STARS ITUONYESHE MWANGA WA CHALENJI LEO

Dimba - - Jumapili -

TIMU ya soka ya Taifa Tanzania (Taifa Stars), leo itajitupa uwanjani kucheza mechi ugenini dhidi ya Benin, ikiwa ni mechi ya kirafiki iliyomo katika kalenda ya Fifa, lakini pia itakuwa ni rasmi kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Chalenji.

Timu hiyo tayari iko nchini humo tangu juzi ikifanya mazoezi, huku hali ya wachezaji ikielezwa kuwa ni njema, isipokuwa nahodha wake tu, Mbwana Samatta, anayekipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, ambaye alipata majeraha na kufanyia upasuaji, hivyo hakuwapo katika mechi hiyo.

Stars inatakiwa kushinda mechi hiyo ili iweze kupanda katika viwango vya Fifa, lakini pia itakuwa imepata mwanga kuelekea michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kufanyika Desemba na kushirikisha nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Sisi Dimba tunaitarajia mechi hiyo iwe ya ushindi kwa Stars, ili iweze kutupa matumaini ya kufanya vizuri katika michuano ya Chalenji, lakini pia itusogeze nafasi yetu kutoka mkiani mwa orodha ya Fifa.

Tunaamini hayo yanawezekana kama alivyoahidi Kocha Mkuu wa Stars, Salum Mayanga, lakini vilevile tunatiwa moyo na jinsi Ligi Kuu ya Tanzania ilivyozidi kuwa bora, kadhalika kuwapo kwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali duniani.

Ndiyo maana tunaungana na Watanzania wote kuiombea dua timu yetu ya Taifa, tukijua kwamba, ushindi wa leo dhidi ya Wabenin ni lazima.

Tunawaombea afya njema wachezaji pamoja na viongozi wa benchi la ufundi ili waweze kutuwakilisha vizuri Watanzania ili warejee na ushindi tunaoutarajia hii leo.

Kwetu wadau wa soka tunatakiwa tuendelee kuipa moyo timu yetu na hata kuipa misaada ya hali na mali ili tushirikishe nguvu zetu katika kutafuta maendeleo ya soka, tuliyoyakosa kwa miaka mingi.

Kadhalika tunayo imani kubwa kwa serikali ya awamu ya tano, hususan waziri anayehusika na michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba jitihada zake, ari anayowapa wachezaji pamoja na makocha itasaidia kurudisha heshima ya michezo nchini na hasa mchezo huu wenye idadi kubwa ya mashabiki.

Daima sisi tunaamini kwa pamoja tunaweza, kwani umoja ni nguvu na penye nia ipo njia, hivyo basi tuendelee kuiombea Stars na kuwapa moyo wachezaji ili waturudishie furaha iliyotoweka. Mungu ibariki Taifa Stars.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.