NAMCHUKIA MUME WANGU (16)

Dimba - - Jumapili -

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA... “Vitabu vya dini vinatufundisha kusamehe, msamehe mwenzako mara saba sabini, nimekusamehe kutoka moyoni, kuwa na amani my dear...,” nilimwambia, nikawaomba wazazi wangu wamshike mikono Saimon na kumsamehe. Mama alimshika mkono kwasababu ya kauli yangu, ingawa alimpa mkono huku amemkunjia uso, baba hakutaka kumpa mkono, nikawaomba tena kwamba kama hawatamsamehe, nitajiua, nikawaomba wamsamehe. Walilazimika kumsamehe! Tukashikana mikono ya heri, tukicheka pamoja, ingawa vicheko vingine vilionekana vya bandia. SASA ENDELEA NA MKASA HUU WA KUSIKITISHA!

“Ahsante, nashukuru kunisamehe...,” aliniambia.

“Nami pia, nashukuru moyo wangu umekusamehe! Sitaki kutenda dhambi, nimeokoka!” Nilisema nikitabasamu. ***** Baada ya kusameheana na Saimon, nilirejea nyumbani na familia yangu, kila nilipokumbuka tukio la kuingiliwa kimwili nililia sana bila kusema sababu ya kilio changu. Mara nyingi nimekuwa nikijifungia chumbani kwangu na kulia muda mrefu, nilipomaliza nilijifuta machozi na kutoka chumbani.

“Rose, mbona macho mekundu, una tatizo gani?” Mama aliniuliza akiniangalia kwa macho ya udadisi.

“Macho yanawasha! Sijui tatizo ni nini?”

“Sio kuwa ulikuwa ukilia?” Mama alinishtukizia, ingawa niligoma kusema ukweli.

“Hapana mama, niko poa!” Nilijibu.

“Sawa mwanangu, ila kuwa makini... kama una tatizo lolote kubwa, naomba uniombe ushauri, nitakusaidia mawazo, umenielewa Rose... kitu chochote unachokiwaza akilini mwako, ukihisi kinakusumbua, naomba uniambie...naelewa mambo mengi ya kidunia...” “Nitakuambia mama...” “Ehee, lakini hebu niambie ukweli, Saimon umemsamehe kutoka moyoni? Na unampenda sana?”

“Nimemsamehe na nampenda sana,” wakati nikijibu maswali ya mama, nilijikuta nikitokwa na machozi, mwili ukaanza kutetemeka kwa hasira ambayo sikuelewa vizuri. Ilionekana nilikuwa nikipingana na vitu kichwani mwangu, moyo uligoma kabisa kumsamehe Saimon, wakati mwili ulishindwa kabisa kuona au kusikia habari hizi za Saimon.

“Mbona unalia, Rose kuna kitu unanificha...” “Hakuna mama!” “Sasa mbona unalia wakati nimekuuliza maswali kuhusiana na huyo mumeo unayedai unampenda sana, eeeh!” Mama alizidi kunitia simanzi moyoni, ukweli sikuwa na uwezo kila nilipokumbuka madhambi niliyofanyiwa na mwanamume.

Nilikwenda kazini kama kawaida kufuatilia masuala yangu ya safari ya China iliyoandaliwa na ofisi yetu kuwa niende kusomea mafunzo ya kijeshi ya taifa hilo lenye wajuzi wengi na wataalamu wa mambo ya mabomu! Nilipofika ofisini, nilisaini na kwenda kuonana na mkuu wangu jeshi katika kitengo changu, alikuwa ameketi ofisini.

Nilimpigia saluti, akanijibu na kunionyesha niketi kiti kimoja katika viti vitatu vilivyokuwa tupu.

“Rose! Mbona hujachangamka...unaumwa?”

“Afadhali ningekuwa naumwa ningeweza kunywa japo dawa nikapona, nina mawazo!” “Mawazo gani?” “Ni muda wa mwaka sasa, tangu niachane na mume wangu...najikuta nikimuwaza sana...”

“Pole sana, Rose unafahamu nakupenda sana, tangu niachane na mke wangu ni miaka mitatu...”

“Uliachana na mkeo miaka mitatu iliyopita?”

“Ndiyo, ndoa yetu ni ya Kikristo! Tumetengana ila kwangu tumeachana kabisa, simhitaji hata kidogo!” “Kwanini?” “Alitembea na bosi wake, roho inaniuma sana...”

“Anafanya kazi gani huyo bosi wake...”

“Ni kijana mmoja, mfanyabiashara...alimwajiri mke wangu katika ofisi yake, hivyo akatumia cheo chake cha ubosi na kufanikiwa kumteka mke wangu, hiki ndicho kilichonifanya niachane naye, maana ndoa ilikuwa sio ndoa, ugomvi kila siku na mke wangu, maisha yakageuka jiwe pamoja na kwamba nina cheo kikubwa jeshini...”

“Una picha yake nimuone huyo kijana aliyetembea na mkeo?” Nilimuuliza akimwangalia Kanali. Nilichukia sana kuona watu ambao si waaminifu katika ndoa zao, katika maisha yangu sikupenda mtu mzinzi wala mwasherati.

“Ninayo, subiri nikuangalizie...ipo kwenye droo yangu...,” alisema Kanali Peter Osugara, mtaalamu wa kuyategea mabomu, kutengeneza na kuyarusha, zamani kabla hajahamia Dar es Salaam, alikuwa kikosi cha Mzinga Morogoro, ambapo alifanya kazi zake za kijeshi na hatimaye akafuzu na kupandishwa cheo. Kitendo cha kumfumania mkewe akifanya mapenzi na bosi wake, kilimchanganya sana. Aliwachukia wanawake na kuwaona hawana msaada wowote katika maisha yake, alibaki na watoto wake akiishi nao na mama yake mzazi.

Dakika mbili, aliinuka na kwenda kwenye droo moja pale ofisini kwake akatoa picha mbili, akaniletea na kuzitupa pale mezani.

“Dah! Kamanda...Bosi wangu...huu ni udhalilishaji...namjua huyu mtu...” “Unamjua?” “Ndiyo, ni mshenzi sana... namjua...” “Anaitwa nani?” “Saimon Mota...” “Kweli, umemfahamia wapi?”

“Nimeshawahi kufanya kazi kwake, na pia alinitenda maana ndiye aliyekuwa mume wangu...” “Hapana, unasema kweli!” “Ndiyo, namjua kabisa...” “Safi sana, kama unamjua jambo jema, hebu keti chini,” Kanali Peter alisema, nikaketi moyo ukiugua na kuungua. Sikuwa na furaha, nilimchukia sana Saimon Mota, hata kumsamehe haikuwa kweli kuwa nimemsamehe, nilichokuwa nakitaka ni kufanya kila linalowezekana niweze kumwangamiza.

“Huyu kijana nimemtafuta sana bila mafanikio, namba zake za simu amebadilisha kabisa!”

“Ninazo, usiwe na shaka... unataka tufanyeje?”

“Mimi nipo tayari kusimamisha safari yako kwa muda mfupi, tufanye kazi moja.” Kanali Peter alisema kwa sauti ndogo aliyohakikisha haivuki kuta za ofisini kwake, kwani jambo hilo lingeweza kumhatarishia kazi yake.

“Umefanya jambo jema bosi!” alisema. Rose alipewa maelekezo yote, akapewa na bastola ndogo ya Kanali, aliyoambiwa lazima awe makini katika suala hilo.

Mikakati ilifanyika baina ya watu wawili, nilimhakikishia ningeweza kufanya ukatili dhidi ya mume wangu nikiwa peke yangu, jambo ambalo mkuu wangu wa kazi aliliridhia, ingawa aliniambia angenisaidia ili kukamilisha zoezi hilo.

“Itabidi tumwangamize wote!”

“Poa...nimeelekezwa mpaka nyumbani kwake, napajua...,” nilimwambia Kanali, Peter .

Baada ya makubaliano yetu, tuliongozana na Kanali kwa ajili ya safari ya kumuona Saimon Mota, haikuwa safari ya furaha bali safari ya kulipiza kisasi, moyoni mwangu nilijipanga kuhakikisha nasuuza moyo wangu kwa kumwaga damu ya Saimon aliyenifanyia ukatili wa kutosha. Tulipofika Kinondoni Studio, tuliongoza taratibu na kukunja Barabara ya Mwananyamala, hatua chache tuliegesha gari kando ya barabara, gari letu lililokuwa na vioo vya tinted lilitufanya tuangalie nje kama tungeweza kumuona Saimon bila wasiwasi.

“Habari yako kaka,” nilimsalimia kaka mmoja niliyemuona ameketi dukani baada ya kushusha kioo cha gari.

“Salama, vipi kwema?” Aliuliza yule mwanamume.

“Ndiyo, ila sisi ni wageni, sijui unamfahamu Saimon Mota?”

“Namfahamu, nyumbani kwake ni hapo nyuma... nendeni na hiyo barabara, mkunje kushoto, utaona jumba lake,” alisema mwelekezaji wetu ambaye hatukumfahamu jina, nilianza kujiuliza maswali, kumbe jamaa alikuwa na nyumba nyingine nzuri. Maana mwelekezaji, alisema ‘jumba moja zuri!’.

Niliondoa gari mwendo mdogo baadaye tulikunja kushoto ambapo tuliegesha gari mbali kidogo, tukaanza kutembea kwa miguu hatua chache na kuliona hilo jumba lenyewe.

Tulisimama nje ya geti na kubonyeza kitufe cha kengele ambapo mlango mdogo wa geti ulifunguliwa, tukakutana na kijana wa Kimasai aliyeshika sime, fimbo na rungu kubwa huku akiwa amevaa rubega (mavazi ya Kimasai). “Habari yako Masai...” “Njema, niwasaidie nini wageni...”

“Sisi ni rafiki wa bosi wako Saimon Mota, sijui tumemkuta .... ”

“Amepumzika, labda mje baadaye...”

“Ahaa, unaweza kumjulisha kwamba tuna shida naye kwa sasa?”

“Hapana, atanitukana, hataki usumbufu hasa akiwa na mgeni mwanamke!” “Mgeni mwanamke!” “Ndiyo...” “Basi, tunaomba tumsubirie ndani,” alisema Kanali Peter. “Majina yenu kwanza...” “Naitwa Queen Masanja,” nilisema nikamgeukia Kanali Peter, “Naitwa James Badru!” Wote tulidanganya majina yetu. Masai akaridhia kwasababu alifahamu wazi kuwa wageni hao ni rafiki wa bosi wake.

Tulikaribishwa nje sehemu yenye bustani nzuri sana, tukaketi. Nilitoa mkoba wangu, kisha nikatoa mvinyo aina ya Robertson winery, tukamuita mlinzi akatuletea glasi, tukaanza kunywa, tukamuomba naye aweze kuonja, aliporidhia kabla ya kumimina, nilimwekea unga wa dawa za kulevya, akajikuta akipokea na kunywa. Hazikupita dakika nyingi, mlinzi wa Kimasai alishalala kwenye ukoka mzuri wa kisasa, tukainuka. Niliingia ndani, Kanali alibaki nje akiangalia mazingira, baadaye alinipigia simu na kuniita nje. “Vipi?” “Wapo chumba hiki, ngoja nipande juu dirishani niangalie kama ni yeye...” alisema Kanali Peter, akainuka na kuchungulia jirishani, akashuka akitetemeka huku jasho likimtoka mwili mzima.

“Vipi, mbona unatetemeka...”

“Saimon, yupo na mke wangu...”

“Achana naye, twende ndani...”

“Hapana, napiga risasi hapa hapa...” alisema Kanali Peter, na bila kufanya ujinga, alimimina risasi zote kichwani mwa mkewe pamoja na Saimon, alipohakikisha wamefariki dunia, alinishika mkono.

“Tukazing’oe kamera...,” alisema Kanali, nilitii sheria, tukaingia na kuzing’oa zile kamera zilizofungwa kwenye nyumba, kisha tukaondoka nazo zote pamoja na kompyuta zake. Hatukutaka kukamatwa kwa mauaji hayo. Sikuweza kuumizwa na kifo hicho, nilibaki mwenye furaha kuona Saimon ametangulia mbele za ahera. “Tummalizie mlinzi...” “Akibaki anaweza kututaja,” tulishauriana na kummalizia mlinzi.

Je, Saimon amesamehewa kweli? Nini kitaendelea? Tukutane wiki ijayo. Usikose kitabu changu cha NAMCHUKIA MKE WANGU, na KAFARA LA KISHETANI. Vinauzwa kila kimoja Tsh 4000 tu; kwa wauzaji wa magazeti nchi nzima. 0712313191 Zubagy Akilimia.

MTUNZI: ZUBAGY AKILIMIA SIMU: 0712313192

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.