kushambulia muda wote ulizimwa na Waghana, ambao walishambulia lango la Tanzania kwa muda mwingi kana kwamba walikuwa nyumbani.

Mara baada ya mchezo kumalizika, wachezaji wa Stars walijiinamia katika benchi lao na wengine kukaa uwanjani huku baadhi wakilia, kitendo kilichomfanya Waziri Mkuu wa wakati ule, Frederick Sumaye, kwenda kuwapa pole kabla ya kuondoka.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, matokeo yalikuwa ni sare ya bila kufungana.

Katika mchezo huo, wageni Ghana walipata bao la kwanza baada ya kipindi cha pili kuanza, bao lililofungwa kwa kichwa na Joseph Fameyed, kutokana na makosa ya kiungo mkabaji Renatus Njohole kushindwa kuondoa mpira wa pasi ndefu uliopigwa golini na kumkuta mfungaji.

Baada ya Stars kufungwa bao hilo walichachamaa na kuanzisha mashambulizi makali langoni mwa timu ya Ghana, ambapo mashambulizi hayo yalizaa matunda, kwani dakika tatu baadaye ilisawazisha bao lililofungwa na Steven Mapunda ‘Garrincher’, aliyewahi mpira uliopigwa na beki Issa Kassim, ambaye alicheza vizuri siku hiyo.

Bao la ushindi la Ghana lilifungwa na winga wa kushoto, Bashiri Gambo, katika dakika ya 76, kutokana na makosa ya beki wa kulia, Kassim Issa. Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika, timu ya Taifa ya Ghana ilitoka uwanjani kifua mbele baada ya kuifunga Taifa Stars mabao 2-1.

Kikosi cha Taifa Stars kiliwakilishwa na kipa Adrian Mohamed, Kassim Issa, Mridi Ally, Omary Kapilima, Ally Mayay, Renatus Njohole, Steven Mapunda ‘Garincha’/Ephrahim Makoye, Abubakar Mkangwa, Wilfred Kidau (Sasa ni Katibu Mkuu wa TFF), Mnenge Suluja, Lameck Sichula, Abdallah Saleh na Victor Kilowoko.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana kiliwakilishwa na kipa Osei Boatey, Fred Yoboalt, Issalt Abdulrhaman, Wagaba Sam/Lanatey Lemki, Kofi Amoako, Hamza Mohamed, Aziz Ansalt, Johnson Eleu, Joel Sam/Abdul Razak, Joseph Fameyeh, Ali Kwame na Bashir Gambo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.