BALE NDIO BASI TENA

Dimba - - Jumapili - MADRID, Hispania

WINGA wa Real Madrid, Gareth Bale, anatarajiwa kubaki nje ya uwanja kwa miezi michache iliyobakia ya mwaka huu baada ya kuumia msuli wa paja la kushoto akiwa mazoezini mapema wiki hii.

Bale hajaonekana tena dimbani tangu aifungie Madrid bao kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Borussia Dortmund mwishoni mwa Septemba, baada ya kuumia kigimbi cha mguu wakati mchezo huo ukikaribia kumalizika na kuzikosa mechi mbili za timu yake ya taifa ya Wales za kufuzu Kombe la Dunia.

Ni hivi karibuni aliripotiwa kurudi mazoezini, lakini baada ya muda mfupi akajisikia maumivu tena kwenye mguu wake wa kushoto mwishoni mwa mazoezi hayo.

Majeraha hayo ya Bale hayajaanza mwaka huu tu, kwani tangu atue Bernabeu mwaka 2013, winga huyo ameichezea Madrid mechi 159 tu na katika mechi 60 za mwisho kwa klabu yake, amekosa 40 kati ya hizo.

Ni changamoto inayokaribia kuharibu maisha mazuri aliyonayo winga huyo ndani ya klabu hiyo kongwe ya Hispania, ambapo majeraha hayo yamekuwa yakiibuka mara kwa mara na tangu aumie enka Novemba 22 mwaka jana, ameichezea Madrid mechi 20 tu.

Alipoumia enka, alikosa mechi 17 mfululizo. Akapona na kuumia tena, ambapo tatizo lingine lilimfanya akose mechi mbili, aliporudi dhidi ya Barcelona, akaumia tena na kukosa mechi nane.

Msimu huu alianza vizuri lakini baada ya kuivaa Dortmund Septemba 26, hajaonekana tena uwanjani na kuna kila dalili akakosa si pungufu ya mechi 10.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.